Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wallace Karia, ukongwe siyo ukubwa kwenye mpira

Wallace Kariaaaaa.jpeg Rais wa TFF, Wallace Karia

Tue, 18 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Juni 15, 2024, itaingia kwenye historia ya soka la Tanzania kwamba kitabu rasmi cha historia ya klabu kongwe zaidi katika zilizo hai hapa nchini, Yanga SC, kilizinduliwa.

Katika hafla hiyo iliyopendeza, Rais wa TFF, Wallace Karia alipata wasaa wa kusema machache, na akasema machache kweli lakini yaliyozaa mengi.

Pamoja na mambo mengine, Karia ambaye aliingia TFF mwaka 2008 kama mwakilishi wa Coastal Union, alisema wao Coastal Union wanaumia sana wakisikia Azam FC inatajwa kama moja ya klabu kubwa Tanzania, halafu Coastal Union haitajwi.

Kwa mujibu wake, klabu kubwa nchini ni Yanga, Simba, Coastal Union na African Sports. Sababu yake ni kwamba zilianzishwa muda mrefu, basi. Yaani Rais wa mpira Tanzania na Afrika Mashariki na Kati, anaamini kwamba ukubwa wa klabu ya mpira ni umri, basi.

Kwa kuwa Coastal na African Sports ni kongwe kuliko Azam FC, basi ni kubwa.

Hii ni aibu kubwa sana kwa mpira…kubwa sana!

Sheffield United ya England ndio klabu kongwe zaidi duniani. Ilianzishwa Oktoba 24, 1857 na ikifika tarehe kama hiyo mwaka huu itafikisha miaka 167.

Real Madrid ya Hispania ni moja kati ya klabu ‘changa’ baranı Ulaya ikiwa imeanzishwa Machi 6, 1902, miaka 122 iliyopita.

Kwa Ulaya, klabu zilizoanzishwa miaka ya 1900 ni changa, klabu kongwe ni vile zilizoanzishwa miaka ya 1800. Chelsea (1905) na PSG (1970) ni klabu changa sana.

Lakini licha ya ukongwe wao, Sheffield United hawana chochote cha kutamba mbele ya ‘wachanga’ hawa. Ukiambiwa taja klabu kubwa duniani, huwezi kuitaja Sheffield United, na yawezekana wengi hapa ndiyo wanaijua kwa mara ya kwanza klabu hii.

Karia anasema kama ni ubingwa Azam imechukua mara moja na Coastal Union mara moja.

Anachokosea ni kwamba ukiacha umri, ukubwa wa katika mpira pia sio historia bali ni namna gani unatoa athari chanya msimu baada ya msimu.

PSG hawajawahi kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini wanahesabika kama majayanti wa Ulaya. Aston Villa na Nottingham Forest wamewahi kushinda ubingwa wa Ulaya, lakini hawahesabiki kama ni majayanti wa Ulaya.

Hii ni kwa sababu PSG wana athari chanya katika mpira wa Ulaya kila msimu, lakini Aston Villa na Nottingham Forest hawana athari bali ‘walikuwaga’ nayo zamani…historia!

Blackburn Rovers wamewahi kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England (1995) lakini Tottenham Hotspur hawajawahi.

Huwezi kusema Blackburn Rovers ni klabu kubwa kuliko Tottenham Hotspur pale England.

Ukubwa wa kwenye mpira sio makombe ya zamani, ni athari chanya za wakati husika.

Na hii ndio sababu CAF na hata FIFA hutumia kanuni ya ‘5 year ranking’ kupima ubora wa klabu. Mafanikio yako kwa kipindi cha miaka mitano ndiyo yatakufanya ukae unapostahili…kama ni kwenye ukubwa au udogo. Sio ukongwe wala makombe yako ya zamani.

Barani Afrika, CS Constantine ya Algeria ndio klabu kongwe zaidi. Ilianzishwa mwaka 1898; na ina miaka 126 sasa.

Lakini klabu hii hata nchini kwao sio kubwa. Imechukua ubingwa mara mbili tu, ikizidiwa na CR Belouizdad (10) iliyoanzishwa Julai 15, 1962; miaka 61 tu iliyopita.

Klabu inaweza kuwa kongwe, lakini sio kubwa. Ukubwa hautokani na umri bali uwezo. Ukiona timu imepanda na kushuka daraja mara nyingi kuliko mataji iliyonayo, kama Coastal au African Sports, hiyo ni timu ndogo. Halafu kuhusu Coastal Union kuchukua ubingwa mara moja. Hapa napo kuna shida.

Coastal hawajawahi kuwa mabingwa wa Tanzania kama walivyokuwa Azam.

Ubingwa wanaotaja wa 1988, haukuwa rasmi. Bingwa wa Tanzania mwaka huo alikuwa African Sports na wala sio Coastal Union.

Na ndio maana Sports wakapata nafasi ya kushiriki KLABU BINGWA AFRIKA na Union wakaenda kushiriki Kagame Cup.

Wakati ule Ligi Kuu ya Tanzania ilikuwa ile ya Muungano ambayo ndio ilitoa wawakilishi wa Tanzania kimataifa. Ligi ya Bara haikuwa ligi rasmi bali sehemu ya Ligi ya Muungano.

Katika Ligi ya Muungano, Coastal ilikuwa ya pili na wakapata tiketi ya kushiriki Kombe la Washindi Afrika.

Kwa hiyo ule ubingwa wa Coastal Union wa 1988 ni sawa na mwanariadha aliyeshinda HEAT, yaani mbio za mchujo kuelekea mashindano rasmi.

Na kosa hili ndilo linalowafanya Yanga wahesabie kuwa wana ubingwa mara 30 wa Tanzania…wanachanganya na nyakati kama hizo.

Tukirudi kwenye hafla ya uzinduzi wa kitabu cha Yanga, sio Karia pekee aliyepuyanga.

Waziri wa zamani wa michezo, Mudhihir Mudhihir, pia aliongea ‘maneno mbofu mbofu’.

Alisema mwaka 1936 mkoloni alimwambia Liwali Mukhsini kwamba Yanga sio klabu ya mpira kwa sababu usiku wanafanya vikao kina Nyerere na Karume.

Kwa wasiyojua, Liwali ni kama Meya kwa sasa. Kwa hiyo Mukhsini alikuwa Liwali wa Dar es Salaam, kwa hiyo ni sawa na kusema alikuwa Meya wa Dar es Salaam.

Lakini sio kweli kwamba MWAKA 1936 mkoloni alimwambia Liwali Mukhsini kuwa kina Nyerere na Karume wanafanya mikutano.

Nyerere alizaliwa 1922 na kuanza kusoma Shule ya Msingi Mwisenge mwaka 1934.

Kutokana na kuwa na akili za ajabu, akarushwa darasa moja baada ya miezi sita tu, akaingia la pili.

Kwa hiyo mwaka 1936 Nyerere alikuwa darasa la nne, hata Musoma mjini hakujui…aliwezaje kuwa Dar es Salaam akiendesha vikao vya usiku klabuni Yanga?

Jambo ambalo halikuwa kweli kwenye simulizi ya Mudhihir ni kwamba Liwali Mukhsini kuanzisha timu ya Queens.

Ukweli ni kwamba wakati huo kulikuwa na Ligi ya Dar es Salaam ambayo ilitawaliwa na timu za wageni na taasisi za serikali ya kikoloni.

Timu za wazawa zilikuwa tatu tu, New Strong, Young Africans na Sunderland.

Timu hizi zilipata wakati mgumu kushindana na zile timu nyingine kama Arab Sports Club ambayo ilikuwa ya Waarabu, Sudanese Community Sports Club ambayo ilikuwa ya Wasudan walioishi nchini, Kharsa Sports Club ambayo ilikuwa ya Wahindi wa Kharsas pamoja na timu za taasisi za serikali kama KAR (Kings African Rifles) ambayo ilikuwa timu ya jeshi la mkoloni na kadhalika.

Hivyo ili kujiweka sawa, timu za wazawa zikataka kuanzisha ligi yao itakayoanza mapema kabla ya ile ya Dar es Salaam.

Na lengo lao halikuwa kujitenga bali kujiandaa kwani walitaka kuitumia Ligi yao kama Pre Season.

Mkoloni alihofia ligi hii kwamba ingevuruga utengamano wa kitaifa. Kwamba wazawa wangecheza peke yao ligi yao ingepeta msisimko sana kwa sababu wako wengi, hivyo kuidhoofisha ligi rasmi.

Ndipo mkoloni akaipiga marufuku Ligi hii ya wazawa. Lakini wazo la wazawa kuwa na Ligi yao liliendelea kukua na kutengeneza presha kwa mkoloni. Ndipo Liwali Mukhsini ambaye alikuwa Mwarabu, akapewa jukumu la kubakikisha Ligi hiyo haifanikiwi.

Alichofanya ni kukaa na viongozi wa Sunderland na kuwashawishi kuunganisha klabu yao na klabu ya Arab Sports. Sunderland wakakubali na kuungana…Waarabu wakaingia kwenye timu ya wazawa.

Waarabu hawa wakawa na nguvu ya ushawishi kupinga ile Ligi kupitia timu ya wazawa, Sunderland.

Wakafanikiwa na Ligi haikufanyika tena. Na hiyo ndio sababu ya Simba kuwa na historia kubwa na jamii ya Kiarabu. Lakini haya yalifanyika miaka mingi baada ya Sunderland kuanzishwa. Na ilianza kama Stanley Sports Club kwa sababu ilianzia mtaa wa Stanley ambao sasa ni mtaa wa Aggrey.

Ikabadili jina na kujiita Queens na baadaye Sunderland kama athari ya klabu ya Sunderland ya England kushinda ubingwa wa ligi 1935/36 badaye ndio wakabadili jina na kuwa Simba SC kwa ushauri wa Rais wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume. Historia imeandikwa na itabaki hivyo hadi itakaporekebishwaa, lakini hata hivyo, ya Yanga waachiwe Yanga wenyewe ila haya ya Wallace Karia hapana…haya ni ya wote. Coastal Union ni klabu kongwe, lakini sio klabu kubwa kama anavyotaka kutuaminisha.

Chanzo: Mwanaspoti