Maisha yanaenda kasi sana. Maisha ya Antonio Conte kwenye kikosi cha Spurs yanaonekana kuwa ni mafupi sana huku baadhi ya taarifa zikidai huenda asifike hata wiki ijayo akawa ameshafukuzwa.
Mbali ya uchungu ambao ataupata wa kufukuzwa kazi, kocha huyo kutoka Italia atakuwa na chakujiliwaza kutokana na kiasi cha pesa ambacho atakipata kinachodaiwa kuwa ni Pauni 4 milioni ambacho kinafikia 9 bilioni kwa pesa za Kitanzania.
Makocha wengi wamekuwa wakipata kiasi kikubwa cha pesa kutokana na kufukuzwa kwao, hapa tunakuletea makocha watano ambao walivunja rekodi ya kulipwa pesa nyingi baada ya kufungashiwa virago katika klabu walizokuwa wakizifundisha
5. Fabio Capello, urusi (Pauni 13.4m)
Wakati anaachana na Timu ya Taifa ya England aliripotiwa kupata Pauni 1.5 milioni lakini hiyo ilikuwa ni utangulizi tu kwani alipata mpunga wa kutosha alipoajiriwa na kuinoa timu ya Taifa ya Urusi.
Mpango ulikuwa ni kuiwezesha Urusi kuchukua Kombe la Dunia mwaka 2018 ambapo ilikuwa ni wenyeji lakini kiwango cha timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 iliyofanyika Brazil ndio kilisababisha mawazo ya mabosi wa Urusi yabadilike na kuamua kumfungashia virago. Lakini alilipwa kiasi kisichopungua Pauni 13.4 milioni kama fidia.
4. Luiz Felipe Scolari, Chelsea (Pauni 13.6m)
Hakumaliza hata msimu mmoja kwenye kikosi cha Chelsea akafukuzwa kwenye kile ambacho watu wengi walitafsiri kwamba haikuwa sawasawa.
Scolari alikuwa ameiongoza timu hiyo kwenye mechi 25 za Ligi Kuu England na alikuwa ameifikisha timu hiyo kwenye hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa.
3. Laurent Blanc, PSG (Pauni 17m)
Paris Saint-Germain ni moja ya timu zilizolipa pesa nyingi kwa makocha mbali mbali waliowaajiri tangu uwezekaji uingie rasmi mwaka 2011.
Kocha wa zamani wa Ufaransa alikuwa ni miongoni mwa makocha wa mwanzoni kuajiriwa ili kuifanya timu hiyo kufika nchi ya ahadi. Alifanikiwa kushinda mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu lakini alifungwa mwisho wa msimu wa 2015-16 baada ya kushindwa kuipa timu hiyo mafanikio kwenye michuano ya Ulaya.
Msimu wake wa mwisho Blanc aliiwezesha PSG kufikisha alama 96 kwenye Ligi Kuu ya Ufaransa na alama hizohadi leo hazijafikiwa na timu yoyote ile.
2. Jose Mourinho, Man Utd (Pauni 19.6m)
Takwimu zinaonyesha huyu ndio kocha aliyepata pesa nyingi kutoka kwenye timu alizofukuzwa kuanzia Chelsea hadi Tottenham.
Lakini kiasi kikubwa zaidi cha pesa alikipata baada ya kufungashiwa virago na Manchester United ambapo iliripotiwa kuwa amepokea Pauni 19.6 milioni kama fidia baada ya kuondoshwa na mashetani hao wekundu mwaka 2018 ikiwa ni miaka miwili tangu alipojiunga nao mwaka 2016.
Baada ya kumaliza nafasi ya pili msimu wa 2017-18, msimu uliofuatia, Man United ilionyesha kiwango kibovu na ilishindwa hata kuingia kwenye nafasi nne za juu baada ya kucheza mechi 17.
1. Antonio Conte, Chelsea (Pauni 26.6m)
HADI sasa huyu ndiye kocha anayetajwa kupata pesa nyingi sana baada ya kufukuzwa. Hii ilikuwa wakati amepoteza kibarua chake pale Chelsea, mjumuisho wa pesa aliyoipata unakadiriwa kufikia Pauni 26.6 milioni. Baada ya kuchukua ubingwa, alisaini mkataba mpya mwaka 2017, lakini aliondoshwa mwishoni mwa msimu wa 2017-18, akiwa ameiwezesha timu hiyo kushinda taji moja Ligi Kuu na FA Cup.
Moja kati ya rekodi alizoziweka ilikuwa ni kushinda mechi 13 mfululizo kwenye kwenye msimu ambao aliwaongoza matajiri hao wa Jiji la London kuchukua ubingwa.