Kila binadamu ana mipango mizuri na hujiwekea malengo na muda anaotaka kuyatimiza.
Hata hivyo, wakati wengi wakijiwekea malengo wakati mwingine mambo huenda tofauti na baadhi ya vitu hutokea na kuharibu mipango yao, hivyo kushindwa kufikia malengo waliyojiwekea.
Baadhi ya watu wanaojiwekea malengo ni makocha wa soka, lakini wengi wao hujikuta wakiishia njiani kutokana na kufukuzwa au kuachia ngazi mapema kutokana na sababu mbalimbali zinazotokea katika majukumu.
Hawa ni baadhi ya makocha ambao hawakumaliza hata nusu mwaka ndani ya timu zao na kujikuta wakifungashiwa virago ilhali wengine wakiamua kujitoa ndani ya klabu hizo katika miaka mitatu ya karibuni Ligi Kuu Bara.
Etienne Ndayiragije - Geita Gold
Kocha huyu wa zamani wa Mbao, Azam, KMC na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ameingia katika rekodi ya makocha waliodumu muda fupi zaidi katika timu walizofundisha ndani ya miaka mitatu ya karibuni. Etienne aliajiriwa
Geita Gold mwishoni mwa Agosti, mwaka huu, lakini kadumu kwa miezi miwili, huku akiiongoza katika mechi nne, akipoteza mbili na kutoka sare mbili. Kocha huyo pia ameweka rekodi ya kuwa wa kwanza kufungashiwa virago mapema kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.
Mohammed Badru -
Kocha huyu alifundisha timu mbili ndani ya msimu mmoja, lakini zote alikaa chini ya miezi sita na kutimka.
Alianza kuinoa Gwambina, Februari, mwaka huu, lakini akadumu miezi mitatu kabla ya kutimkia Mtibwa Sugar aliyojiunga nayo Mei.
Badru alidumu ndani ya kikosi cha wakata miwa kwa miezi miwili na nusu na kufanikiwa kuinusuru kushuka daraja. Hata hivyo, licha ya kuwa na lengo la kuendelea kukinoa kikosi hicho, lakini ukimya wa viongozi wa timu hiyo kuhusu kumpa mkataba mpya ulimfanya aachane nayo. Kwa sasa Badru ni kocha wa timu ya vijana chini ya miaka 17 ya Azam FC.
Athuman Bilal ‘Billo’- Alliance
Julai 20, 2019 alitangazwa kuwa kocha mpya wa Alliance FC iliyokuwa ikishiriki Ligi Kuu Bara akichukua mikoba ya Malale Hamsini. Hata hivyo, alidumu ndani ya kikosi hicho kwa siku 36 tu kwani Agosti 27 alitimuliwa huku akiiongoza timu hiyo kucheza mchezo mmoja tu wa ligi.
Usishangae! Ni mchezo wa kwanza tu wa ligi msimu wa 2019/2010 dhidi ya Mbao FC uliomalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1 ulitosha kumpa Billo mkono wa kwaher. Baada ya kutimuliwa alimrushia lawama mmiliki wa
Alliance FC kuwa ndiye chanzo kwani alikuwa akimuingilia majukumu yake.
Zlatko Krmpotic - Yanga
Kocha huyu raia wa Yugoslavia ndiye aliyeweka rekodi ya kudumu muda mfupi zaidi katika timu za Ligi Kuu Bara katika kipindi cha miaka mitatu ya karibuni. Zlatko alidumu kwa siku 35 tu ndani ya kikosi cha Yanga kabla ya kutimuliwa kutokana na mabosi kutoridhishwa na kiwango cha timu yao. Kutimuliwa kwake kuliibua maswali mengi kutoka kwa wadau wa soka, kwani waliona Yanga haikuwa imepoteza mchezo.
Zlatko alikuwa na mkataba wa miaka miwili aliousaini Agosti 29, mwaka jana lakini Oktoba 3, baada ya Yanga kuichapa Coastal Union mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa akafutwa kazi. Zlatko aliingoza Yanga katika michezo mitano tu na ilishinda minne na kutoka sare mchezo mmoja, lakini aliweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kutimuliwa mapema msimu huo.
Amir Said - Mbeya City
Kocha huyu anaingia katika rekodi ya kudumu katika timu kwa muda mfupi, kwani baada ya Oktoba, mwaka jana kutimuliwa Mbeya City, Januari mwaka huu alipata kazi kuinoa Mwadui FC. Hata hivyo, alidumu kwa miezi miwili tu kabla ya kuamua mwenyewe kubwaga manyanga kwa madai kuwa uongozi wa klabu hiyo ulishindwa kumlipa stahiki zake kwa wakati.
Hitimana Thierry - Namungo FC
Huyu alitua nchini mwaka 2019 na kupata kibarua cha kuinoa Namungo FC. Desemba mwaka jana alipewa jukumu la kuinoa Mtibwa Sugar, lakini akadumu kwa miezi minne tu na kuamua kutimka kwa madai ya kutokuwa na maelewano mazuri na mmoja wa watu waliokuwa wasaidizi wake katika benchi la ufundi.
Cedrick Kaze - Yanga
Ni mmoja wa makocha ambao ujio wao ulivutia Yanga na mashabiki walikuwa na imani kubwa kwake, lakini matokeo yake alidumu kwa miezi mitano. Alijiunga na Yanga Oktoba 16, mwaka jana, akichukua mikoba ya Zlatko Krmpotic na kuiongoza katika michezo 18, akishinda 10, sare saba na kupoteza mmoja.
Sare ya bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania katika mchezo uliofanyika Machi 7, mwaka huu ndio ilisababisha uongozi kufanya uamuzi mgumu wa kuachana naye. Hata hivyo, Kaze amerejea tena Yanga msimu huu akiwa kama kocha msaidizi chini ya kocha mkuu, Nasreddine Nabi.
WASIKIE MASHABIKI
Twalib Bilal, shabiki wa soka anasema kuna makocha wanaotimuliwa lakini wakiwa na ubora wao katika timu wanazofundisha, suala ambalo viongozi wanapaswa kuwa wanaliangalia kabla ya kuchukua uamuzi.
“Kuna jambo fulani la kujifunza katika suala hili. Nadhani viongozi wawe na utaratibu wa kuwaangalia makocha wao kwa umakini sio kukimbilia kuwafukuza tu,” anasema.
Doreen Mwambuke anasema makocha huwa wanakuwa na programu nyingi ambazo wanazipanga kuzitekeleza katika timu zao, lakini huishia kufukuzwa kabla ya wakati na wakati mwingine timu zikiwa katika ubora wa juu zaidi.
“Mfano, nitashaangaa sana kusikia kwamba kocha kama yule wa Yanga kwa sasa anafukuzwa eti tu kwa kuwa timu labda itateleza mchezo fulani. Jamani hawa watu wana mipango mingi na huwa wanacheza na akili za wachezaji wengi kuwaingizia ubora, wasikimbilie kufukuzwa tu,” anasema.