Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walitesa Yanga SC, lakini...

Mayele: Nabi Na Kaze Waliondoka Na Mabegi Yao Yote Mechi Ya Africain Walitesa Yanga SC, lakini...

Fri, 10 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Miaka mitatu ya hivi karibuni Yanga imekuwa imara zaidi kwenye eneo la benchi la ufundi na timu kwa ujumla kutokana na mafanikio iliyoyapata hivi karibuni.

Ndani ya misimu mitatu Yanga imeandika rekodi chini ya makocha wawili tofauti ambao wote wametua kikosini hapo kwa nyakati tofauti.

Alianza Nasreddine Nabi ambaye alitambulishwa ndani ya kikosi hicho Aprili 20 na alianza kazi yake ya kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kukubali kichapo cha bao 1-0.

Chini ya kocha huyo ambaye aliomba kuondoka ndani ya timu hiyo ili kwenda kujaribu maisha sehemu nyingine mwishoni mwa msimu uliopita, ametwaa mataji sita - mawili mawili ya Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ngao ya Jamii.

Licha ya rekodi ya kurudisha mataji, pia aliandika rekodi ya kumfunga mtani wao, Simba mara nne kwenye mechi saba wakitoka sare moja na kukubali kichapo kimoja.

Pia aliandika rekodi ya kuifikisha Yanga katika fainali Kombe la Shirikisho Afrika na kucheza mechi 38 bila kufungwa akishinda 28 na kutoka sare 10.

Uongozi wa Yanga licha ya kukubali kuondoka kwa Nabi ulituliza kichwa na kumshusha kocha mwingine ambaye ni Miguel Gamondi ambaye tayari ameandika rekodi ndani ya timu hiyo akiifikisha Yanga katika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka 25.

Mbali na hilo pia amelipa kisasi cha miaka 11 kwa kumfunga Mnyama mabao 5-1 tukio ambalo walilifanya Simba 2012 wakiwafunga Yanga mabao 5-0. Hadi sasa ameiongoza timu hiyo kwenye mechi nane ikifungwa mchezo mmoja na kukusanya pointi 21.

Mwanaspoti licha ya kubaini ubora katika eneo hilo linakuletea makocha watano ambao wamepita kwenye timu hiyo sasa wanapambana kufanya vizuri kwenye timu walizopo.

CEDRICK KAZE

Ni kocha ambaye alikuwa kwenye mafanikio ya Yanga misimu miwili iliyopita akiwa msaidizi chini ya Nabi aliyeshindwa kuongezewa mkataba mara baada ya mkataba wake kumalizika msimu uliopita. Baada ya kutoongezewa mkataba Kaze aliibukia Namungo kwa mkataba wa miaka miwili na alidumu timu hiyo kwa muda mfupi akiiongoza katika mechi sita, sare tatu na kufungwa tatu.

MWINYI ZAHERA

Zahera licha ya kupambana kumaliza nafasi ya pili Yanga na baadaye kutimuliwa nafasi yake ikachukuliwa na Boniface Mkwasa. Baada ya muda alirudi Yanga akakabidhiwa timu za vijana, lakini baada ya mkata wake kumalizika alitimkia Polisi Tanzania ambako aliishusha daraja.

Baada ya hapo aliibukia Coastal Union ambako aliiongoza katika mechi tano akifungwa tatu na sare mbili. Baada ya matokeo hayo aliondolewa benchi la ufundi na kupelekwa timu ya vijana kuwa mkurugenzi wa benchi la ufundi. Miongoni mwa timu ambazo Zahera amewahi kuzifundisha ni DC Motema Pembe ya DR Congo tangu Machi 1, 2015 hadi Machi 10, 2016 akitoka kuwa kaimu kocha wa AFC Tubize ya Ubelgiji kati ya Oktoba 7 na Oktoba 23, 2014 ambayo alijiunga nayo akitoka kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya DRC kati ya Agosti 14 na 28, 2017 chini ya Florent Ibengé.

HANS VAN PLUIJM

Aliachiwa timu baada ya kupandishwa kutoka Daraja la Kwanza msimu wake wa kwanza Singida Big Stars akiiongoza kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo msimu uliopita na kuipa nafasi timu hiyo kushiriki mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Msimu huu ameiongoza SBS kwenye mechi moja tu iliyochezwa Agosti 22 dhidi ya Tanzania Prisons na kuambulia pointi moja baada ya sare 1-1. Alijiuzulu Agosti 29 baada ya kuiongoza SBS kufuzu hatua ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuifunga JKU mabao 4-3.

NASREDDINE NABI

Kaondoka Yanga akiwa na rekodi nzuri baada ya kuipa mataji sita timu hiyo ambayo sasa ipo chini ya Gamondi ametua FAR Rabat ambayo inaongoza msimamo baada ya kukusanya pointi 17 kwenye mechi nane alizocheza ameshinda tano, sare mbili na kufungwa mchezo mmoja.

Licha ya kufanikiwa kuiongoza timu hiyo kwenye ligi ameshindwa kuipeleka timu hiyo nafasi inayofuata Ligi ya Mabingwa na kuiondoa ikiishia hatua ya awali huku timu yake ya zamani Yanga akiifikisha hatua ya fainali Kombe la Shirikisho.

FRED FELIX ‘MINZIRO’

Licha ya kusifika kwa kupandisha timu Ligi Kuu, lakini kwa sasa Minziro anapitia nyakati ngumu kwenye kikosi cha Tanzania Prisons alikotua akitokea Geita Gold. Timu hiyo ameiongoza kwenye mechi tisa, imeshinda moja, sare nne pamoja vichapo vinne.

Minziro ambaye alipita Yanga akiwa kocha msaidizi msimu wa 2012 amekalia kuti kavu ndani ya timu hiyo ambayo inapambana kujiimarisha kuhakikisha inafanya vizuri katika michezo iliyobaki.

Chanzo: Mwanaspoti