Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walipo mastaa wa Ufaransa wa mechi ya fainali Russia 2018

Ufaransa Pic Walipo mastaa wa Ufaransa wa mechi ya fainali Russia 2018

Thu, 15 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Ufaransa ilifuta machungu ya kuchapwa fainali ya Euro 2016 kwa kwenda kubeba ubingwa wa Kombe la Dunia 2018 huko Russia.

Ufaransa ilibeba ubingwa wao wa pili wa Kombe la Dunia hiyo 2018 kwa kuwachapa Croatia 4-2 katika mchezo wa fainali uliofanyika uwanjani Luzhniki jijini Moscow.

Katika fainali hizo za Russia 2018, Les Bleus ilishinda mechi sita kati ya saba, ikiwapiga Argentina (4-3), Uruguay (2-0) na Ubelgiji (1-0) kwenye raundi ya 16, robo fainali na nusu fainali mtawalia.

Katika mchezo wa fainali, Ufaransa ilitangulia kutikisa nyavu za Croatia kwenye dakika ya 18 tu kwa bao la kujifunga la Mario Mandzukic.

Croatia ilisawazisha kupitia kwa Ivan Perisic kwenye dakika 28, lakini Les Bleus ilifunga tena kupitia kwa Antoine Griezmann kwa penalti dakika 38 kisha Paul Pogba na Kylian Mbappe nao wakitupia nyavuni dakika 59 na 65 mtawalia.

Mandzukic, aliyefunga naye alifunga na kufanya mechi hiyo ya fainali kumalizika kwa matokeo ya 4-2, Ufaransa wakiwa mabingwa.

Wakat usiku wa jana Jumatano, Ufaransa ilikuwa uwanjani kukipiga na Morocco kwenye mchezo wa nusu fainali wa Kombe la Dunia 2022 huko Qatar – na kilichotokea kimetokea, ni mastaa hao wa Les Bleus walioipa ubingwa wa dunia timu hiyo minne iliyopita na wapo wapi kwa sasa wachezaji hao?

Hugo Lloris – kipa

Kipa namba moja wa Ufaransa, Hugo Lloris amekuwa kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur tangu 2012, huku kabla ya hapo alizichezea Nice na Lyon kwenye Ligue 1.

Alipita kwenye kipindi kigumu ndani ya muda huo wa miaka minne, lakini bado ameendelea kuwa chaguo la kwanza kwenye goli la Spurs na Ufaransa.

Benjamin Pavard – beki wa kulia

Unapotaja jina la Pavard, utakumbuka lile bao lake matata kabisa dhidi ya Argentina. Beki huyo wa kiraka, alikuwa akizichezea klabu za Lille na Stuttgart kabla ya kujiunga na Bayern Munich mwaka 2019, ambako anacheza hadi sasa. Pavard bado yupo kwneye kikosi cha Ufaransa cha Kombe la Dunia 2022 huko Qatar.

Raphael Varane – beki wa kati

Beki huyo alijiunga na Real Madrid kutoka Lens mwaka 2011 na alitumikia misimu 10 kabla ya kutimkia zake Manchester United mwaka 2021. Kwenye msimu wake wa kwanza huko Old Trafford, Varane ameunda pacha imara na Lisandro Martinez chini ya Kocha Erik ten Hag. Bado yupo kikosini Les Bleus kilichoenda Qatar.

Samuel Umtiti – beki wa kati

Maisha ya soka la beki huyo wa kati, Umtiti yameporomoka tangu alipobeba ubingwa wa Kombe la Dunia 2018 huko Russia. Staa huyo alichelewesha upasuaji wa goti ili acheza Kombe la Dunia na tangu wakati huo ameshindwa kabisa kupona sawasawa. Barcelona ilimpeleka Lecce kwa mkopo mwaka huu kukwepa kumlipa mshahara.

Lucas Hernandez – beki wa kushoto

Beki huyo wa penalti alicheza mechi yake ya kwanza Atletico Madrid mwaka 2014 na kudumu hapo kwa misimu mitano kabla ya kwenda kujiunga na Bayern Munich mwaka 2019.

Majeruhi yamemtibulia mpango wa kucheza soka la kiwango cha juu. Yupo kwenye kikosi cha Ufaransa, lakini ameumia akiwa Qatar 2022.

Paul Pogba – kiungo wa kati

Kiungo huyo wa zamani wa Manchester United alikuwa mchezaji muhimu wa Ufaransa wakati inabeba ubingwa 2018, akitawala mchezo na alifunga bao kwenye fainali yenyewe.

Amerudi Juventus mwaka huu, lakini majeruhi yamekuwa yakitibua maisha yake na kumfanya akose fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar.

N’Golo Kante – kiungo wa kati

Kiungo huyo anayekaba kupita maelezo alicheza Boulogne, Caen, Leicester City na sasa yupo Chelsea, alikojiunga tangu 2016. Majeruhi yamekuwa yakimwandama na kuvuruga mipango yake na hivyo kukosekana uwanjani huko Chelsea na sasa Ufaransa, ambayo ilikwenda Qatar 2022 kwa lengo la kutetea ubingwa wao wa dunia.

Kylian Mbappe – winga wa kulia

Alinyakua tuzo ya Kinda Bora kwenye Kombe la Dunia 2018 na alifunga mabao manne kuipa Ufaransa ubingwa. Baada ya miezi kadhaa ya minong’ono ya kwenda Real Madrid, Mbappe aliamua kubaki zake Paris Saint-Germain. Amekuwa mtu muhimu kwenye kikosi cha Ufaransa kwenye fainali za Qatar 2022.

Antoine Griezmann – mshambuliaji

Fowadi huyo naye alifunga mabao manne kwenye fainali hizo za Russia 2018 kama ambavyo alifanya Mbappe.

Griezmann ameendelea kubaki kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Les Bleus, licha ya kwamba mchezaji huyo wa Atletico Madrid haonekani kuwa kwenye kiwango kile cha kutosha kama 2018.

Blaise Matuidi – winga wa kushoto

Matuidi alizichezea Juventus, Paris Saint-Germain na Saint-Etienne katika kipindi chake cha soka la kulipwa kabla ya mara ya mwisho kwenda Ligi Kuu Marekani kuichezea Inter Miami.

Alikuwa muhimu sana wakati Ufaransa inabeba ubingwa 2018 huko Russia, akiwa wingi wa kushoto na pia Pogba na Kante kwenye kiungo.

Olivier Giroud - mshambuliaji

Kinara wa mabao wa muda wote wa Ufaransa, Giroud amefanya kweli kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar kama ambavyo alitoa mchango muhimu wakati Les Bleus inabeba ubingwa huo wa dunia miaka minne iliyopita huko Russia. Giroud kwa sasa aaichezea AC Milan, lakini alipita pia Montpellier, Arsenal na Chelsea.

Steven Nzonzi – sub

Kiungo wa kati, Nzonzi kwa sasa anacheza soka lake huko Qatar kwenye klabu ya Al-Rayyan, aliyojiunga nayo mwaka 2021 kwa dili la miaka miwili.

Mechi yake ya kwanza Ufaransa ilikuwa 2017 na mara ya mwisho kuichezea Les Bleus ilikuwa 2019.

Nabil Fekir – sub

Zao la akademia ya Lyon na alichezea miamba hiyo kwenye Ligue 1 kwa misimu sita kabla ya kwenda kujiunga na Real Betis mwaka 2019.

Mechi yake ya kwanza kuichezea Ufaransa ilikuwa mwaka 2015 na bado yupo hajatundika daruga kuichezea Les Bleus.

Corentin Tolisso – sub

Kiungo huyo aliibukia kwenye kikosi cha Lyon kabla ya kwenda Bayern Munich mwaka 2017, alipokwenda kutengeneza jina ng’ambo. Baada ya misimu mitano Bayern, Tolisso alirudi nyumbani.

Mechi yake ya kwanza Ufaransa ilikuwa 2017 na bado Les Bleus inaweza kumteua kwenye kikosi itakapohitajika.

Chanzo: Mwanaspoti