Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliotoka Mapinduzi wakaula Bara

Fei Toto Asd.jpeg Fei Toto

Fri, 29 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Michuano ya Mapinduzi Cup tayari yashaanza huku Tanzania Bara ikiwakilishwa na timu nne za Simba, Yanga, Azam FC na Singida Big Stars kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Mashindano hayo ambayo yamekuwa yakiwanufaisha mastaa wa visiwani Zanzibar kwa kupata nafasi ya kusajiliwa kwenye timu za Bara. Dirisha dogo la usajili limefunguliwa Desemba 16 na linatarajiwa kufungwa Januari 15 hivyo ni muda sahihi kwa mastaa wa timu za Zanzibar kufanya vizuri ili kujihakikishia ulaji Bara.

Hadi sasa tayari kiungo mmoja mshambuliaji kutoka JKU, Shekhan Ibrahim Khamis amefungua njia baada ya kumwaga wino kwenye kikosi cha Yanga kwa mkataba wa miaka mitatu.

Kupitia Kombe la Mapinduzi lililoanzishwa mwaka 1998 mpaka sasa ni miaka 22, limewatoa wanasoka wengi wa Zanzibar ambao wamebahatika kuonja pesa ndefu za Simba, Yanga na Azam FC, Geita Gold, Coastal Union ingawa wapo waliojiunga na timu nje ya hizo.

Msimu uliopita, Mlandege ilitwaa ubingwa wa Mapinduzi ikiwa mara ni  ya  kwanza tangu mashindano hayo kuanzishwa na pia ni wa kwanza kwa timu za Zanzibar ambao ndio wenyeji wa mashindano.

Mwanaspoti linakuletea baadhi ya wachezaji ambao wameonekana katika michuano ya Kombe la Mapinduzi kisha wakasajiliwa kwenye klabu hizo kuelekea usajili huu unaoendelea je? Nani Ataibukia bara dirisha hili.

YASSIN MGAZA (DODOMA JIJI)

Alikuwa kinara wa upachikaji mabao msimu uliopita, kutokana na umahiri wake wa kutupia Dodoma Jiji ilivutiwa na huduma yake na kumpa mkataba wa kuitumikia katika dirisha dogo la usajili la msimu uliopita. Mshambuliaji huyo licha ya kuonesha makali kwenye klabu yake ya zamani KMKM ameshindwa kuendeleza makali yake ndani Dodoma Jiji kwani hadi sasa ligi ikiwa imesimama akiwa ametupia mabao mawili tu.

GAMAL ABDUL NASIR (MASHUJAA)

Ni mshambuliaji aliyesajiliwa msimu huu akitokea Mlandege hii ni baada ya kufanya vizuri kwenye Kombe la Mapinduzi lakini hadi sasa akiwa ndani ya timu hiyo hajaonyesha maajabu yake.

Gamal amefanikiwa kuifungia Mashujaa bao moja tu ambalo  Desemba 2 dhidi ya KMC timu yake ikikubali kichapo cha mabao 3-2 ameitwa kikosi cha Zanzibar Herous.

HASSAN HADJI CHEDA (MASHUJAA)

Ni kiraka anatumika katika nafasi za kiungo na winga ni mchezaji ambaye amekuja na bahati Bara kwani amekuwa akipata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza. Cheda alisajiliwa akitokea Zimamoto umahiri wake umemfanya Kocha wa Timu ya Taifa ya Zanzibar, Hemed Morroco kumjumuisha kwenye kikosi cha Zanzibar Heroes.

MOHAMMED MUSSA (SIMBA)

Usajili wake ulizungumzwa sana huku akitajwa na aliyekuwa kocha wa timu Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kuwa ni mchezaji mzuri akipunguza kilo baada ya kuongezeka sana uzito kutokana na kukosa nafasi ya kucheza.

Mussa alisajiliwa na Simba akitokea Malindi ambayo aliifanyia kazi kubwa michuano iliyopita akionyesha uwezo mkubwa uliowashawishi viongozi wa Simba ambao walimsainisha mkataba wa miaka mitatu, tangu ametua Simba amefunga bao moja tu kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) akiifunga African Sports.

ABASS ATHUMAN NZIAJOSE (TABORA UNITED)

Licha ya Tabora United kutoshiriki mashindano ya Mapinduzi Cup lakini walikuwa na jicho la kuona wachezaji ni baada ya kunasa saini ya Nziajose Katoka Jang’ombe. Licha ya kukosa namba ya moja kwa moja kikosi cha kwanza amekuwa akicheza dakika chache tofauti na wachezaji wengine ambao wamesajiliwa ndani ya timu hiyo.

LAURIAN OMAR MAKAME (SINGIDA FOUNTAIN GATE)

Singida Big Stars licha ya kukosa taji katika fainali ya Kombe la Mapinduzi msimu uliopita ilifanikiwa kuinasa saini ya  Laurian Makame ambaye kutoka Black Sailors. Huyu ni beki wa kati lakini hajawahi kuwa katika chaguo la kwanza na amekuwa akipata nafasi dakika chache.

KHALID HABIB IDD (SINGIDA FOUNTAIN GATE)

Mbali na Laurian Omar Makame, Singida Big Stars licha ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 lwenye fainli dhidi ya Mlandege pia ilifanikiwa kunasa saini ya Khalid Habib Idd kutoka KMKM.

Mchezaji huyo licha ya kujinyakulia kitita kutoka kwa walima Alizeti hao hana namba ya kudumu kikosi cha kwanzalicha ya kuonekana kuwa bora Zanzibar kwenye nafasi ya kiungo amekutana na kina Yusuf Kagoma, Moris Chuku na amekuwa akipata nafasi ya kucheza mara  chache .

RAHIM SHOMARY (KMC)

Alisajiliwa na KMC kutoka KVZ ni kipenzi cha Kocha Abdihamid Moallin kwani ameenda kumkalisha benchi Hans Masoud ni beki namba tatu ambaye amefanya mapinduzi makubwa ndani ya timu hiyo. Shomary ni chaguo la kwanza na amekuwa akikiwasha vilivyo chini ya Mollin ambaye ameonekana kumwamini zaidi kwa kumpa nafasi ya kucheza mara kwa mara.

MAABAD MAULID (COASTAL UNION)

Alisajiliwa na Coastal Union baada ya kuibuka mfungaji bora Ligi Kuu Zanzibar ndani ya kikosi cha KVZ akimaliza kwa kupachika mabao 19 ana misimu miwili sasa ndani ya timu hiyo. Msimu wake wa kwanza alitupia mabao manne na msimu huu ambao ni wa pili kwake tayari amekwamisha mabao matatu nyavuni hivyo amebakiza bao moja kuvunja rekodi yake mwenyewe.

AHMED ALLY SULEIMAN SALULA (AZAM FC)

Huu ulikuwa ni usajili wa mwisho wa Azam FC ikimsajili kipa huyo kutoka KMKM msim wa 2021 kwa mkataba wa miaka miwili lakini hakufanya majabu pamoja na kupata nafasi ya kucheza. Msimu uliofuata dirisha dogo la usajili 2022 Azam FC ilitangaza kuachana na kipa huyo kutokana na kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara kutokana na uwezo mdogo  mbele ya makipa wengine ndani ya timu hiyo.

MWADINI ALI - AZAM FC

Uongozi wa Azam FC uliona kipaji cha kipa huyo kupitia Kombe la Mapinduzi akiwa na timu ya Mafunzo, ikamsajili lakini sasa hayupo ndani ya timu hiyo baada ya kutupiwa virago baada ya kudumu kwa muda mrefu.

Kipa huyo alisajiliwa  mwaka 2011 akadumu ndani ya timu hiyo kwa miaka 10 alikumbana na changamoto mbalimbali za majeraha na muda mwingine kukosa namba ndani ya kikosi cha kwanza, hivyo ni kati ya wachezaji wenye historia na michuano hiyo.

HAJI MWINYI

Yanga ilimsajili beki namba mbili Haji Mwinyi mwaka 2015 akitokea KMKM ya Zanzibar, uwezo wake ulionekana kwnye michuano ya Kombe la Mapinduzi. Beki ambaye baada ya soka la Bara kumshinda alirudi tena visiwani Zanzibar sasa anakipiga kwenye timu yake ya KMKM iliyompa maisha Bara.

MASOUD NASSORO ‘CHILLO’

Simba pia mwaka 2007 ilimsajili beki namba mbili, Masoud Nassor ‘Chollo’aliyekuwa nahodha wa kikosi chao, ilimuona kwenye Kombe la Mapinduzi mwaka mmoja nyuma yake. Huyu ni kati ya wachezaji waliofanikiwa sana baada ya kuja Bara.

AGREY MORIS - AZAM FC

Azam FC ilimuona beki namba tatu ambaye ni tegemeo ndani ya kikosi chao na Taifa Stars kupitia Kombe la Mapinduzi akiwa na Mafunzo ya Zanzibar. Moris ambaye hivi karibuni ametoka kumpoteza mke wake,tangu asajiliwe na ndani ya kikosi hicho amekuwa na kiwango cha juu na kucheza kwenye kikosi cha kwanza. Hadi anastaafu kuitumikia Azam FC, Moris alikuwa nahodha aliyecheza kwa mafanikio makubwa.

ABDALLAH SHAIBU ‘NINJA’ - YANGA

Mwaka 2017 Yanga ilimsajili beki namba nne,Ninja baada ya kuonekana kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi akiwa na timu ya Taifa Jang’ombe ambao walimuaga kwa kumfanyia sherehe.

Beki huyo ambaye sasa anakipiga nje ya Tanzania akijaribu bahati huko baada ya kutemwa na Yanga amepata mafanikio makubwa ndani ya timu yake hiyo ya zamani akitwaa mataji.

ABDALLAH SIBO - AZAM FC

Kama si michuano ya Kombe la Mapinduzi,beki namba tano wa Azam FC,Abdallah Sibo huenda asingepata dili la kuichezea Azam FC mpaka sasa. Sibo nimiongoni mwa wachezaji walionekana kupitia michuano hiyo akiwa na timu ya Mafunzo, kiwango chake kikakubalika na mabosi wa Azam FC wakamsajili hadi sasa anaitumikia timu hiyo licha ya sasa kuwa nje ya uwanja kutokana na kuuguza jeraha la goti.

ABDULAZIZ MAKAME -YANGA

Michuano ya Kombe la Mapinduzi ya mwaka 2018 ilimtoa kiungo mkabaji namba sita Abdalaziz Makame kupata bahati ya kuichezea Yanga. Yanga ilimsajili Makame akitokea Mafunzo ingawa si mara ya kwanza kwa mchezaji huyo kuchezea timu za Bara kwa mara ya kwanza alisajiliwa Simba nao walimuona kwenye Kombe la Mapinduzi. Baada ya kuzitumikia timu za Namungo na Kagera Sugar alirudi visiwani.

FEISAL SALUM ‘FEI TOTO’ - AZAM FC

Kiungo namba nane wa zamani wa Yanga, Feisali Salum ‘Fei Toto’ alionekana kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi uwezo wake ukaja kuonekana zaidi akiwa na JKU ya Zanzibar. Kiwango chake kiligeuka dili kwa Simba, Azam FC, Singida United lakini Yanga ikazipiga bao zote na kumsajili. Ameitumikia Yanga kwa mafanikio makubwa kabla ya kuamua kuondoka na sasa anakipiga Azam FC ambayo imemnunua Yanga a akiwa ndani ya timu hiyo amefanikiwa kufunga mabao saba akihusika na pasi nne za mwisho zilizozaa mabao.

KHLEFFIN HAMDOUN - AZAM

Michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa mwaka huu, limemfanya Mshambuliaji Khleffin Hamdou aonekane na Azam FC kwa kandarasi ya miaka minne. Ameonekana  na timu yake ya Mlandege ambayo ilikuwa inashiriki michuano hiyo na kutolea hatua za awali.

KHAMIS MCHA - AZAM FC

Ingawa kwa sasa yupo Tanzania Prisons kwa Mara ya kwanza mchezaji huyo anaweza akasimama namba 10 na 11 alionekana kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi. Azam FC ilimsajili kutoka timu ya Miembeni baada ya kuonyesha kiwango kikubwa Kombe la Mapinduzi.

MATHEO ANTHONY - YANGA

Yanga ilimuona Matheo Anthony kwenye Kombe la Mapinduzi n sasa anakipiga  Mtibwa Sugar. Yanga ilimtoa Kipanga ya Zanzibar hata hivyo hakupata namba kwenye kikosi cha kwanza cha Wanajangwani.

Kati ya wachezaji wa Kizanzibari walioweka alama Yanga ni pamoja na nahodha wa zamani wa timu hiyo Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye alipostaafu alipewa umeneja kisha ikamtoa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live