Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliofungwa mabao 16-1 kushtakiwa TFF

Waliofungwa Mabao Waliofungwa mabao 16-1 kushtakiwa TFF

Mon, 21 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Timu za Nyota na Domingo zimeitupia lawama Olasiti FC na Arusha City FC zikiwatuhumu kupanga matokeo katika mchezo wa mwisho wa kundi B ya Ligi Daraja la tatu mkoa wa Arusha msimu wa 2022/23.

Mchezo huo ulipigwa kwenye uwanja wa shule ya sekondari Ilboru wikiendi iliyopita Olasiti ikikubali kichapo cha mabao 16-1 na kugeuka daraja kwa Arusha City kutinga hatua ya Sita bora, Nyota ikipoteza kwa mabao 4-1 mbele ya Royal SC huku Meserani FC  wakishindwa kutokea katika uwanja wao wa nyumbani ili kumenyana na Domingo FC.

Kabla ya mechi hizo katika msimamo wa kundi B ya ligi ya Mkoa wa Arusha,Vinara walikuwa ni Royal SC kwa alama 20, ambao tayari walishafuzu nafasi ya pili Nyota kwa alama 18, Domingo FC wakishika nafasi ya Tatu kwa alama 15 sawa na Arusha City FC, nafasi ya tano ilikuwa ni Olasiti FC kwa alama nne huku Meserani FC wakiburuza mkia kwa alama mbili baada ya mechi tisa.

Arusha City FC walikuwa wanahitaji ushindi wa mabao kuanzia 11 kupanda juu ili kufikisha alama 18 sawa na Nyota wakati huo ikiziombea Nyota na Domingo kupoteza ili wapate nafasi ya kutinga hatua ya Sita bora kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa.

Katibu wa timu ya Nyota, Ezekiel Kidenye amesema wamepanga kupeleka malalamiko yao kwa kamati ya mashindano ya Ligi hiyo pamoja na shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwani mechi hiyo ilikuwa na viashiria vyote vya upangaji wa matokeo.

"Kwanza tunapeleka malalamiko wakati tukijipanga kukata na rufaa tunataka timu zipite kihalali na siyo kubebana hivyo",amesema Kidenye.

Ameongeza kuwa wanaoushaidi unaonyesha katika mchezo huo wa Arusha  City dhidi ya Olasiti, mabao saba yalifungwa kipindi cha kwanza huku mabao tisa yakifungwa kipindi cha pili lakini pia zilipatikana penati saba pamoja na mchezo wenyewe kuchezwa zaidi ya dakika 90.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Domingo FC, Mwinyi Hamza amesema nao wanapanga kuikatia Arusha City rufaa wakiwatuhumu kuwalaghai wapinzani wao Meserani FC ili wasitokee uwanjani huku wakiweka wazi kuwa kama hawatasikilizwa wataachana na soka la Arusha.

Mwanaspoti imemtafuta Katibu wa kamati ya mashindano ya Ligi daraja la tatu Arusha, Samwel Mpenzu ambaye amesema hawezi kulizungumzia suala ilo kwani hawajapokea barua ya malalamiko kutoka kwa timu yoyote.

Matokeo ya mechi tisa za nyuma kwa Olasiti FC kabla ya kupoteza 16-1 dhidi ya Arusha City FC ni Olasiti 0-3 Arusha City, Nyota 4-1 Olasiti, Meserani 0-0 Olasiti, Domingo 2-1 Olasiti, Olasiti 0-1 Royal, Royal SC  2-0 Olasiti, Olasiti 0-8 Domingo, Olasiti 4-1 Meserani FC, Olasiti 1-3 Nyota, Arusha City 16-1 Olasiti.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live