Walinzi watatu wa Kampuni ya Samike Security Campany iliyopo Wilayani Geita wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumpiga rungu na kumuua Mfanyabiashara na Shabiki maarufu wa Yanga Alex Mayaya (40) baada ya kumhisi ni mwizi usiku wa Novemba 05, 2023.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo huku akisema chanzo ni Walinzi hao kujichukulia sheria mkononi.
"Baada ya ushindi ule wa Yanga, Alex alishangilia kupita kiasi na akanywa pombe za kupita kiasi kisha akaenda kwenye duka lake lililopo eneo la Kilimahewa Katoro Wilaya ya Geita na akafungua hilo duka na akatoa matairi mawili ya pikipiki huyo Mfanyabiashara alikuwa anauza vifaa vya pikipiki, kwa bahati mbaya duka lake lile linaendeshwa na kijana wake kwa hiyo wale walinzi hawamfahamu vizuri wakahisi ni mwizi kwa hiyo baada ya kuhisi ni mwizi walimkamata walimshambulia kwa kumpiga na rungu.
“Baada ya kumpa kipigo Mfanyabiashara huyo walinzi hawakumpeleka Kituo cha Polisi walikaa nae mpaka asubuhi kulipokucha huku hali yake ikiwa mbaya na kupelekea umauti wake baada ya kumfikisha Hospitali kwa matibabu zaidi asubuhi,” alisema Kamanda Jongo.