Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waleteni tuwaonyeshe kazi

Yanga Mapinduzi Fg Waleteni tuwaonyeshe kazi

Sun, 7 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ule utamu wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 ndio umefikia mahala pake wakati mechi za robo fainali za kwanza zikipigwa leo Jumapili kabla ya kumalizwa kesho Jumatatu, huku mashabiki wa klabu kongwe nchini Simba na Yanga visiwani hapa wakitambiana wakitaka timu hizo zikutane fainali.

Mashabiki hao wanajua kabisa kuna uwezekano mdogo kwa timu hizo kukutana hatua ya nusu fainali kutokana na ratiba ilivyo, lakini wanaamini kila moja ikipenya hatua mbili zilizo mbele yao, basi kuna uwezekano mkubwa ile derby ya Novemba 5, mwaka jana ambapo Simba ilichapwa 5-1 ikajirudia hapa.

Ipo hivi. Leo zinapigwa mechi mbili za robo fainali, mapema saa 10:15 jioni watetezi Mlandege watavaana na ndugu zao wa KVZ katika mechi inayokumbushia pambano la Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), lililopigwa Septemba 24 mwaka jana ambalo liliisha bila timu hizo kufungana.

Kisha usiku itakuwa zamu ya Yanga ya Miguel Gamondi itakayocheza na APR ya Rwanda iliyopita kama moja kati ya timu mbili za ‘best looser’ ikiwamo Jamhuri ya Pemba ambayo kesho itakuwa na kibarua usiku dhidi ya Simba, ikitanguliwa na mechi baina ya Azam FC na Singida Fountain Gate.

Washindi wa mechi za leo Jumapili ndio watakaokutana kwenye mchezo wa nusu fainali ya kwanza itakayopigwa mapema Jumatano kisha itafuatiwa na washindi mechi za kesho kukiwa na harufu ya kuwepo kwa Mzizima Derby inayozihusu Simba na Azam kama zitavuka salama hiyo kesho Jumatatu.

Kumbuka michuano hiyo inayochezwa kwa msimu wa 18 tangu ilipoasisiwa kwa mfumo wa sasa mwaka 2007, zimeshuhudia timu nne zikiaga mapema kupitia hatua ya makundi zikiwamo mbili za Zanzibar JKU, Chipukizi na zile za kigeni, Vital’O ya Burundi na Jamus ya Sudan Kusini.

Tuanze mechi ya Wazanzibar. Mchezo huu licha ya upinzani, lakini ni wa kuchujana baina yao, kwani timu itakayoshinda itaiondoa nyingine na kupunguza nafasi ya timu za visiwani hapa kutinga mbili hatua ya nusu fainali.

Kazi kubwa ipo kwa Mlandege inayotetea taji hilo ililolitwaa msimu uliopita kwa kuifunga Singida mabao 2-1, kwani ikizembea mbele ya Maafande wa KVZ, itakuwa imeacha michuano na kulitema rasmi taji hilo na kuziachia timu nyingine kupambana ili kulibeba katika fainali ya Januari 13.

Timu hizo zinakutana zikiwa na kumbukumbu kuwa, kabla ya michuano hiyo kuanza zilicheza mechi ya kutesti mitambo na KVZ iliisasambua Mlandege mabao 5-1, hivyo kuifanya iwe mechi ya kisasi.

KVZ nayo haitataka kutibua rekodi yake, hivyo itashuka uwanjani ikiwa imejipanga kushinda na kwenda nusu fainali itakayokuwa ya kwanza kwenye michuano hiyo kwa kuitumia Mlandege kama daraja.

Kwenye hatua ya makundi KVZ ilishinda mchezo mmoja na kutoka sare moja na kupoteza mmoja na kumaliza ya pili nyuma ya Yanga katika Kundi C, wakati Mlandege  ilimaliza ya pili nyuma ya Azam katika Kundi A ikitoka sare mechi zote tatu na kutinga hatua hiyo na pointi tatu tu.

Kocha wa Mlandege, Hassan Pele alisema mechi hiyo itakuwa ngumu kwa kuwa wanakutana na timu zinazojuana lakini wataingia na akili ya kutaka kufuzu nusu fainali.

“Ni kweli walitufunga kabla ya mashindano haya lakini hii mechi ya kesho (leo) itakuwa tofauti, hii ni mechi ya mashindano na ni lazima mshindi apatikane, tunawaheshimu KVZ, tutaingia na hesabu zetu ili tufuzu,” alisema Pele atakayemtegemea straika Mjamaica, Khori Bennet aliyeifungia bao lililoivusha hatua hiyo ilipolazimishwa sare ya 1-1 na Chipukizi ya Pemba iliyoaga mashindano..

Mbali na Mjamaica huyo aliyetua kikosini hivi karibuni, lakini ina nyota wengine waliobeba matumaini ya Mlandege katika kuitafuta nusu fainali, japokuwa ni lazima icheze kwa tahadhari kwani KVZ ni wepesi, ikimtegemea zaidi straika, Akram Omar ‘Haaland’ anayeisaka tuzo ya Mfungaji Bora.

Kocha wa KVZ, Ally Mohamed akizungumzia mchezo huo alisema muda unavyosogea timu yake inaendelea kuimarika na kwamba Jana wamefanya maandalizi ya mwisho wanayoaminj yatawapa ushindi.

“Timu yangu kadiri muda unavyosogea tunakuwa na ubora ambao tunautaka, tunakwenda kukutana na Mlandege ni kikosi kizuri kinachofundishwa na kocha mzuri, kila timu inataka kutinga robo fainali nadhani kikosi kitakachokuwa bora na bahati ya matokeo kitafuzu, sisi tumejipanga kisawasawa kwenda kutafuta ushindi,” alisema Mohamed.

KAZI IPO HAPA

Ikimalizika mechi hiyo ya saa 10:15 jioni, kazi itahamia saa 2:15 usiku wakati watu wakiwa wanajiandaa kupata mlo wa usiku baada ya swala wa Insha, Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga watavaana na mabingwa wenzao kutoka Rwanda, APR.

Yanga ambayo imekuwa na kikosi flani mseto chenye wachezaji wa kikosi cha kwanza na wale makinda kutoka timu ya vijana imechekelea hatua ya kumkwepa mtani wake, Simba nafasi ya kukutana nayo ikiwa ni fainali kama zitafuzu itakuwa na kazi mbele ya Wanyarwanda walioisumbua Simba juzi.

Kwenye mchezo wa kufungia makundi dhidi ya Simba, wanajeshi hao wa Rwanda waliupiga mpira mwingi, lakini kitu cha kuvutia ni kwamba Yanga walikuwa uwanjani kuwasoma na leo watashuka wakiwa wameshajua uimara na udhaifu wao katika pambano hilo la kukata na shoka.

Yanga imeonyesha haitaki masihara kwenye mchezo huo kuna uwezekano mkubwa ikapunguza makinda wake na kuwatumia wachache huku wazoefu wakiwa wengi baada ya nyota waliokuwa mapumziko kuitwa haraka visiwani Zanzibar.

Habari mbaya kwa Yanga ni kuendelea kumkosa winga mpya, Augustine Okrah ambaye aliumia mfupa wa pua kwenye mchezo wake wa kwanza akiwa na timu hiyo siku chache tangu asajiliwe.

Yanga licha ya kuwakosa mastaa wengine waliopo timu za taifa, lakini bado haijapoteza ubora wake wa eneo la katikati ya uwanja huku changamoto pekee itabaki kwenye beki ya kati ambayo watu wote wa kikosi cha kwanza hawapo.

Wachezaji walioitwa ni Salum Abubakar ‘Sure Boy’ aliyekuwa ameachwa Dar es Salaam, Yao Kouassi, Khalid Aucho na Pacome Zouzoua ambao Mwanaspoti lilishawahabarisha tangu jana kuwa wameitwa na Kocha Miguel Gamondi kutoka kwenye mapumziko waliyopewa hapo awali.

Kocha Gamondi, alisema jana, kila mchezo una ugumu wake ambapo wapinzani wao APR ni timu nzuri inayoundwa na wachezaji vijana wenye ari ya kusaka matokeo.

“Hakuna mchezo rahisi unajua ugumu wa hizi mechi zipo karibu karibu kila baada ya siku moja unatakiwa uingie uwanjani ucheze kwa kiwango kikubwa kwa kuwa ushindani ni mkali sana, tumewaona APR kama mnaoelewa mpira mnawaona walivyo na ubora lakini tutapambana nao,” alisema Gamondi.

APR ambayo inatumia zaidi pembeni ya uwanja kujenga mashambulizi yake ikiwa na watu wenye mbio Yanga kama itataka kulinda heshima yake itatakiwa kuwadhibiti wanajeshi hao eneo hilo sambamba na washambuliaji wao wa katikati.

Kocha wa APR, Mfaransa Thierry Frogger akizungumzia mchezo dhidi ya Yanga alisema wanakwenda kukutana na timu nyingine bora mbali ya  Simba ambapo wataingia na tahadhari zote ili watinge nusu fainali.

“Tutacheza na timu hizi kubwa mbili hapa Tanzania ndani ya siku tatu lakini kitu tofauti ni kwamba mifumo ya uchezaji ndio zinazitofautisha, haitakuwa mechi rahisi tumewaona Yanga wanavyocheza wana vijana na wale wenye uzoefu haitakuwa mechi rahisi tutatafuta akili ya jinsi ya kuweza kushinda mechi hiyo,” alisema Frogger.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live