Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakongwe wa dabi hawa hapa

MWAMNYETO MOHAMMED HUSSEIN Wakongwe wa dabi hawa hapa

Fri, 3 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jumapili nyasi za uwanja wa Mkapa zitakuwa na shughuli nzito kwa kuwakutanisha watani wa jadi Simba na Yanga mchezo utakaochezwa saa 11:00 jioni.

Katika mchezo huo ambao unateka hisia za mashabiki wengi hapa nchini wapo wachezaji ambao wamecheza mechi hizi zaidi ya mara tano hivyo hawana uoga nazo.

Makala hii inakuletea wachezaji ambao wameshacheza dabi takribani tano na sasa ni wakongwe kwenye mechi hizi.

JONAS MKUDE Ndiye mchezaji mkongwe zaidi ambaye amecheza dabi nyingi akiwa na kikosi cha Simba kwani alijiunga na timu hiyo (kucheza timu ya wakubwa) 2011 hadi 2023.

Amecheza dabi takribani 20 na msimu huu amejiunga na Yanga hivyo kama atakuwa sehemu ya kikosi cha kwenye mechi basi ataendelea na rekodi yake.

Mkude hajawa chaguo la kwanza kwa kocha wa Yanga, Miguel Gamondi kutokana na uwepo wa mastaa wengine kama Khaldi Aucho, Mudathir Yahya na Zawadi Mauya ambayo wamekuwa wakipewa nafasi ya kuanza mara kwa mara.

MOHAMED HUSSEIN 'TSHABALALA' Tshabalala alijiunga na Simba 2014 akitokea kikosi cha Kagera Sugar na hadi sasa tayari amedumu kwenye timu hiyo kwa miaka tisa.

Ni miongoni mwa wachezaji wakongwe kwenye timu ya Simba ambao wamedumu hadi sasa.

Tshabalala ni wazi amecheza takribani dabi 20 akiwa katika kikosi cha Simba na Jumapili anaingia akiwa ni mzoefu na nahodha wa timu yake katika dabi nyingine.

BAKARI MWAMNYETO Hana muda mrefu sana katika kikosi cha Yanga kwa sababu amesajiliwa na timu hiyo mwaka 2020 ambapo ameitumikia kwa miaka mitatu hadi sasa.

Mwamnyeto amecheza takribani mechi 10 za dabi katika mashindano yote hadi sasa.

Ni wazi kabisa beki huyu ambaye amekuwa mhimili mkubwa katika eneo la beki wa kati atakuwa na dabi nyingine Jumapili dhidi ya Simba.

Mwamnyeto ni nahodha katika kikosi cha Gamondi na amekuwa muongozaji mzuri kwa wachezaji kuhakikisha wanafanya kile wanachoelekezwa ndani ya uwanja.

JOHN BOCCO Tangu atoke Azam Fc hadi sasa 2023 ana miaka saba ndani ya Simba. Ana dabi takribani 20 katika mashindano yote ambapo Simba na Yanga zimekutana.

Bocco ni miongoni mwa wachezaji ambao wamecheza kwa muda mrefu katika Ligi Kuu Bara lakini leo hii na yeye ni sehemu ya wachezaji wakongwe kwenye dabi.

Msimu huu hajawa akipewa nafasi ya kuanza mara kwa mara katika kikosi cha Simba lakini kocha Robertinho kuna muda anamtumia na bado anaonyesha wazi bado ana kitu miguuni mwake.

DICKSON JOB Job kwa sasa ana miaka mitatu katika kikosi cha Yanga. Beki huyu alijiunga na timu hii Januari 11,2020 akitokea Mtibwa Sugar baada ya kununuliwa.

Huu ni mwaka wake wa tatu akiwa na Yanga na katika mashindano yote amecheza takribani dabi 10 ambazo zinamuweka katika orodha ya wachezaji wakongwe kwenye dabi.

Job ametengeneza uhimili wake mkubwa katika kikosi cha Yanga kwenye eneo la ulinzi iwe beki wa kati au kulia bado anafanya vizuri na wikiendi hii anatarajia kuwepo.

KENNEDY JUMA Kitasa cha maana lakini hakizungumziwi sana. Kennedy ni miongoni mwa wachezaji waliocheza dabi nyingi katika kikosi cha Simba.

Beki huyu alijiunga na Simba Julai 14,2019 na yupo hadi sasa akiwa na miaka mitano na kumfanya awe na dabi zisizopungua 18 akiwa na Simba.

Licha ya kwamba hana muda mwingi wa kucheza katika kikosi cha kwanza lakini bado amekuwa akilinda kiwango chake na akipewa nafasi basi huendelea kuonyesha shughuli nzito katika eneo lake la ulinzi.

KIBWANA SHOMARI Beki huyu alisajiliwa sambamba na Dickson Job wote kutoka Mtibwa ila ikiwa ni miezi tofauti, Job alisajiliwa Januari huku yeye Agosti.

Alipojiunga na Yanga hadi sasa ameshacheza mechi takribani mechi 11 za dabi hivyo anaingia kwenye ukongwe wa mastaa waliocheza mechi hizo nyingi.

Kibwana tangu msimu uliopita alianza kuwa kwenye wakati mgumu wa kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza lakini hilo halimuondoi katika wachezaji 18 watakaokuwa kwenye kikosi cha dabi.

AISHI MANULA Alijiunga na Simba tangu Agosti 9,2017 hivyo ana miaka sita kwenye kikosi hicho.

Manula kwenye miaka hiyo sita amekuwa ni kipa tegemeo kwenye kikosi cha Simba kutokana na pafomansi ambayo amekuwa akiionyesha.

Amecheza takribani mechi 20 akiwa na Simba na amejitengenezea rekodi tofauti tofauti akiwa na timu hiyo.

Mchezo wa Jumapili ni suala la kocha Robertinho kuamua kama kumpanga Manula au kuendelea kumuamini Ally Salim baada ya yeye (Manula) kutokuwa fiti akitoka kwenye majeraha.

WENGINE Mastaa wengine ambao ni wakongwe wa dabi ni Shomari Kapombe, Clatous Chama , Saidi Ntibazonkiza, Zawadi Mauya na Jesus Moloko.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live