Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakongwe wa Dabi wanusa jambo Simba vs Yanga

Dabi Pi Data Wakongwe wa Dabi waibua jambo Simba vs Yanga

Sat, 15 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati homa ya pambano ka watani wa jadi ikizidi kupanda kwa wachezaji wa timu zote mbili, mashabiki na viongozi, imeonekana vita kubwa katika mchezo huo itakuwa kwa mastraika dhidi ya mabeki.

Wachezaji wa zamani na makocha wazoefu wamesema kuwa mechi hiyo itakuwa na upinzani zaidi kwa mastraika na mabeki kutokana na na ubora waliona washambuliaji wa timu zote mbili waliongozwa na Fiston Mayele ya Yanga na Jean Baleke wa Simba.

Pia ubora wa Aziz Ki wa Yanga na Clatous Chama wa Simba nao umetajwa kuwa utaifanya dabi hiyo kuwa yenye mvuto. Beki wa pembeni wa zamani wa Simba, Said Sued' Panucci' anasema mechi hiyo itakuwa ngumu na yenye mvuto kwani Yanga watataka ushindi ili kujihakikishia ubingwa wakati Simba nao hawatakubali kufanywa daraja.

" Unajua raha ya ubingwa ni pamoja na umfunge mtani sasa Yanga wataingia uwanjani kutaka kufanikisha hilo lakini Simba ni ngumu nao kukubali kuwa wanyonge.

"Pia kutakuwa na upinzani mkubwa kwenye eneo la kiungo yaani ile vita ya Mzamiru Yassin wa Simba na Khalid Aucho wa Yanga iliyokuwepo kwenye mchezo wa kufuzu Afcon dhidi ya Uganda itarudi tena kila mmoja akitaka kuthibitisha kuwa ni bora.

"Kutakuwa na bato nyingine kwa mabeki na washambuliaji , beki ya Yanga dhidi ya Baleke ambaye ameonekana yuko kwenye ubora na safu ya ulinzi ya Simba dhidi ya Fiston Mayele ambaye makali yake yanajulikana, " anasema Sued na kuongeza

"Watu wanaweza kuona beki ya Simba ni mbovu hasa Onyango ambaye katika mchezo wa kimataifa dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco alicheza vibaya lakini lazima wajue kila binadanu huwa ana siku mbaya kazini na sio kila siku atafanya hivyo ndio maana hata Henock Inonga, Mwamnyeto, Dickson Job na wengineo kuna siku mpira unawakataa hivyo naamini bado Onyango anaweza kufanya vizuri katika hiyo mechi na akashangaza.

Naye kocha Mohammed Adolph Rishard anasema upinzani mkubwa katika mchezo huo utakuwa kwenye eneo la kiungo ambalo ndilo litaifanya timu kuwa bora.

"Mchezo wa dabi wa safari hii utakuwa wa kimataifa zaidi kwa sababu timu zote ziko moto kwenye michuano ya kimataifa na zimefanya vizuri hivyo natarajia kuona mechi ya kiwango. "Naamini mchezo huo utavutia zaidi kwenye safu za kiungo ambazo zina wachezaji wazuri ambao ndio wataamua timu zao ziwe kwenye ubora au zipotee, ngoja tuache dakika 90 ziamue, " anasema Rishald. Kocha Charles Boniface Mkwasa anasema hafikirii kuona mchezo wa kufunguka zaidi kwani timu zote zitajiimarisha kwenye ulinzi kutokana na kila timu kuwa na washambuliaji wazuri wenye uchu wa mabao.

"Kwa namna walivyocheza mechi zao za karibuni timu zote zilikuwa kwenye ubora lakini inapokuja dabi yanaangaliwa matokeo zaidi ya ushindi na huwezi kuona mpira mzuri. "Mechi iko wazi kwani kila timu ina kiwango bora kwa sasa na hasa eneo la ushambuliaji kila mchezaji anataka kufunga aonyeshe yeye mwamba(Mayele, Baleke, Aziz Ki, Chama ) hivyo itasababisha kuwa mechi yenye kujilinda zaidi, " anasema Mkwasa.

Naye mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Simba, Mohammed Hussein 'Mmachinga' anasema itakuwa mechi nzuri yenye ushindani mkubwa lakini ametoa angalizo kwa waamuzi kutoiharibu. "Kama waamuzi wakichezesha vizuri kwa haki basi hata wachezaji wataonyesha ubora wao na watu wanaona burudani nzuri.

"Burudani kubwa katika mchezo huo italetwa na washambuliaji wa timu zote mbili kwani wana mastraika wazuri na ndio itakuwa kupimo cha kuangalia umri wa mabeki. "Itakuwa vita ya mabeki dhidi ya mastraika ingawa Yanga safu yao yote ya ulinzi iko vizuri tofauti na Simba ambayo mabeki wao mmoja mmoja ndio wana kiwango.

"Mabeki wa Simba wanaweza kuigharimu timu yao kwa sababu ya umri walionao kwa sababu Yanga ina wachezaji wenye kasi sana hivyo wanatakiwa kuwa makini kujilinda, "anasema Mmachinga. Kocha mzoefu, Kennedy Mwaisabula "Mzazi" anasema Dabi za Simba na Yanga zina maajabu yake na usizibetie kwani hata timu yenye kiwango kwa wakati huo inaweza kupoteza mchezo.

"Mvuto wa mchezo huo ni jinsi timu zote zilivyo na wachezaji wazuri kutoka nje ya nchi hivyo mechi itakuwa yenye burudani. "Itakuwa mechi yenye upinzani mkubwa kati ya mabeki na mastraika. Baleke dhidi ya kina Job au Bacca na kama Phiri nae atakuwa yuko vizuri itakuwa balaa na Inonga dhidi ya Mayele itakuwa hatari kubwa, " anasema Mzazi Straika wa zamani wa Kagera Sugar na Azam, Phillipo Alando anasema kutokana na ubora w timu zote mbili kwa sasa itakuwa dabi ya kiwango.

"Ni dabi ambayo Itatia fora kwa kukutanisha wachezaji wengi wa kigeni, hivyo itakuwa balaa. "Katikati ya uwanja ndio kutaleta mvuti wa mechi hiyo kwani timu zote zitahitaji kumiliki mpira ili kupata wanachokitafuta, " anasema Alando. Naye kocha wa zamani wa Mbeya City, Yanga, Azam na Ihefu, Juma Mwambusi anasema mechi hiyo itakuwa na ushindani na vita kubwa ya kufunga kati ya Mayele na Baleke, Aziz Ki na Chama.

"Eneo la ushambuliaji litakuwa moto sana hivyo mabeki wa timu zote mbili wanatakiwa kujipanga kwa sababu washambuliaji wote ni wazuri, wana kasi, nguvu na wana maamuzi mazuri wanapolifikia lango, yaani wana uwezo wa kufunga hata wakiwa katika mazingira magumu hivyo watanogesha mchezo huo. " anasema Mwambusi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live