Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakongo walivyoteka shoo Bara

Bangala, Mayele Tunis.jpeg Wakongo walivyoteka shoo Bara

Sat, 10 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Msimu wa 2022/2023 wa Ligi Kuu Bara unafikia tamati Juni 9, mwaka huu huku kila timu ikivuna kile ambacho ilipanda.

Yanga imetetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Bara iliouchukua msimu uliopita huku Maafande wa Ruvu Shooting ikiwa ndio timu pekee hadi sasa ambayo imeshuka daraja na kwenda Championship baada ya matokeo mabovu mfululizo.

Wakati ikibakia michezo miwili, Mwanaspoti linakuletea mastaa kutoka Congo wanaocheza Yanga na Simba ambao wamekuwa na msimu mzuri.

FISTON MAYELE (YANGA)

Unapotaja mafanikio ya Yanga msimu huu hutoacha kulitaja jina la mshambuliaji wa timu hiyo, Fiston Mayele ambaye kwa kiasi kikubwa amechagia kutokana na uwezo wake mkubwa aliojaaliwa wa kuweza kupachika mabao.

Hadi sasa nyota huyo ndiye kinara wa mabao akifunga 16 ya Ligi Kuu Bara na kuiwezesha timu hiyo kutetea taji lake ililolichukua msimu uliopita na mbali na hilo ila ameisaidia kufika hadi fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Wakati Bongo akiwa na nafasi ya kutwaa kiatu cha ufungaji bora ila hadi huko kwenye Kombe la Shirikisho moto wake pia sio mchezo kwani bao lake kwenye mchezo wa fainali dhidi ya USM Alger limemfanya kuongoza akiwa na saba.

Kama haitoshi bao moja alilolifunga dhidi ya Singida Big Stars kwenye mchezo wao wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) linaonyesha ni jinsi gani nyota huyo amekuwa mhimili mkubwa ndani ya kikosi hicho.

JEAN BALEKE (SIMBA)

Ingawa Simba imemaliza msimu bila taji lolote ila hutoacha kutaja kiwango bora kilichoonyeshwa na nyota wa timu hiyo, Jean Baleke kwani licha ya kujiunga dirisha dogo la Januari mwaka huu ila moto wake umekuwa ni gumzo.

Baleke alijiunga na Simba kwa mkopo akitokea Nejmeh ya Lebanon ambayo pia ilikuwa inamtumia akitokea Klabu ya TP Mazembe na hadi sasa nyota huyo amekuwa mwiba kwa makipa ambapo amefunga mabao manane kwenye Ligi Kuu Bara.

Straika huyo amekuwa mchezaji wa nne kwa miaka ya karibuni kutoka nchini Congo kukipiga Simba, akitanguliwa na mastaa wenzake Deo Kanda, Chris Mugalu anayecheza kwa sasa Irak na Henock Inonga anayeendelea kuichezea.

DJUMA SHAABAN (YANGA)

Ndiye beki wa kulia wa sasa wa Yanga akiwa anaichezea timu hiyo akitokea AS Vita ya DR Congo ingawa ile kasi yake imepungua ukitofautisha na alivyokuwa mwanzo hali iliyosababisha kutokucheza kikosi cha kwanza mara kwa mara.

Uwepo wake umekuwa ni chachu kwani ameisaidia timu hiyo kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya pili mfululizo, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), Ngao ya jamii hivyo kuifanya Simba kumaliza bila taji lolote.

Djuma ni beki anayegombea namba sambamba na beki kiraka mzawa Kibwana Shomari ambaye anamudu kucheza upande wa kushoto.

JOYCE LOMALISA (YANGA)

Huyu ni beki wa kushoto aliyetua Jangwani msimu uliopita akitokea klabu ya FC Onze Bravos do Maquis ya Angola.

Mwanzoni alichukuliwa kawaida, pengine alisajiliwa akitokea kwenye majeraha, lakini kwa sasa moto wake ni balaa kiasi wale waliokuwa wakimbeza wameamua kumkaushia kwa soka analopiga hasa kupandisha timu na kupiga krosi.

Beki huyo anabadilishana namba na nyota wengine wanaocheza upande wa kushoto, wakati mwingine na Kibwana Pia kuna muda anapishana na David Brayson na winga Farid Mussa ambaye naye amekuwa hana nafasi mara kwa mara.

HENOCK INONGA (SIMBA)

Ukiachana na Simba kutotwaa taji lolote msimu huu ila hutoacha kutaja jina la beki wa kati, Henock Inonga ambaye licha ya uwepo wa mastaa wengi wanaocheza nafasi hiyo ila ameendelea kuwa muhimili mkubwa kikosini.

Inonga ambaye alichukua tuzo ya beki bora msimu uliopita ameendelea kuonyesha makali yake ndani ya timu hiyo msimu huu chini ya Kocha Mkuu, Roberto Oliveira 'Robertinho' akishirikiana na mkongwe Mkenya, Joash Onyango.

Kuonyesha uwezo alionao mbali na kuzuia ila pia nyota huyo ana uwezo mkubwa wa kufunga mabao kwani hadi sasa amefunga matatu akimzidi Kibu Denis ambaye licha ya kuzungumzwa sana na mashabiki ila amefunga mawili tu.

YANNICK BANGALA (YANGA)

Tangu ajiunge na kikosi hicho akitokea FAR Rabat ya Morocco, Bangala ni moja kati ya wachezaji muhimu sana akimudu kucheza beki wa kati akishirikiana na Bakari Mwamnyeto, Dickson Job na Ibrahim Mohamed 'Bacca'.

Mbali na kucheza beki wa kati ila ana uwezo mkubwa pia wa kucheza kama kiungo mkabaji jambo ambalo limekuwa ni faida kwa kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi katika machaguo ya kikosi chake kutokana na mpinzani anayecheza nae.

Bangala aliyechukua tuzo ya mchezaji bora msimu uliopita mbali na kucheza beki au kiungo ila amefunga mabao mawili ya Ligi Kuu Bara.

TUISILA KISINDA/ JESUS MOLOKO (YANGA)

Wanamuita Tuisila Kisinda 'TK Master' ambaye katika msimu wake wa kwanza Yanga alikuwa ana kasi, chenga na kupiga krosi zilizoibeba Yanga katika Ligi Kuu Bara na hata kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Baadaye aliuzwa RS Berkane ya Morocco na kutwaa nayo Kombe la Shirikisho Afrika kabla ya Yanga msimu huu kumrejesha ila akiwa amepungua makali.

Unaweza kumuanzisha winga ya kulia na kama utaona vipi, mbadala wake aliyesajiliwa msimu uliopita wakati TK alipouzwa, yaani Jesus Ducapel Moloko naye ni fundi haswa kwenye wingi hiyo sambamba na ile pia ya kushoto.

Chanzo: Mwanaspoti