Kama Dodoma Jiji itapata ushindi katika mchezo dhidi ya Simba kila mchezaji atapewa Sh1.5 milioni na uongozi wa timu hiyo.
Dodoma Jiji itacheza dhidi ya Simba saa 1 usiku katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uwanja wa Jamhuri.
Kiongozi wa juu wa timu hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema wameamua kufanya hivyo ili kuleta motisha kwa wachezaji.
MASHABIKI KIDUCHU
Mashabiki wachache wamejitokeza kukata tiketi kwa ajili ya kuangalia mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Dodoma Jiji na Simba.
Sehemu za kukatia tiketi zilizopo upande wa magharibi mwa uwanja wa Jamhuri kuna watu wachache ambao wanakata tiketi.
Mwanaspoti imeshuhudia mashabiki wachache wakijitokeza kukata tiketi huku baadhi wakidai sababu kubwa ya kuwa wachache ni kutokana na mechi kuchezwa usiku.
Ramadhan Juma amesema baadhi ya mashabiki wa Simba Mkoa wa Dodoma wapo vijijini hivyo wameona mechi kuchezwa usiku ni shida kwao na watakosa usafiri wa kuwarudisha katika maeneo yao.
"Mimi natokea Mpwapwa mechi saa moja usiku mpaka imalizike saa tatu usiku narudije Mpwapwa, nimekuja kwa sababu nina gari yangu binafsi," amesema Juma.