Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakiamua, mbona wanatoboa freshi tu

Simba X Kapama Wakiamua, mbona wanatoboa freshi tu

Sat, 8 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Sikumbuki mwezi, lakini ilikuwa 2007 Simba ilifanikiwa kumsajili beki wa kati mwenye mwili jumba kutoka Tusker ya Kenya. Namzungumzia George Owino aliyewahi pia kukipiga Yanga kwa misimu miwili tofauti baada ya kukiwasha sana tu pale Msimbazi.

Ni beki mmoja aliyekuwa mpole wa sura, lakini mkali uwanjani kwa namna ya kuwadhibiti washambuliaji wasumbufu. Kwa sasa jamaa kastaafu soka akiwa na umri wa miaka 42.

Mara ya mwuisho kuwepo uwanjani ilikuwa 2019 akiichezea Mathare United baada ya kukiwasha sana tu pale Sofapaka, moja ya timu iliyotetesha soka la Kenya na ukanda wa Afrika Mashariki kabla ya kuzimika.

Simkumbuki Owino kwa sababu ya soka lake, la! Namkumbuka kwa vile niliwahi kufanya mahojiano naye kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) mara alipotua Msimbazi.

Katika mahojiano hayo alikizungumza kitu ambacho, mwanzoni sikukutilia maanani. Nilijua ni mbwembwe tu za Wakenya.

Beki huyo alisema kwa utulivu nilivyomuuliza anaonaje vipaji vya soka vilivyopo nchini hususani ndani ya timu yake ya Simba (wakati huo).

"Tanzania ina vipaji vingi, tena havijalelewa kwenye misingi ya soka, lakini vinajua kucheza soka na lau kama wangepitia kwenye hizi akademia kama ilivyo kule kwetu au kwa Uganda, naamini wangekuwa mbali kuliko nchi yoyote kwa ukanda wa Afrika Mashariki," alisema Owino na kuongeza kipindi hicho;

"Nipo hapa Simba kwa muda mfupi, lakini nimebaini Watanzania wanajua sana soka, tatizo lao ni moja tu, wengi wa wachezaji hawajui thamani yao. Hawajui wapo kwenye soka kwa sababu gani, ila nafurahia kucheza hapa na kukutana na wachezaji wenye vipaji na uwezo mkubwa uwanjani."

Hapa chini ni makala inayoeleza kitu gani ambacho kinakwamisha nyota wengi wa Tanzania kushindwa kuwika kwa muda mrefu na kufika mbali kisoka licha ya kuwa na vipaji maridhawa ambavyo kama wangevitumia kwa ufanisi huenda tungekuwa na kina Mbwana Samatta na Simon Msuva wengi kama sio Dismas Novatus wanaopeperuisha bendera ya taifa, nje ya bara la Afrika.

KAMA UTANI VILE

Ukisikia kelele za mashabiki wanavyozungumzia wachezaji wazawa dhidi ya wageni utahisi kama Tanzania hakuna vipaji.

Wakati mwingine unapata ugumu kuendelea kuwajadili nyota wa zamani kwa namna walivyojitoa na kujituma uwanjani kulingana na nyota wa zama hizi.

Wadau bado wanawajadili kina Edibily Lunyamila, Mohammed Hussein 'Mmachinga', Madaraka Seleman, Innocent Haule, Zamoyoni Mogella, Said Mwamba 'Kizota', Said Mrisho 'Zico wa Kilosa', Makumbi Juma, Mabvumbi Omary, Mohammed Mwameja na wengine kila uchao.

Hukisikia wakiwajadili nyota wa sasa basi ni wale wa kigeni na kazi kubwa wanayoifanya uwanjani, hata kama kuna wachezaji wa sampuli ya kina Ismael Sawadogo, Victor Akpan, Lazarious Kambole na wengine ambao hawakuwa na maajabu.

Wazawa wanazungumzwa kwa uvivu walionao na kushindwa kuchuana na wageni na kuishia kusingizia kupigwa miba, sijui kutopendwa na makocha na kujikita kwenye starehe za kila aina.

Kukwama kwa mastaa wazawa ndiko kunakoifanya Tanzania kwa miaka kibao tangu ipate uhuru kwenda fainali mbili tu za Afcon na mbili nyingine za Chan kulinganisha na majirani zao au mataifa mengine ya Afrika yanayopisha kila msimu kwenda kwenye michuano hiyo ya Mataifa ya Afrika.

Tulienda fainali za Afcon 1980 kule Nigeria kwa kikosi cha zamani, Simba ilifika nusu fainali ya Klabu Bingwa (ssa Ligi ya Mabingwa Afrika) 1974 kwa mastaa wazawa watupu, mwaka 1993 ilicheza fainali za Kombe la CAF ikiwa na wazawa watupu.

Yanga ilicheza makundi ya Ligi ya Mabingwa 1998 ikiwa na wageni wachache, kikosi kilijaa mastaa wazawa. Kilimanjario Stars ilibeba taji la Chalenji 1994 jijini Nairobi Kenya. Simba ilifika makundi ya Ligi ya Mabingwa 2003 kwa kuivua taji watetezi, Zamalek ya Misri ikiwa na wazawa watupu isipokuwa Ramadhan Wasso.

Kifupi wazawa enzi hizo walikimbiza na kuzifanya klabu za Tanzania kutotegemea wageni na hata hizi kelele kwamba wageni wanaiangusha Taifa Stars haikuwepo.

Hakuna anayejua kitu gani kimelikumba soka la Tanzania na kushuka kwa wazawa na kuishia sasa kutegemea wageni kwa kila kitu ili kufikia mafanikio, kwani hata Yanga imefika fainali za Kombe la Shirikisho Afrika ikibebwa zaidi na wageni.

Simba imetinga robo fainali za CAF katika misimu mitano mfululizo kwa nguvu ya mapro wa kigeni, huku Stars imefika fainali za Afcon 2019 kwa nguvu ya Uganda The Cranes na fainali za CHAN 2009 na 2020 tu. Tatizo ni nini wakati soka la sasa linaendeshwa kisasa zaidi na wachezaji wana uwezo wa kujifunza mbinu tofauti na zamani? Hakuna anayejua!

UKWELI ULIVYO

Kutokana na kuonekana kuwa na tatizo kubwa hasa katika ubora wa wachezaji wazawa, Mwanaspoti limefanya uchunguzi wa kina juu ya tatizo hilo ili kubaini sababu za wachezaji wa sasa kuonekana kuwa na viwango duni hasa wanapofananishwa na wale waliotamba zamani.

Kitu cha kwanza kilichobainika ni kwamba wachezaji wengi wa zama hizi wanapenda starehe zaidi pengine kuliko kazi yao ya msingi ya soka.

Wachezaji hawa wamekuwa wakionekana katika kumbi mbalimbali za starehe nchini wakila bata tena wakati mwingine timu wanazozichezea zikiwa na majukumu makubwa ya mechi za Ligi Kuu ama michuano mingine mbalimbali za ndani na za kimataifa. Wachezaji ambao wamekuwa wakifanya mazoezi asubuhi pekee na kupumzika jioni, wamekuwa wakipata muda mwingi wa kupumzika na kujivinjari katika kumbi hizo, jambo ambalo linawafanya kushindwa kutumika vizuri uwanjani.

Starehe hizi zinaharibu miili ya wachezaji ambayo hukosa utimamu wa kutosha na wanapolazimika kucheza soka la nguvu hushindwa na kuonekana kuwa wameshuka viwango.

Mbwana Samatta aliwahi kufanya mahojiano na Mwanaspoti akiwa Genk kipindi hicho na kusema kuwa, kule Ulaya hakuna kuchungwa au kuweka kambini kama ilivyo kwa timu nyingi za haopa nchini hasa Simba na Yanga. Mchezaji aelekezwi ale nini au afanya kitu gani, isipokuwa ni jukumu la kila mchezaji maadamu ni mchezaji wa kulipwa kujichunga mwenyewe.

Samatta alisema ndio maana alikuwa na mpishi wake binafsi aliyekuwa anamuandalia chakula kulingana na mahitaji aliyonayo na hakuwa na mambo mengi atokapo mazoezini au kwenye mechi zaidi ya kurejea kwenye maskani yake na kujipanga kwa mazoezi na mechi nyingine bila uangalizi wa mtu maalumu au kocha.

"Ukijiachia na kunenepeana au kujichosha, utajihukumu mazoezini na kwenye mechi, huku watu wanaishi kivyao, lakini wapo makini kwani kama mchezaji wa kulipwa ni lazima ujue unatakiwa kufanya nini, ukizembea kidogo inakula kwako," alisema Samatta alipohojiwa na Edo Kumwembe.

MITANDAO YA KIJAMII

Unaweza kushangaa, lakini ukweli ni kwamba mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram na WhatsApp zinaonekana kuwa sumu katika soka la bongo. Wachezaji wengi wa timu za Ligi Kuu na hata madaraja mengine ya nchini wamekuwa wakitumia muda mwingi katika mitandao hiyo na kukosa muda wa kutosha kupumzika.

Inashangaza sana, kwani kuna wakati mwingine wachezaji hawa huwa bize na mitandao ya kijamii hadi majira ya usiku wa manane wakichati kiasi cha kuwafanya walale mida mibovu mno.

Kwa mfano, imebainika wapo nyota wengi wa soka nchini ambao wakuwa bize na Facebook na Instaghram hadi usiku mwingi wa saa 7 au 8 usiku wakati siku inayofuata ana programu ya mazoezi asubuhi ama kuwa na mechi za ligi na michuano mingine inayioshiriki timu zao.

Wachezaji wengine wamekuwa wakioneakena WhatsApp na Telegram kama sio Instagram hadi usiku huo mkubwa jambo ambalo linaashiria kuwa wachezaji wengi huwa hawapumziki.

Viashiria vya baadhi ya wachezaji kushindwa kumudu mazoezi vizuri wakati wa asubuhi kumeonekana pia kuhusisha mitandao hii moja kwa moja.

Kuna baadhi ya klabu za soka nchini zimekuwa zikiwabana wachezaji kwa kuweka masharti magumu juu ya mitandao ya kijamii ili angalau kuwafanya wapate mapumziko kwa kuwalipisha faini za fedha ndani kwa ndani, lakini wengi wanakwama kwa vile wachezaji ni watu wazima hawachungiki kama watoto wadogo au wanafunzi.

MAPENZI

Hakuna ubishi wapo wachezaji wachache wa timu za Ligi Kuu wanaojiheshimu na kujua mipaka yao kama vioo vya jamii, lakini wengine wengi wamekuwa wakifanya mapenzi bila utaratibu maalumu. Wachezaji hawa kutokana na kuwa na umaarufu mkubwa, wamekuwa wakijizolea rundo la wanawake ambapo huwafanya kutumika kupita kiasi na kushindwa kumudu kazi yao. Bahati mbaya wenyewe wanaona ni sifa kupapatikiwa na mademu wakiwamo mijimama inayowalea, lakini bila kujua kama wanajiua kisoka kwa kutofanya kwa kiasi.

Mwanaspoti lilipata kisa cha wachezaji tofauti mmoja anayecheza nafasi ya beki na mwingine kiungo mshambuliaji kutoka klabu mbili tofauti kubwa nchini ambao walicheza msimu mmoja na kuwika kabla ya kuporomoka na kutolewa katika klabu hizo kwa sababu yab kuendekeza ngono.

Yaani kwa umri walionao na mijimama iliyokuwa nayo, ilichangia kuwafanya washindwe kabisa kucheza kama ilivyowahi kumkuta mmoja ya nyota aliyekuwa akiibuka kwa kasi katika moja ya klabu za Kariakoo aliyepotea kwa sababu ya kuendekeza mijimama hadi kuingia anga za mabosi wake.

Visa vingine vilibainika pia kwa wachezaji ambao walishindwa kujizuia kutokana na kupapatikiwa na wasichana kadhaa hivyo kujikuta wakitumbukia katika dimbi la mahaba ambalo linaua viwango vyao na pia kuwafanya wasiwe makini tena na kazi zao. Ikumbukwe kuwa, kufanya mapenzi kwa kiasi inaelezwa kama ni njia nzuri ya kuwafanya wachezaji kuwa na utulivu mkubwa uwanjani, lakini sio kuendekeza kiasi cha kumfanya mchezaji ashindwe hata kupiga mpira kutokana miguu kukosa nguvu.

UVIVU WA MAZOEZI

Hili ni tatizo kubwa kwa wachezaji wengi wazawa. Hawapendi mazoezi hasa yle magumu. Hili lipo tena kwa wachezaji wengi hasa wale wenye majina makubwa. Mara kadhaa imeripotia na Mwanaspoti limeshuhudia wachezaji wenye majina makubwa kadhaa wakitegea mazoezi wanayopewa na makocha wao tena wengine wakijificha kabisa nyuma ya wachezaji wenzao ili wasionekane.

Jambo hili la aibu hufanywa na wachezaji hao mara kwa mara hivyo kuwaweka katika wakati mgumu wa kufanya vizuri na kuisaidia klabu na hata timu ya taifa. Mara kadha kwenye viwanja vya mazoezi imekuwa ikishuhudiwa wachezaji kadhaa wa klabu kubwa wakitegea mazoezi hayo hasa kutokana na kuwa na majina makubwa katika timu zao na kuwa na imani ya kupewa nafasi na makocha wao.

Hali hii huwa mbaya zaidi pale baadhi ya wachezaji kujidai kuwa wana majeraha ili waondolewe tu katika programu za mazoezi na kupata muda wa kupumzika kumbe hawana ugonjwa wowote. Hili limekuwa likishuhudiwa katika timu kubwa hasa kutokana na kukosekana kwa usimamizi madhubuti wa mazoezi.

Wachezaji wengi wa zamani wanaeleza kuwa wakati huo ilikuwa ni jambo gumu kumpata mchezaji anayetegea mazoezi.

Kwa miaka ya nyuma kuna baadhi ya wachezaji walikuwa wakijifanyia mazoezi wenyewe mitaani kabla ya kwenda kuungana na wenzao kambini. Bakar Malima 'Jembe Ulaya' na wengine tulikuwa tunawaona ufukwe wa Coco wakijifua. Juma Kaseja na Shaaban Kado ilikuwa ni rahisi kuwakuta Uwanja wa Mwenge Vinyago wakijifua hata wakati timu zao hazipo kambini. Kwa sasa wachezaji wamekuwa wavivu wakisubiri kupigishwa tizi na makocha wao tu mazoezini na sio kufanya binafsi.

Pia wanapokuwa na kocha anayekomaliza programu za mazoezi na kuwapigisha tizi la nguvu kubwa, visingizio huwa haviishi na wengine kumfanyia zengwe kocha wa aina hiyo ili atemwe na kuja kocha anayewafanyia mazoezi mepesi na asiyewafuatilia kiviiile wakidhani inawasaidia kulinda vipaji vyao.

MICHEZO SHULENI

Kwa wadau wanaofuatilia soka tangu miaka ya nyuma watakubaliana kwamba mfumo wa zamani wa michezo shuleni unatofautiana kwa kiasi kikubwa na ulivyo sasa. Hata michezo ya mashule kama Umitashumta na Umisseta ya sasa sio kama ile ya enzi za Mwalimu, ambapo wachezaji walitengenezwa tangu chini na kuja kuwa nyota na tegemeo kwa taifa.

Vipaji vingi viliibukia kwenye mashindano hayo ya Shule ya Msingi na Sekondari na hata vyuoni na kuja kulitumikia taifa baada ya kusajiliwa kwenye klabu mbalimbali za soka nchini.

Ukaja mzomu mbaya wa siasa kwa michezo kufutwa shuleni na kuchangia kwa kiasi kikubwa kupoteza viopaji vingine na kuporomosha mafanikio ya soka na michezo mingine nchini kwa ujumla.

Kufutwa kwa michezo kuliibua tatizo kubwa kwa soka la Tanzania kutokana na michezo iliyokuwa maarufu mashuleni ya Umisseta na Umitashunta kufutwa kipindi cha nyuma na hata iliporejeshwa imekuwa haina mvuto tena. Wachezaji wengi wa zamani walitokana na michezo hiyo ambayo kwa wakati huo ilikuwa na mvuto wa kipee kabla ya kufutwa enzi za Utawala wa Awamu ya Tatu iliyokuwa chini ya Benjamin Mkapa. Kwa sasa ni nadra kusikia michuano hii imezalisha mchezaji mahiri tena.

Mbali na hilo, baadhi ya wadau wa soka waliokuwa wakisaka vipaji katika shule hizo za Msingi na Sekondari wameshindwa kuzitembelea tena hivyo kuifanya michuano hiyo kuwa ya kawaida. Jambo hili limesababisha vipaji vingi vya maana kupotea huku wale wanaoibuka wakiwa wanaibuka umri ukiwa umeshasonga.

Kwa sasa Tanzania inategemea michuano ya michache ya vijana baada ya kutowekwa kwa Copa Coca Cola, Uhai Cup na Airtel Rising Stars kupata vipaji, hata kama ado michuano hii pekee imeshindwa kuzalisha vipaji katika umri sahihi. Wachezaji wanaoibuka katika michuano hii inawachukua muda mwingi zaidi kuweza kufanya vizuri.

TAIFA CUP IREJESHWE

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imeamua kukomalia Ligi za Vijana U15, U17 na U20, lakini bado haiendeshwi kwa ufanisi kutokana na chuprichupri nyingi zilizopo kwa baadhi ya klabu kuchezesha vijeba waliobadilishiwa umri, lakini wakisutwa na ukomavu wa sura na miili yao.

Klabu zimekuwa zikiendeshwa kijanjajanja kwenye soka la vijana tofauti na miaka ya 1970-2000 klabu zilipokuwa na timu za watoto (kids) na zile za Vijana marufu kama timu B zilizochangia kuibua vipaji vilivyiopelekea Tanzania kwenye fainali za Afcon 1980.

Lakini wakati ikiendelea kuboresha soka hilo na hasa Ligi Kuu zinazotambulishwa kwa vijana, TFF irejee makabrasha ya ahadi zake kwa viongozi waliopo kabla ya kuchagiliwa katika chaguzi zilizopita kwa kurejesha michuano ya Kombe la Taifa (Taifa Cup).

Michuano hii kwa kiasi kikubwa ilichangia kuibua vipaji vilivyo nje ya klabu za soka hasa zile maarufu ambao baadaye walikuwa kuwa tegemeo kwa taifa kwenye michuano ya kimataifa.

Utabisha nini wakati Mohammed Chuma aliibuliwa Mtwara kupitia michuano hiyo akitolewa kijijini kabisa na kuja kuwa beki wa kushoto tegemeo kwa miaka 10 mfululizo akiwa hajawahi kutemwa wala kuwekwa benchi hadi alipostaafu!

TFF ikitaka kurejesha heshima ya soka la Tanzania na kuibua vipaji tofauti na ule mfumo waliokuja nao enzi za Jamal Malinzi wa Stars Maboresho ni kuirudisha tena michuano hiyo ya Kombe la Taifa na kutengeneza mfumo mzuri wa kuchezwa tofauti na uliowekwa mara ya mwisho kabla hayajafa.

Katika mfumo huo, Taifa Cup ilikuwa na kanuni za hovyo vya kutaka kila mchezaji hasa wa Ligi Kuu kwenda kuchezea mkoa anakotokea au kuichagua timu za kuchezea. Ikiletwa kwa mfumo mzuri wa kutafutwa timu za mikoa huko huko zilipo kwa vipaji vipya kisha kuongezwa nguvu na wachezaji wachache wa timu zilizopo kwenye mkoa husika, inaweza kurejesha moto mkali uliokuwa zamani na ulioibeba nchi kwenye soka la kimataifa, kwani Tanzania ina vipaji.

MABORESHO LIGI ZA CHINI

Kwenye ligi za chini kuanzia Championship, First League, Mabingwa wa Mikoa (RCL) na zile za ngazi za Mikoa ikiboreshwa na kutengenezewa mazingira kama ya Ligi Kuu, kuna uwezekano mkubwa wa kuibua vipaji vitakavyoleta mapinduzi katika soka la Tanzania.

Hizi kelele za kwanini kina Fiston Mayele, Saido Ntibazonkiza kama sio Clatous Chama na Prince Dube kuimbwa sana na mashabiki zitaisha kwa vile ligi hizo zinachezwa sana na wazawa wenye uwezo, lakini wanakwama kutokana na ligi hizo kuendeshwa kama mabonanza na sio ligi halisi.

TFF ipambane kutafuta wadhamini na kuifanya ligi hizo zile na hadhi zinazochangia kuongeza nguvu kwenye Ligi Kuu kwa vile zinazotoka huko ndiko zinazokuja kucheza Ligi Kuu, hivyo kama zinapanda timu goigoi na zisizojua thamani ya Ligi, ni ngumu kulisaidia soka la Tanzania.

Lakini kubwa ni wadau kwa ujumla kuelekeza nguvu ya pamoja kuhakikisha soka la Tanzania linasonga mbele kwa wazawa kujengwa kisoka ili kuweza kuchuana na hawa wageni na hata ikiwesekana kuwafunika kwa hata Juma Nature aliwahi kuimba

'Wao waweze wana nini na sisi tushindwe tuna nini....? Soka ni mchezo wa wazi na ukipatia wala huna haja ya kujipata kwani kila mtu anakiona, wazawa wana uwezo mkubwa, ila baadhi ya matatizo ni hayo yaliyoainishwa yakiyaacha na kisha kutengenezwa mazingira ya kuwarahisishia kazi, kila kitu kitakuwa mswano!

Chanzo: Mwanaspoti