Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakenya wanavyotawala soka la wanawake Bongo

Wakenya Wakenya wanavyotawala soka la wanawake Bongo

Wed, 7 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu Bara kuna rundo la wachezaji wanaotoka taifa la dr Congo na wanafanya vizuri wakipishana kila msimu. Hata hivyo, wakati Wacongo wakitajwa sana kwenye ligi hiyo, Ligi Kuu ya Wanawake nchini wanaotajwa zaidi ni Wakenya na ndiyo inayoongoza kuwa na wachezaji wengi kutoka nchi hiyo.

Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), inakua kwa kasi na wachezaji kutoka mataiofa mbalimbali wanaikimbilia huku pia ikitajwa kuwa na maokoto yanayowafanya wakimbie ligi zao kuja kujiunga na miamba ya soka la wanawake nchini.

Wachezaji wa Kenya wametawala kwenye ligi hiyo na Simba Queens na Bunda Queens ndizo zinazoongoza kuwa nao wengi na wanafanya vizuri kwenye timu zao hizo.

Kwa sasa kwenye ligi hiyo kuna wanasoka 15 wa kike kutoka Kenya wanaocheza soka la kulipwa Tanzania ikiwa na wachezaji walioko Simba (5), Fountain Gates Princess (2), Yanga (3) na Bunda Queens (5).

SIMBA QUEENS

1. Corazone Aquino Msimu wake wa nne akiwa na wanamsimbazi wa kike tangu ajiunge mwaka 2020 akitokea Gaspo Youth ya Kenya. Alikuja nchini kujitafuta baada ya janga la Corona na ligi za nchi hiyo zilisimama kwa muda mrefu kipindi hicho tofauti na nchi nyingine zilizoruhusu michezo kuendelea licha ya janga hilo ila kwa tahadhari kubwa.

Corazone amekuwa kiungo tegemeo wa Simba Queens na tangu ametua nchini amekuwa na kiwango bora ambacho kimemfanya acheze hadi sasa na kama ilivyo kwa Wakenya wenzake, maokoto pia ni kilichomleta huku ingawa kwenye eneo lake la kazi anafanya vyema na hadi sasa msimu huu amecheza mechi saba na kufunga mabao matatu.

2. Elizabeth Wambui

Huu ni msimu wake wa kwanza tangu alipojiunga na Simba Queens akitokea Gaspo Women inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya. Ubora wa ligi kuu nchini ndio sababu za kimbilio lake huku ikiwamo maokoto na ukubwa wa timu utakaomwezesha kupiga hatua zaidi ikiwa atafanya vyema na timu hiyo.

Winga huyo hadi sasa hajafunga bao lolote lakini ametoa assist mbili kwenye mechi saba za ligi na ameonyesha kiwango bora.

3. Caroline Rufaa

Kipa namba moja wa Simba Queens akiwaweka benchi Gelwa Yona, Janet Shija na Zubeda Mgunda ambao walikuwa bora. Ameleta ushindani mkubwa kwenye kikosi hicho katika nafasi ya kipa na kuifanya timu hiyo kuwa na ubora eneo hilo.

Alijiunga na Wekundu mwaka 2022 akitokea Fountain Gate Princess na huko alikuwa moto ambako nako alikuwa kipa tegemeo.

4. Jentrix Shikangwa

Ukitaja jina la straika Jentrix, wadau na mashabiki wa soka la wanawake wanamfahamu vizuri namna anavyojua kucheka na nyavu za wapinzani.

Mkenya huyo alijiunga na Simba msimu wa 2022/2023 akitokea Vihiga Queens ya nchini kwao na kufanya vizuri na kutwaa kiatu cha ufungaji bora akiweka kambani mabao 19.

Baada ya kufanya vizuri msimu huo akatimkia Beijing Professional FC ya China kwa mkataba wa miezi sita na baada ya kuisha msimu huu karejea tena akiwa tayari amefunga mabao manne kwenye mechi mbili.

Ujio wake nchini umeleta ushindani ndani ya kikosi hicho chini ya Kocha Mkuu, Juma Mgunda kwani nafasi yake yupo Aisha Mnuka na Asha Djafar ambao nao wamekuwa na mwanzo mzuri.

5. Ruth Ingosi

Alikuwa miongoni mwa wachezaji wanne waliojiunga na Simba pamoja na Situma, Vivian na Shikangwa akitokea Lakatamia inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Cyprus. Akiwa Kenya alikipiga kwenye timu ya Eldoret Falcons inayoshiriki ligi kuu. Msimu huu klwenye Ligi Kuu ya Wanawake nchini amekumbana na ushindani nkwenye kikosi cha Simba Queens ingawa ana uwezo na nafasi yake wanacheza wazawa, Fatuma Issa ‘Fetty Densa’ na Violeth Nickolaus.

YANGA PRINCESS

1. Wincate Kaari

Ni beki wa kulia na msimu huu haukuwa mzuri kwake baada ya kukaa nje kwa miezi mitatu akiiguza majeraha na amerejea kwenye mchezo wa Ligi dhidi ya Geita Gold timu huyo ilipoondoka na ushindi wa mabao 2-0.

Kutokana na kuwa na umuhimu kwenye eneo la ulinzi Yanga hawakumuacha dirisha la usajili licha ya kupata majeraha hayo.

Alisajiliwa akitokea Thika Queens inayoshiriki Ligi Kuu ya wanawake Kenya na ni mmoja wa nyota wa nchi hiyo waliokuja kutafuta ugani nchini na kazi yao siyo mchezo wakiwafunika baadhi ya wazawa.

2. Janet Moraa Bundi

Amejiunga na Yanga Desemba mwaka huu akitokea Vihiga Queens ambako alikuwa mfungaji bora akiweka kambani mabao manne kwenye mechi tano.

Tangu ajiunge na wananchi hao ameingia kwenye kikosi moja kwa moja na tayari amefunga mabao mawili kwenye mechi sita akionyesha kiwango bora na kuipa matumaini timu hiyo.

3. Airin Madalina

Ameifungia bao moja Yanga kwenye mechi dhidi ya Fountain Gate na alisajiliwa akitokea Bunyore Starlets ya Ligi Kuu ya wanawake ya Kenya.

Madalina alikuwa mfungaji bora msimu uliopita Kenya akiifungia Bunyore mabao 18 na sasa ametua Yanga kuonyesha moto wake na kuongeza idadi ya nyota wa kike wa Kenya kwenye ligi hii inayokuwa kwa kasi.

BUNDA QUEENS

Bunda ndio msimu wao wa kwanza kushiriki Ligi Kuu nchini wakipana daraja na hawakuanza msimu vyema wakipokea vichapo.

Dirisha dogo lililofungwa Januari 15 liliwasajili wakenya watano, Saumu Baya, Liz Khisa ambaye tayari amefunga bao moja, Fanis Kwamboka, Eunice Kwangu na Lorine Awuor. Uwepo wa wakenya hao umewaongezea ushindani kwenye kikosi hicho ambacho kiko nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi kikiendelea kujitafuta kuhimili mikikimikiki ya ligi kuu.

FOUNTAIN GATES PRINCESS

Monicah Sedah na Inviolata Mukosh

Licha ya kusajiliwa msimu huu, Monicah amekuwa mmoja wa makipa tegemeo kwenye kikosi hicho huku Mukosh akiwa hapati nafasi ya kutosha kikosini.

Nyota hao ni miongoni mwa wanaokipiga timu ya taifa ya Harambee Starlets na wako nchini kama wenzao kuonyesha viwango vyao ikiwamo kusaka ugali kutokana na kukua kwa ligi kuu ya wanawake.

WASIKIE WENYEWE

Mwanaspoti limeshuhudia kundi kubwa la Wakenya wakiingia nchini kupiga soka na wenyewe wanasema ni kutokana na kukua kwa soka nchini na kipato kizuri na ni tofauti na Kenya kwani ni ngumu kupata mafanikio kiuychumi.

“Nipo kwa sababu za kifedha na kupata fursa ya kuonyesha talanta yangu, Ligi ya Tanzania inajulikana kwa aina yake ya uchezaji, ambayo ni tofauti na ligi ya nyumbani, Lengo langu ni kuandika historia hapa,” anasema Bundi aliyesaini mkataba wa miaka miwili na Yanga.

Baada ya kurejea Simba Shikangwa anasema “Simba sasa ni nyumbani. Nilikaribishwa kwa moyo mkunjufu, Uwepo wa Wakenya wenzangu umerahisisha mambo na pamoja na wachezaji wenzangu, tutaisaidia timu kupata matokeo mazuri, Klabu iliweka ofa nzuri mezani na kwa kuzingatia asili ya taaluma yangu na hitaji la kifedha, nilikubali.”

Wambui anasema “Tulitoka nyumbani kwenda kutafuta riziki, soka la Kenya hailipi kabisa, Sisi tuko kazini na tunajijengea jina, hapa Tanzania wachezaji wanalipwa posho za mechi na mishahara kwa wakati,” anasema Wambui.

Chanzo: Mwanaspoti