Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakenya wamechungulia fursa Azam Media, sisi je?

Azam Media XFKF Wakenya wamechungulia fursa Azam Media, sisi je?

Tue, 5 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wiki hii Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) lilisaini mkataba wa urushaji matangazo ya moja kwa moja ya mechi za Ligi Kuu ya nchi hiyo na kampuni ya Azam Media.

Mkataba huo ni wa miaka saba na utashuhudia Azam Media ikitoa Sh22.7bilioni ambazo sehemu kubwa itaenda kwa klabu zinazoshiriki ligi hiyo, ambayo inaonekana kupoteza msisimko kutokana na mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa fedha za kutosha na migongano ya kisiasa iliyosababisha Kenya ifungiwe na Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa).

Hiyo inamaanisha kuwa kwa mwaka, Azam Media itakuwa ikitoa takriban Sh2.3bilioni na kutakuwa na ongezeko la dola 100,000 kila mwaka.

Habari za mkataba huo kusainiwa zimepokewa kwa shangwe na klabu za nchi hiyo, ambazo zimeeleza kuwa donge hilo nono kutoka kampuni inayozidi kukua katika ukanda wa Afrika Mashariki, litazisaidia katika kuboresha uendeshaji wao.

Ni mkataba ambao umekuja zaidi ya miaka kumi baada ya Azam Media kuanzishwa na baada ya kampuni hiyo kuingia mkataba na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya kuonyesha mechi za Ligi Kuu. Kisheria, chama cha soka cha nchi ndicho chenye haki za matangazo ya moja kwa moja ya mechi za mchezo huo.

Klabu zinaweza kuwa zinafurahia ahueni inayotokana na mkataba huo, lakini mchezo wa soka ndio unaweza kunufaika zaidi iwapo mipango ya viongozi wa FKF itatekelezwa kama rais wake, Nick Mwenda alivyoeleza wakati wa hafla ya kusaini mkataba huo.

Kwanza, kwa kuanzia, Azam Media haitaonyesha mechi zote za Ligi Kuu ya Kenya, hivyo FKF imetumia fursa hiyo kutafuta mshirika mwingine wa kushirikiana na Azam Media kwa mechi ambazo hazitateuliwa na kampuni hiyo.

Yaani kwa kawaida kampuni inayoonyesha mechi za moja kwa moja kwa malipo (pay per view), itakuwa na haki ya kuamua ionyeshe mechi zipi kwa kuwa mkataba wake ni wa haki peke (exclusive rights). Kwa hiyo zile zilizobaki, FKF inaendelea na kampuni ya habari inayorusha matangazo yake bila malipo (free to air) ili ionyeshe mechi zitakazobaki kwa makubaliano na shirikisho hilo.

Hapa ni kwamba FKF haikupokea mkataba wa haki za matangazo kama zawadi, bali imekwenda mbele zaidi kuangalia mashabiki watakaoshindwa kumudu kununua ving’amuzi au ambao watashindwa kwenda kwenye vijiwe vinavyoonyesha ligi hiyo, watawezaje kuona mechi bila matatizo.

Kwa mujibu wa Mwendwa, hiyo ni kawaida duniani kote na ndio maana huwa tunaona baadhi ya mechi za fainali za Kombe la Dunia bila kupitia kampuni zilizonunua haki peke za ukanda fulani.

Mbali na mkakati huo, FKF imepewa chaneli maalum kwa ajili ya soka la Kenya, na si kwa ajili ya Ligi Kuu pekee. Na hapo mwenda alieleza vizuri jinsi wanavyojipanga kutumia fursa hiyo.

“Sisi tutakuwa na dedicated channel (chaneli maalum kwa ajili yetu). Wamenihakikishia. Hiyo chaneli hautaona kitu kingine; ni football ya Kenya peke yake,” alisema Mwendwa katika hafla hiyo.

“It also mean (pia inamaanisha) si mechi peke yake. Tutaenda kutengeneza content (maudhui) ya wachezaji, na makocha, na football yetu na grassroot na nini na equipments (vifaa) wanaleta na that is what we wanted when we started this negotiations (na hicho ndicho tulichotaka wakati tukianza mazungumzo haya).”

Hiyo ni kauli muhimu kutoka kwa kiongozi mkuu wa soka nchini Kenya. Na kauli hiyo inanikumbusha jinsi kulivyokuwa na matatizo wakati Azam Media wanaingia mkataba na TFF. Kuna klabu ilikuwa inatia ngumu bila ya kujua fursa zilizomo ndani ya mkataba hadi ikaelezwa jinsi inavyoweza kuzitumia, lakini hadi leo inasuasua.

Hata sisi wenyewe kama TFF hatukuona fursa ambazo Mwendwa amezieleza katika hotuba yake.

Muda ambao TFF na baadhi ya klabu zimepewa kwa ajili ya maudhui yao, hautumiki kikamilifu na pengine unatumika pale pande hizo zinapojisikia.

Kukumbuka soka la Kenya kwa ujumla kunamaanisha FKF itaweka mbele kutangaza program zake za maendeleo kama Mwendwa alivyotaja kuwa ni pamoja na soka la watoto (grassroot football) ambalo ndio nguzo ya nchi yoyote ile inayotaka kupiga hatua katika maendeleo ya soka. Kwa mujibu wa Fifa, hakuna taifa ambalo limetwaa Kombe la Dunia bila ya kuwa na soka la watoto.

Kwa kufanya hivyo, FKF itakuwa ikiwaambia washirika wake kuwa kuna sehemu nyingine za kuwekeza kwa kuwa hupata muda katika matangazo ya televisheni na hivyo kujiongezea fedha zaidi kwa ajili ya kuendeshea programu za watoto na vijana ambazo kwa kawaida ni ngumu kupata uwekezaji.

FKF itakuwa ikiwaambia washirika wake kuhusu mipango mbalimbali kama ya timu za taifa, mafunzo kwa makocha, waamuzi, watawala, madaktari na wengine.

Mkataba huo ni mdogo kulinganisha na ule ambao Azam Media imeingia na TFF. Lakini kitu kizuri ni kwamba Mwendwa ametambua hilo. Kutambua udhaifu ni kupiga hatua mbele na Mwendwa amesema pamoja na ukweli kwamba soka lao limepoa na watu hawaendi viwanjani, baada ya miaka mitatu Tanzania ndio itauliza kinachoendelea Kenya badala ya kipindi hiki ambacho Tanzania inaonekana kama mfano.

Na Mwendwa ametoa onyo kwamba miaka mitatu ya mwanzo itakuwa mikubwa katika kukubali mtazamo wa watu kuhusu maendeleo ya soka Kenya.

Nami nasema hatusubiri miaka hiyo mitatu ndio tuanze kuuliza nini kimetokea Kenya hadi wanatuzidi. Kwangu, kwa fikra hizo za Mwendwa na wenzake, tayari FKF wametuacha mbali kimipango. Baada ya zaidi ya miaka kumi, Tanzania bado hatujaziona fursa ambazo Mwendwa na wenzake wameziona. Tuna programu nyingi nzuri, lakini hatujui tunazitangazaje.

Kwetu Yanga na Simba wakifanya jambo likajaza uwanja, tunashangilia kwa nguvu kwamba tumepiga hatua, kumbe Mtibwa Sugar hawezi kujaza nusu ya uwanja anapocheza na Kagera Sugar.

Tunahitaji akili hiyo ya Mwendwa katika shirikisho letu na klabu zetu. Na akili hiyo haitoki kwa rais wa TFF pekee, bali wote wanaomzunguka kama wafanyakazi na marafiki ili mchezo wetu utoke kule ulikokuwa miaka kumi iliyopita.

Wakenya wameziona fursa ambazo tulitakiwa tuzione miaka mingi iliyopita.

Chanzo: Mwanaspoti