Ishu kubwa uwanjani kwa timu zote ni kusaka ushindi na hauwezi kupatikana mpaka kuwe na wale wakali wa kucheka na nyavu ili waweze kuipa ushindi timu husika.
Katika Ligi Kuu England huko Ulaya nyota ya Mohamed Salah mwarabu wa Misri inazidi kuwaka sawa na ile ya mshikaji wake Sadio Mane huyu ni Msenegal hivyo ikiwa wataendelea kuwa katika ubora huo wataandika rekodi nyingi na tamu.
Leo tunatazama namna wakali wa kutupia wanavyokiwasha ila kwa wale ambao wamefunga mabao kuanzia manne pamoja na pasi zao namna ilivyokuwa.
Na namba moja ipo kwa Salah nyota anayekipiga ndani ya Liverpool inayonolewa na Jurgen Klopp ni namba moja kwa timu yake hiyo akiwa ametupia mabao sita kibindoni na amecheza mechi 7.
Raia huyo wa Misri ana wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 105 na amepiga jumla ya mashuti 22 ni moja ya washambuliaji wenye ushkaji mkubwa na kucheka nyavu.
Mbali na kufunga pia anauwezo wa kutengeneza pasi za mwisho ambapo anazo tatu mpaka sasa hivyo amehusika katika mabao 10 kati ya 17 ambayo yamefungwa na timu hiyo iliyo nafasi ya pili kwenye msimamo na pointi 15.
Mwingine ni Jamie Vardy huyu ni kinara ndani ya Klabu ya Leicester City akiwa ametupia mabao 6 na ana pasi moja ya bao hivyo amehusika katika mabao 7 kati ya 9 ambayo yamefungwa na timu hiyo iliyo nafasi ya 13 na pointi zake ni 8.
Amecheza jumla ya mechi 7 na ana wastani wa kufunga bao kila baada ya dakika 104 akiwa amepiga jumla ya mashuti 17 ndani ya Ligi Kuu England.
Yupo Michael Antonio huyu yupo zake ndani ya West Ham United iliyo nafasi ya 9 na pointi zake ni 11, mwamba huyu amehusika katika mabao nane kati ya 14 ,ametupia mabao matano na pasi tatu za mabao akiwa na wastani wa kufunga bao kila baada ya dakika 107 na amepiga mashuti 18.
Ukienda ndani ya Manchester United utamkuta Bruno Fernandes yeye amehusika katika mabao matano akiwa ametupia mabao manne na pasi moja ya bao kati mabao 14 ambayo yamefungwa na timu hiyo iliyo nafasi ya nne kwenye msimamo na pointi zake ni 14.
Ana wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 156 akiwa amecheza jumla ya mechi 7 na amepiga jumla ya mashuti 16.
Neal Maupay ni mali ya Brighton akiwa ametupia mabao manne katika mechi saba hajatengeneza pasi akiwa na wastani wa kufunga kila baada ya dakika 146 na mashuti aliyopiga ni 13.
Msenegal Sadio Mane wa Liverpool naye ametupia mabao manne akiwa hajatoa pasi na ana wastani wa kucheka na nyavu kila baada ya dakika 158 na ni mashuti 15 amepiga.
Mwingine mwenye mabao manne ni Ismaila Sarr huyu ni wa pale Watford ana wastani wakutupia kila baada ya dakika 158 na ni mashuti 16 amepiga.