Baada ya kuibadilisha Coastal Union kwa kiasi kikubwa namna ya uchezaji kocha wa timu hiyo Mkenya David Ouma amefunguka kuwa kwake anahusudu sana mpira wa chini na siyo butua butua.
Ouma alirithi mikoba ya Mwinyi Zahera ambaye alifungashiwa virago Novemba 10,2023 mpaka amefanya kazi kubwa ya kubadilisha kikosi kwenye uchezaji hali ambayo inaifanya Coastal kuwa miongoni mwa timu ambazo zinacheza soka safi kwa sasa.
Katika mechi saba za Ligi ambazo ameiongoza timu hiyo imepata ushindi mechi tano huku ikipoteza moja sawa na sare ambayo imetoka ambapo chini yake Magushi imekufanya alama 16 na kuifanya kushika nafasi ya nne kwenye msimamo kwa alama 23.
Mechi hizo ni dhidi ya Geita Gold FC (3-1), Kagera Sugar (1-0), Dodoma Jiji (1-0) zote nyumbani lakini Tanzania Prisons (0-1), JKT Tanzania (0-1), Singida Fountain Gate (1-0) na KM C (0-0) ugenini.
Ouma alisema falsafa yake ni kuweka mpira chini na wala yeye siyo muumini wa mipira ya juu (butua butua) ndio maana katika mechi ambazo ameiongoza Coastal timu hiyo inacheza vyema.
Alisema ili timu ipate matokeo ni lazima kucheza kwa kuelewana kwa maana ya kila mmoja kupiga pasi zenye usahii na siyo kupiga piga ilimradi mpira utoke kwako lakini kwa kuweka mpira chini jambo ambalo kwake anaona amefauli kwa kiasi chake.
“Kwangu nataka mpira wa chini ndio inakuwezesha kupata matokeo na sasa naona wachezaji wangu ilo wamelifanyia kazi ndio maana timu inapiga soka safi,” alisema Ouma.
Aliongeza kwa kusema, silaha kubwa kwa upande wao hadi sasa ni uharaka wa wachezaji wake kuanzia idara ya ulinzi,viungo na ushambualiaji kila mtu kwa nafasi yake kufuta na kufanyia kazi nafasi wanazotengeneza.
Ametumia fursa hiyo kuweka wazi kikosi chake kiko vyema kwa ajili ya mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Mbeya Kwanza ambayo itapigwa leo Jumatatu kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga.