Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wagombea TFF watua Tanga na mikakati mizito

Tanga Pic Data Rais wa TFF, Wallace Karia

Fri, 6 Aug 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Tangu jana wagombea kwenye uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania  (TFF) wameanza kuwasili mjini Tanga na wengine wakiwasili leo tayari kwa uchaguzi hapo kesho Jumamosi huku kila mmoja akiwa na mikakati kabambe endapo atapewa ridhaa na wapiga kura.

Uchaguzi huo utaanza saa 2 Asubuhi kwenye hoteli ya Tanga Beach Resort huku mchuano ukisalia kwa wagombea wa nafasi za ujumbe kutoka kanda sita.

Kanda hizo ni ile namba moja ya mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Morogoro na Pwani, kanda namba mbili ina mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga, kanda namba tatu ni mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe, Ruvuma na Songwe.

Kanda namba nne ina mikoa ya Dodoma, Shinyanga, Simiyu na Singida na kanda namba tano ina mikoa ya Geita, Mara, Mwanza na Kagera huku kanda namba sita ikiunganisha mikoa ya Katavi, Kigoma, Rukwa na Tabora.

Ikiwa ni siku ya mwisho ya kampeni kwa wagombea kwenye uchaguzi huo, baadhi yao wameeleza mikakati waliyonayo katika kumshauri rais wa TFF endapo watapewa riadhaa.

Bukuku anayeiwakilisha kanda namba mbili amesema atakapopewa ridhaa atamshauri rais juu ya ustawishaji wa mikoa,vyama shiriki  na klabu na kuimarisha mfumo wa soka la vijana na kuendelea kumshauri rais namna bora ya uendeshaji TFF.

Hamisi Kitila yeye ana mkakati wa ufadhili wa Ligi daraja lla kwanza, soka la vijana na mkakati wa kuwajengea uwezo viongozi wa mikoa na wilaya.

Salum Umande Chama katika kampeni zake za mwisho mjini hapa amesema atamshauri rais katika

kuongeza na kuboresha sekta ya waamuzi na makocha.

Osuri Kosuri ambaye pia ni mjumbe kamati tendaji, makamu mwenyekiti wa kamati ya habari na masoko TFF, mwenyekiti wa chama cha soka Simiyu, Matchcomissner wa ligi  na kocha mwenye leseni B ya CAF amesema ataendelea kumshauri rais wa TFF kulifanya Shirikisho hilo liendelee kufanya kazi kwa ufanisi na kuunganisha mikoa yote kwenye kanda anayotoka.

Salum Alli Kulunge ambaye pia ni mwenyekiti chama cha mpira wa miguu Geita anasema moja ya mikakati yake kama atapewa ridhaa ni kumshauri rais ili mikoa iweze kupata ruzuku za kila mwaka kwa ajili ya maendeleo ya mpira Mikoani toka kwenye Shirikisho.

CPA Hosseah Lugano anayetokea kanda namba moja anasema, amejitosa kuwania nafasi ya ujumbe wa TFF ili kuongeza ubunifu, kuhoji, kushauri katika usimamizi na utendaji.

 Leo saa 12:00 jioni wagombea watahitimisha kampeni zilizofanyika kwa siku sita  huku wale waliowasili mjini hapa wakifanya kampeni za mwisho mwisho kwa baadhi ya wapiga kura ambao tayari wamewasili.

Makamu mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, Benjamin Karume amesema wako katika hatua za mwisho kukamilisha mchakato  huo ulioanza miezi miwili iliyopita na baadhi ya wagombea kuenguliwa katika mchujo wa awali na kwenye usaili wakiwamo watano wa nafasi ya urais.

Uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Mpira wa miguu Tanzania(TFF) unatarajiwa kufanyika kesho Agosti 7 Jijini Tanga,huku nafasi ya Mgombea Urais ikigombewa na Wallace Karia pekee baada ya wengine kuondolewa kwa kutotimiza masharti.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz