Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wageni wawapania vigogo SWPL

Wanawake Pic Wageni wawapania vigogo SWPL

Fri, 30 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara (SWPL), imekamilika kwa JKT Queens kutwaa ubingwa ikiivua taji Simba Queens iliyokuwa inaushikilia kwa misimu mitatu mfululizo.

JKT Queens ndio watetezi wa michuano ya Cecafa ambayo msimu huu itafanyika Uganda na maafande hao watashiriki michuano kwa msimu huu kusaka tiketi ya Klabu Bingwa ya Afrika, Michuano hiyo itafanyika kati ya Agosti 12 hadi 26.

Timu za Bunda Queens na Geita Gold Queens zimepanda daraja msimu huu baada ya kufanya vizuri katika Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2022/2023, zimepania kufanya vizuri katika msimu wake wa kwanza wa 2023/2024.

Ligi Daraja la Kwanza ilikuwa inashirikisha timu 14 zilizogawanywa katika makundi manne, kila kundi lilitoa timu moja ambapo zikakutana hatua ya robo fainali hadi fainali.

Timu zilizokuwa zinashiriki ligi hiyo ni Bunda Queens, Geita Gold, Bilo FC, TSC Queens, Ukerewe Queens, Singida Warriaors, Mt.Hanang Queens, Lengo Queens, Mlandizi Queens, JMK Park Queens, Masala Queens, Oysterbay Queens, Ruangwa Queens na Mapinduzi Queens.

BUNDA QUEENS

Bunda Queens imepanda ligi hiyo ikiwa ni miezi michache tu tangu ilipotwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) mwaka jana, jijini Mwanza.

Mwenyekiti wa timu hiyo, Stephano Kasondi, anasema wamejipanga vizuri kukabiliana na timu kongwe za Ligi Kuu kama Simba Queens, JKT Queens, Yanga Princess na zingine.

“Tumejipanga vizuri tunaendelea kuboresha kikosi kulingana na mahitaji ya mwalimu, hivyo naamini tutakuwa na timu bora ya ushindani kwa msimu huo ujao.

Anasema pamoja na kuwepo na timu kongwe katika Ligi Kuu hawatakata tamaa zaidi wataongeza juhudi kuhakikisha wanakabiliana nao.

Anasema wanaamini wanaweza kuhimili mikikimikiki ya Ligi Kuu na hakuna kitu kipya zaidi ya kuongeza umakini na juhudi.

“Uwezo tunao maana kila kitu ni maandalizi na sisi tunaendelea kujiandaa kwa kucheza michezo mingi ya kirafiki na kutafuta wadhamini kuweza kutusaidia katika mahitaji mbalimbali.

“Hivi sasa tunaweza kumudu usafiri tu, lakini sehemu zingine bado tunaendelea na mazungumzo na wadau mbalimbali kuhakikisha tunaweza kumudu gharama zote, Kocha wa Bunda Queens, Alley Ibrahim, anasema mafanikio hayo ni matunda ya uwekezaji walioufanya wa miaka minne ambapo, walikaa na kikosi chao kwa muda wote huo na kutengeneza muunganiko na timu imara ambayo imetwaa makombe ya RCL na WFDL.

"Tulijipanga na tulikuja kwa malengo mawili kupanda daraja na kutwaa ubingwa, tunamshukuru Mungu tumefanikisha yote, nawapongeza wachezaji wangu na kila mmoja aliyetuunga mkono hivi sasa tunajipanga kwa msimu ujao Ligi Kuu," anasema Ibrahim.

GEITA GOLD QUEENS

Kocha wa timu ya Geita Gold Queens, Frank Aloys, anasema wamejipanga vizuri kukabiliana na timu kongwe ambazo zinashiriki ligi hiyo kwa kuanza na kusajili wachezaji wapya 12.

“Wachezaji wetu wapya wana uzoefu mkubwa wa mashindano haya, tunatambua kuwa michuano hii ni migumu lakini tumejipanga vya kutosha.

“Iwe jua iwe mvua,lazima tukabiliane na timu hizi kongwe licha ya kuwa, timu yetu bado changa katika michuano hii,”anasema.

Kocha huyo anasema hadi kufikia Juni mwaka huu, wanategemea kupata wadhamini ambao watasaidia timu hiyo kujimudu katika mahitaji yote.

Mbali na hayo, Kocha huyo anasema wanajipanga kutoa ushindi na wala siyo kushiriki hivyo, mashabiki wa timu hiyo wasubirie matunda mazuri.

Kocha wa makipa wa timu hiyo, Mussa Haule anasema wanaendelea na maandalizi kuweza kupambana na baadhi ya changamoto zitakazo kuwepo katika Ligi Kuu.

Anasema wachezaji hivi sasa wanaendelea na mazoezi ambayo yatasaidia kuleta matokeo mazuri ya timu hiyo.

Chanzo: Mwanaspoti