Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wageni wabeba lawama Kariakoo Derby

Che Malone Gift Wageni wabeba lawama Kariakoo Derby

Tue, 31 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Historia ya ubabe wa wachezaji wa kigeni katika kufumania nyavu katika mechi ya watani wa jadi , Simba na Yanga 'Kariakoo Derby', inaonekana kuwa katika nafasi kubwa ya kuendelea wakati timu hizo zitakapokutana katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu, Novemba 5 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika miaka ya hivi karibuni, wachezaji wa kigeni ndio wameonekana kuwa moto wa kuotea mbali katika ufungaji wa mabao kwenye mechi baina ya timu hizo huku wazawa wakipachika mabao kiduchu.

Ingawa michezo ya watani wa jadi mara nyingi imekuwa na matokeo ya kushangaza na huwa vigumu kutabirika, ifuatayo ni tathmini ya sababu zinazofanya wachezaji wa kigeni kuendelea kubeba imani ya kutanba katika mchezo huo kwa kufunga mabao yanayoweza kuuamua.

Takwimu za mechi 20

Katika miaka sita ya hivi karibuni, Simba na Yanga zimekutana mara 20 katika mashindano tofauti ambapo katika michezo hiyo, timu hizo zimefunga idadi ya mabao 30 kwa pamoja.

Wagemi ndio wameonekana kufumania nyavu mara nyingi zaidi katika mechi hizo 20 za watani wa jadi ambapo kati ya mabao yote 30, wenyewe wamefumania nyavu mara 20 na mabao 10 tu yakipachikwa na wazawa.

Kati ya mechi hizo 20, mechi 13 ni za Ligi Kuu ambazo zilishuhudiwa idadi ya mabao 19 yakifungwa ambapo kati ya mabao hayo, mabao 12 yalipachikwa na wachezaji wa kigeni na wazawa wenyewe walifunga mabao saba.

Katika Kombe la Shirikisho la Azam, timu hizo zimekutana mara tatu ambapo yalifungwa mabao saba na kati ya hayo, mabao matatu yalifungwa na wazawa huku wageni wakipachika mabao manne.

Yanga na Simba zimekutana mara tatu katika mechi ya Ngao ya Jamii katika miaka ya hivi karibuni na wakafunga mabao manne ambayo yote yalipachikwa na nyota wa kigeni.

Wazawa ambao wamefunga mabao 10 kwenye mechi 20 zilizopita za Simba na Yanga ni Mapinduzi Balama, Shiza Kichuya, Zawadi Mauya, Mohammed Hussein, Kibu Denis, Erasto Nyoni, Mzamiru Yassin na Feisal Salum.

Wageni waliopachika mabao 20 ya kwenye mechi hizo za watani wa jadi ni Clatous Chama, Medie Kagere, Aziz Ki Stephane, Deo Kanda, Enock Inonga, Joash Onyango, Michael Sarpong, Gerson Fraga, Luis Miquissone, Augustine Okrah, Laudit Mavugo, Tambwe Hamis, Fiston Mayele na Bernard Morrison.

Kiwango bora kwa sasa

Ukiondoa historia, makali ya kufumania nyavu katika mechi za Ligi Kuu msimu huu ambayo wageni wameendelea kuonyesha, yanazidi kuongeza imani kwamba wana nafasi kubwa ya kuibeba mechi ya Kariakoo Derby Jumapili ijayo.

Yanga katika raundi saba ilizocheza kwenye Ligi Kuu msimu huu, tayati imeshapachika mabao 20 ambayo asilimia kubwa yamewekwa kimiani na wageni.

Katika mabao hayo 20 ya Yanga msimu huu, mabao 17 sawa na 85% yamefungwa na wachezaji wa kigeni ambao ni Aziz Ki, Kennedy Musonda, Pacome Zouzoua, Yao Atohoula, Maxi Nzengeli na Hafidh Konkoni wakati mabao matatu ambayo ni sawa na asilimia 15 yamefungwa na wazawa, Dickson Job na Mudathir Yahaya.

Kwa upande wa Simba, nao wameendelea kwa kiasi kikubwa kutegemea mchango wa wageni katika kupatia mabao yao katika mechi sita walizocheza kwenye Ligi Kuu hadi sasa.

Simba imefunga mabao 16 ambapo kati ya hayo, mabao 15 sawa na 93.75% yamefungwa na wageni na bao moja tu limepachikwa na mzawa.

Wageni walioifungia Simba mabao 15 kwenye Ligi Kuu ni , Saido NtibazonkizaChama, Jean Baleke, Willy Onana, Moses Phiri na Fabrice Ngoma wakati mzawa aliyefunga ni John Bocco.

Uhakika wa namba

Nyota wa kigeni wamekuwa tegemeo kubwa la timu hizo mbili kongwe nchini katika siku za hivi karibuni kulinganisha na wazawa jambo ambalo limechangia wawe wanapata nafasi mara kwa mara katika vikosi vyao kulinganisha na wazawa.

Katika kikosi cha kwa kwanza Simba, wageni wasiopungua sita wamekuwa na uhakika wa kuanza kama ilivyo katika kikosi cha Yanga.

Wasikie wadau Mshambuliaji wa zamani Simba, Bakari Kigodeko alikiri wageni kuwa na wakati mzuri kwa sasa lakini hilo haliwezi kuwafanya waweze kuamua mechi ya watani wa jadi moja kwa moja.

"Wageni wanafanya vizuri kwa sasa ni kweli lakini hilo haliwezi kufanya tuwape moja kwa moja uhakika wa kuamua mechi kama hii;

"Dabi mara nyingi inakuja kwa taswira tofauti, hauwezi kuamua kwa pafomansi ya timu wakati husika bali ni matokeo ya ndani ya uwanja siku husika."

Mshambuliaji wa zamani Yanga, Mohamed Hussein 'Mmachinga', alisema wageni wanakuwa wanatawala sana kutokana na kujitoa zaidi kwenye mechi kubwa kama hizi ili kujihakikishia wanapata namba za kudumu kwenye kikosi.

"Mechi hizi kila mmoja huwa anatafuta namba ya kudumu, wachezaji wazawa mara nyingi huwa na kawaida ya kulizika na ndio changamoto huwa inaanzia hapo,"alisema Mmachinga.

Kauli hiyo iliungwa mkono na mshambuliaji wa zamani Yanga, Herry Morris ambaye alisema wachezaji wazawa hawapendi kujifunza kwa wenzao waliotangulia.

"Wazawa mara nyingi wanapenda kulizika na hiyo ni changamoto kubwa waliyonayo, sisi tulikuwa tunajifunza zamani kwa waliotutangulia," alisema Morris.

Chanzo: Mwanaspoti