Tangu mwaka huo wa kwanza ambapo timu ya Sunderland kwa sasa Simba ilipoweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutwaa ubingwa ulioshirikisha timu zote Tanzania, kuna baadhi ya wachezaji wameweka rekodi mbalimbali, ikiwamo kuwa wafungaji bora wa msimu.
Hata hivyo, kuna baadhi ya wachezaji wameweka rekodi za aina yake ya kufunga mabao mengi kwa msimu mmoja wa ligi, huku wakitwaa Kiatu cha Dhahabu.
Kwa miaka ya hivi karibuni kuna baadhi ya wachezaji wamekuwa wakionekana kutishia kuivuka rekodi ya kufunga mabao mengi, ingawa imekuwa ngumu kidogo.
Kwenye makala haya, mwandishi amekusanya rekodi za wachezaji waliowahi kuwa wafungaji wa wakati wote kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa idadi kubwa ya mabao yanayoingia kwenye rekodi ya soka la Bongo.
1. Mohamed Hussein 'Mmachinga' - Yanga (mabao 26) Huyu ndiye mfungaji bora wa muda wote kwenye soka la Tanzania tangu Ligi Kuu ianze mwaka 1965 kwa kufunga mabao mengi zaidi kuliko mtu mwingine yeyote.
Mohamed Hussein maarufu kama 'Mmachinga' ni Mtanzania ambaye rekodi yake inaendelea kuwapo hadi leo, ikiwashinda hata wachezaji wengi wa kigeni ambao wakati mwingine wamekuwa wakikaribia zaidi kuifikia.
Aliiweka mwaka 1997, akifunga mabao 26, akiifanya timu yake ya Yanga kutwaa ubingwa kwa pointi 44, ikiipiku Simba iliyomaliza ikiwa na pointi 38, akiwa mfungaji bora msimu huo.
Kwenye ligi hiyo, Yanga ilifunga mabao 30, ikiwa na maana kuwa ni manne tu ambayo yalifungwa na wachezaji wengine msimu mzima, kukiwa na timu 12 tu, Reli na Sigara zikishuka daraja.
2. Abdallah Juma - Mtibwa Sugar (mabao 25) Almanusura straika Abdallah Juma aifikie rekodi hiyo mwaka 2005, alipopachika mabao 25, likiwa limebaki bao moja tu aikute rekodi ya Mmachinga.
Pamoja na kufunga idadi hiyo ya mabao na kuwa mfungaji bora msimu huo, timu yake ya Mtibwa Sugar iliishia kushika nafasi ya saba kwenye msimamo, Yanga ikitwaa ubingwa, Moro United ya pili na Simba ikawa ya tatu, huku Majimaji na Mji Mpwapwa zikireteremka daraja. Anashika nafasi ya pili kwa mabao mengi.
3. Meddie Kagere - Simba (mabao 23) Anakamata nafasi ya tatu kwa mfungaji wa wakati wote Ligi Kuu Bara kutokana na kupachika mabao 23, akiwa mfungaji bora msimu uliopita wa 2018/19. Meddie Kagere ambaye ni Mnyarwanda, aliisaidia timu yake ya Simba kutwaa ubingwa kwa pointi 93, ikifuatiwa na Yanga iliyomaliza na pointi 86, timu za Stand United na African Lyon zikishuka daraja.
4. Emmanuel Okwi - Simba (mabao 20) Mganda Emmanuel Okwi, alichukua Kiatu cha Dhahabu msimu wa 2017/18, akipachika mabao 20 kwa msimu akiingia kwenye orodha ya wafungaji bora waliopachika mabao mengi kwenye historia ya Ligi ya Tanzania akiwa wa nne. Ni msimu ambao aliipa Simba ubingwa kwa pointi 69, Majimaji na Njombe Mji zikishuka daraja.
5. John Bocco - Azam FC (mabao 19) Straika ambaye kwa sasa anaichezea Simba, John Bocco, alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu wa 2011/12, akipachika mabao 19, yeye anashika nafasi ya tano kwa wafungaji wenye mabao mengi kwenye historia ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Wakati huo akiichezea Azam FC, alifunga idadi hiyo ya mabao, lakini hayakuweza kufua dafu na kuifanya timu yake iwe bingwa, kwani iliishia kumaliza na pointi 56, Simba ikiwa bingwa kwa pointi sita zaidi, ikiwa nazo 62, huku timu za Villa Squad, Moro United na Polisi Dodoma zikishuka daraja.