Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadhamini wachukuliwe kama watetezi wa mpira wetu, wasikatishwe tamaa

Wadhamini Pic Data Viongozi wa Makampuni yanayodhamini vilabu vya Simba na Yanga

Tue, 9 Nov 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mjadala mkubwa ambao ulikaribia kuiteka wiki ni hoja ya ‘Fair Competition’ ikibeba maana ya usawa wa ushindani kati ya klabu moja dhidi ya nyingine.

Msingi wa mjadala huu ulikuwa kwamba wapo ambao waliona kuna ukakasi kwa kampuni za GSM kuzidhamini klabu tatu za Namungo, Yanga na Coastal Union ambazo zote zinashiriki ligi moja.

Niliufuatilia mjadala huu kwa kina nikijipa siku kadhaa kuangalia na kujiuliza GSM ni nani ndani ya hizo klabu tatu na kugundua kwamba anasimama kama mdhamini tu ndani ya klabu zote lakini ipo sura nyingine tofauti kidogo anapokuwa pale Yanga.

Anapokuwa Yanga mbali na kuwa mdhamini na watengenezaji wa jezi za Yanga (kit sponsor) lakini pia ameamua kuwa mwana familia akisaiidia kurudisha ushindani wa klabu hiyo baada ya hapa kati kuzorota na kupoteza makali.

Akiwa Coastal Union pale anaweka bidhaa zake kama mdhamini kwenye jezi yaani ‘kit sponsor’ kupitia bidhaa zake lakini pia akiwa Namungo hali inakuwa kama hivyo na tukumbuke sio mdhamini mkuu katika klabu zote hizo tatu.

Klabu nyingi zinazoshiriki ligi bado hazijafikia ubora wa kuwafanya wadhamini kuwafuata wenyewe na kutaka kuingia nao mikataba na kinachofanyika ni klabu zinaamua kuzifuata kampuni na kuomba udhamini kitu ambacho hakina ubaya.

Katika kusimamia ushindani wa usawa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kuna kitu ilizuia ambalo ni umiliki wa klabu zaidi ya moja kuwa chini ya mtu mmoja hasa katika mashindano yanayolingana.

Msingi mkubwa hapa waliondoa wasiwasi katika upangwaji wa matokeo lakini Fifa hawakuzuia udhamini wa kampuni moja kudhamini hata klabu zaidi ya moja kwa kuwa wanajua mpira unahitaji fedha.

GSM haimiliki klabu yoyote na kama ipo klabu ambayo imeamua kuingia ndani zaidi ni Yanga lakini haijafanya hivyo kwa Coastal Union wala Namungo wakiishia kuwa mdhamini pekee.

Coastal Union wanakula fedha za GSM tangu msimu uliopita na tukumbuke walipokutana na Yanga pale Mkwakwani Yanga alikiona cha moto akipokea kipigo tena mabosi wa GSM wakiwa jukwaani, nafikiri tukio hili linatosha kuonyesha kwamba wapi GSM wameishia katika klabu hizi.

Lakini kwa wale wanaoshikia bango wamesahau kuwa hata kampuni ya Mohamed Enterprises, iliyo chini ya bilionea wa Simba, Mohammed ‘Mo’ Dewji’ ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba kabla ya kujiuzulu hivi karibuni ina udhamini Simba na klabu ya Namungo, lakini hakuna aliyepiga kelele.

Si dhambi kwa kampuni moja kudhamini zaidi ya klabu moja katika ligi moja. Ni vitu vya kawaida sana, kwani hata Simba na Yanga zinadhaminiwa na SportPesa na awali kampuni hiyo hiyo iliidhamini pia Singida United ikiwa Ligi Kuu Bara.

Awali klabu hizo kongwe zilikuwa zikidhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager na hakukuwa na tatizo lolote ni sawa tu na sasa haki za televisheni za Azam Media zinahusu klabu zote kupitia Shirikisho la Soka (TFF), lakini huwezi kusikia kilele kuonyesha kuna kitu nyuma ya kelele hizo kwamba Azam wana timu Ligi Kuu kisha wanadhamini ligi hiyo na Kombe la Shirikisho linaloitwa Azam Sports Federation Cup.

Haipo tu Tanzania zipo klabu kubwa kama Arsenal, Real Madrid, PSG, AC Milan, Olympiacos na nyingine nyingi ambazo zinadhaminiwa na kampuni moja na bado zikashiriki mashindano hayohayo wakikutana katika ligi kubwa za Ulaya na hakuna wasiwasi wa upangwaji wa matokeo.

Mtu akifadhili au kudhamini timu zaidi ya moja hakuna madhara yoyote kiushindani au kupanga matokeo hilo litabaki kwa wasimamizi wa ligi ambao wanatakiwa kuhakikisha ushindani upo na mpaka sasa hakuna viashiria kama hivyo.

Kwa sasa ligi yetu inazidi kutanuka katika udhamini kwa klabu nyingi kupata udhamini lakini pia hata wasimamizi wa ligi nao wamekuwa wakihangaika kuhakikisha kampuni zinakuja kusaidia uendeshaji wa ligi.

Mjadala wa namna hii unaweza kupunguza nguvu ya wadhamini badala ya kuwapa nafasi tunapowaongezea wasiwasi. Zipo klabu zitakutana na nyakati ngumu kupata udhamini jambo ambalo tutazifanya baadhi ya timu kuwa na nguvu na zingine kuwa na nguvu hafifu kiu-shindani.

Nafi-kiri ipo haja ya kuwapongeza GSM na sio kujaribu kuwachafua na mijadala dhaifu kama hii ambayo inaweza kukoma kwa picha halisi tu ya maisha ya hizi timu katika kipi wanakipata kutoka kwa mdhamini wao.

Ligi yetu ni moja kati ya ligi bora Afrika Mashariki na Kati ambayo ubora huo umetokana na uwekezaji wa kampuni mbalimbali ambazo zimeamua kuingiza fedha zao katika klabu kitu ambacho kimeongeza ushindani, lakini zisitulevye na kuanza kujibomoa na kurudisha thamani ya soka nyuma.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz