Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadhamini Ligi Kuu hamasisheni uzalendo timu za nyumbani

Simba Vs Yanga Kibu DD.jpeg Wadhamini Ligi Kuu hamasisheni uzalendo timu za nyumbani

Wed, 21 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Matilda Buriani alimwaga chozi hadharani akililia uzalendo kwa watu wa mkoa wake kwa timu yao ya nyumbani, Tabora United.

Kwenye mchezo dhidi ya Simba, Februari 6, mwaka huu, wana Tabora waliisaliti timu yao na wote kuishangilia Simba.

Tabora ni mfano wa mikoa yote nchini ambayo ina timu kwenye Ligi Kuu Bara. Watu wao watazipenda hizo, lakini siku Simba au Yanga zikifika mkoa husika watu wanahama na kusaliti timu zao.

Watu wanakosa uzalendo kwa timu zao za nyumbani na kuvunja nyoyo za wale wanaojitolea kuhakikisha mikoa hiyo inakuwa na timu hadi kwenye Ligi Kuu.

Lakini chanzo cha tatizo hilo siyo tu mapenzi ya watu kwa timu kongwe za Dar es Salaam, hapana. Ni msukumo unaoendelea kwenye maisha ya soka kutoka kwa wadau mbalimbali. Tungetarajia kusaidia kuinua mapenzi ya watu kwa timu zao za nyumbani.

Vipindi vya michezo vya TV na redio, na hata magazetini habari zinazotawala kila siku ni za Yanga na Simba. Lakini katika wote hao, hakuna wanaopaswa kulaumiwa kama wadhamini wakuu, NBC. Wao kama wamiliki wakuu wa jina la ligi yetu wanapaswa kuinadi ligi kizalendo kama wanavyoinadi benki yao.

Sisemi kama hawafanyi kazi nzuri kwenye ligi, la hasha, ila kuna sehemu wameacha pamelegea. Kwa mfano, NBC wameweka picha za wachezaji wa Ligi Kuu kwenye ofisi zao za mikoa yote. Hii ni sehemu ya matangazo na ni mkakati mzuri, lakini picha hizo hazijazingatia uzalendo ninaouhubiri hapa.

Ukienda kwenye tawi la NBC Kigoma kwa mfano ambako kuna timu ya Mashujaa, picha utakazokuta ni za wachezaji wa timu za Yanga, Simba na Azam. Hakuna picha hata moja ya mchezaji wa Mashujaa. Ukienda Tabora ni vivyo hivyo, hakuna picha ya mchezaji wa Tabora United.

Na hii ni kwenye matawi yote. Hiyo siyo sawa. Ilipaswa NBC wazingatie kuhamasisha watu wa nyumbani kushangilia timu za nyumbani kwa kuwafanya wachezaji wao mashujaa. Najua kwamba wanajua umuhimu wa hizo picha kwenye matangazo, basi wazitumie kusaidia kukuza ushabiki wa timu za nyumbani kwa watu wa mikoani.

NBC pia itengeneze mkakati kwa kushirikiana na vyombo vya habari kuinua na kukuza mapenzi ya watu kwa timu za nyumbani.

Mpira wetu ambao unakwenda vizuri hadi sasa utapiga hatua kubwa endapo hamasa itakuwa kubwa kwa timu za nyumbani kila sehemu.

Ukienda Geita ukute uwanja umejaa watu wenye jezi za Geita Gold wakiishangilia timu yao hata kama inacheza dhidi ya Simba au Yanga. Hali iwe hivyo ukienda Kagera, Mbeya na kadhalika.

Ni katika hali kama hiyo ambapo udhamini kwenye timu za ligi huongezeka kwa sababu kampuni huwa na uhakika wa kundi kubwa la watu nyuma ya timu wanazozidhamini. Hii inaweza kuchukua muda kidogo hadi kufanikiwa, lakini cha msingi ni kwamba lazima ianze.

Na kama kuanza kwa maono ya macho ya nyama haiwezekani, basi mamlaka za soka ziweke kipengele kwenye mikataba ya udhamini kinachomtaka mdhamini kuhimiza uzalendo kwa timu za nyumbani.

Yanga na Simba zina mvuto wa zaidi ya asilimia 80 kwenye ligi, timu zilizobaki zinagawana asilimia 20 zilizobaki. Hali hii ni mbaya katika namna mbalimbali:

1. KIBIASHARA

Biashara yoyote hufuata watu na mvuto. Kwa kuwa watu na mvuto kwenye mpira wetu viko kwa Yanga na Simba, basi kila kitu kinaangukia huko.

Wadhamini wakubwa wanapigana vikumbo huko na hata kama kuna wadhamini wengine wanaenda sehemu nyingine, basi ni kwa dau dogo.

2. USHAWISHI

Mtaji wa watu na mvuto kwa timu hizo mbili kongwe husababisha ziwe na ushawishi katika maeneo mengi. Mamlaka za soka hufikia wakati huziogopa timu hizo kwa sababu zina makundi makubwa ya watu nyuma.

Hii husababisha hata kanuni kuvunjwa ili kuzifaidisha timu hizo. Kwa mfano msimu huu mechi ya Yanga na Azam FC ambayo ilitakiwa ifanyike Azam Complex, ilihamishwa ghafla na kupelekwa Uwanja wa Mkapa.

Huo ulikuwa uvunjifu wa wazi wa kanuni za ligi kwa sababu kikanuni mechi haipaswi kuhamishwa uwanja hadi ibainike kwamba uwanja husika una matatizo. Azam Complex haikuwa na tatizo lolote, ila tu Yanga hawakutaka kuchezea pale mechi hiyo.

3. KIBURI

Kwa kuwa zinafahamu kwamba zina watu wengi na mvuto mkubwa, timu za aina hiyo hujawa kiburi na kusababisha mivutano isiyo ya lazima na mamlaka.

Timu yao inafungwa uwanjani, wanataka kuanzisha maandamano hadi ikulu. Hii ni kwa sababu wanajua kwamba wana watu nyuma na wakiitisha maandamano yataitikiwa.

Jambo hilo na mambo mengine mengi husababisha kuchafuka kwa hali ya hewa pasi na sababu ya msingi.

HITIMISHO

Ni muhimu sana kuwekeza kwenye mikakati ya kuhakikisha timu za mikoani zinakuwa na ufuasi mkubwa ili kupunguza hali hiyo.

Hakuna kijiji kisicho na wazee, na hawa ndiyo wazee wetu hapa nchini, lakini haina maana kwamba vijana hawapaswi kuwa na miji na mamlaka ya ndani na familia zao. Wazee tuwaheshimu lakini vijana wapewe nafasi.

Chanzo: Mwanaspoti