Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadau wazipa mbinu Simba, Yanga Afrika

Yanga Rekodi Mpyaaaaa.jpeg Wadau wazipa mbinu Simba, Yanga Afrika

Sat, 16 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati mashabiki wa Simba na Yanga wakiwa Zambia na Rwanda kwa ajili ya michezo ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baadhi ya wadau wa soka nchini wamefunguka juu ya mambo yanayoweza kuwabeba wawakilishi hao katika michuano ya kimataifa.

Wadau hao wakiwemo wachezaji wa zamani wa timu hizo walifunguka majuzi kwenye mdahalo wa X Space unaoendeshwa na kampuni ya Mwananchi Communications (MCL) ikiwa zimesalia saa chache kabla ya Simba, Yanga na Singida BS kutupa karata za kwanza ya michuano hiyo.

Simba na Yanga ambao ni wanakipiga kwenye Ligi ya Mabingwa, leo wapo ugenini Mnyama akiwa Zambia kucheza na Power Dynamos, huku vijana wa Miguel Gamondi wakiwa Rwanda kucheza na Al-Merrikh ya Sudan kabla ya kesho Singida BS iliyopo Kombe la Shirikisho kuikaribisha Future ya Misri.

Kocha wa Makipa wa Ihefu, Peter Manyika alisema: ”Nimefanya kazi Afrika na nje hivyo kuna vitu nimeviona ambavyo vinaweza vikatusaidia, kipindi chetu tulikuwa tunapata michezo mikubwa kabla ya mashindano yenyewe kitu ambacho kilikuwa kinawafanya wachezaji kutengeneza ile hali ya kujiamini zaidi.”

Kipa wa zamani wa Yanga na Simba, Deogratius Munishi ‘Dida’ alisema ili timu zetu zifanye vizuri kimataifa inatakiwa Serikali kuzipa sapoti kubwa kwasababu ndiye ‘mama na baba’.

Kipa wa zamani wa Yanga, Benjamin Haule alisema: “Kuna haja ya kufanya usajili wa maana ili kupata wachezaji watakaoshindana kunyakua mataji ya kimataifa, kama zilivyo timu za Misri na kwingineko mfano mzuri Yanga imefanya vizuri mechi za kwanza iwe hivyo na kwa timu watakazokutana nazo mbele, vivyo hivyo Simba.”

Beki wa zamani wa Simba na Yanga, Amir Maftah alisema ili klabu zifanye vizuri, wachezaji wanatakiwa kuongeza umakini kuzingatia wanayoambiwa na makocha.

Mchezaji wa zamani wa Yanga, William Mtendamema alisema ili timu zifanye vizuri kimataifa zinahitaji usajili bora utakaozisaidia na sio kuleta wimbi kubwa la wachezaji kutoka nje.

Nyota wa zamani wa Simba na Yanga, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ anaamini kitakachozibeba kimataifa ni ubora wa wachezaji. “Timu zimepiga hatua kutokana na ubora wa wachezaji hususani wale wa kigeni hivyo ukichanganya na waliopo naamini tutafanya vizuri.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: