Zimesalia raundi tano tu kuhitimisha msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2023/14, huku timu zikiwa zimeshajipambanua zenyewe kwenye msimamo.
Kuna zinazoonekana kusaka ubingwa, lakini kupata nafasi mbili za juu ili kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao. Timu hizo ni Yanga, Simba na Azam FC ambazo moja wapo ndiyo itatwaa ubingwa, na mbili kati ya hizo zitacheza michuano hiyo ya kimataifa.
Zipo zinazowania nafasi ya nne, ili kujiwekea akiba ya kucheza Kombe la Shirikisho msimu ujao kutokana na kanuni zilivyo.
Timu itakayochukua ubingwa wa Kombe la FA, kama itakuwa ni moja kati ya timu tatu zitakazomaliza nafasi ya juu, basi itakayoshika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu, nayo itacheza Kombe la Shirikisho.
Coastal Union, KMC na Prisons zinaonekana kuinyemelea nafasi hiyo msimu huu.
Hali ni mbaya kwa timu za Mtibwa Sugar inayoshika mkia, Tabora United, Mashujaa FC, Geita Gold, Ihefu na Namungo, ambazo kama hazikufanya vema katika michezo yao iliyosalia, ama zinaweza kushuka daraja, au kwenda kucheza mechi za mchujo na timu kutoka Ligi ya Championship.
Ukiacha matokeo na rekodi za timu, wachezaji nao wanapambana kila mmoja kujitengenezea rekodi yake.
Katika makala haya, tumekusanya takwimu za baadhi ya wachezaji wanaoonekana 'kuupiga mwingi' mpaka sasa ambao wanaweza kujiwekea rekodi binafsi mwishoni mwa msimu...
1# Stephane Aziz Ki (mashuti ya mbali)
Kiungo mshambuliaji huyu wa Yanga, anaongoza kwa kufunga mabao kwa mashuti ya mbali. Mburkina Faso huyo amefunga mabao matano akiwa nje ya boksi mpaka sasa. Aziz Ki, ambaye ndiye kinara wa mabao kwenye Ligi Kuu akipachika 15 kabla ya mechi ya jana, ni mmoja wa wachezaji ambao ni hatari kwa kupiga mashuti ya mbali, akiwa anakokota mpira, au kwenye mikwaju ya faulo.
Wakati Aziz Ki, aliongoza kwa mabao ya mashuti ya mbali, kiungo mshambuliaji mwingine wa Ihefu FC, raia wa Togo, Marouf Tchakei, anafuatia akiwa na mabao matatu ambayo ameyapachika akiwa nje ya boksi.
2# Fei Toto (mkali ndani ya boksi)
Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto', yeye anaongoza kwa kufunga mabao ndani ya eneo la hatari. Feisal, maarufu kama Fei Toto, amefunga mabao 13 akiwa kwenye boksi.
Mchezaji huyo aliyesajiliwa msimu huu akitokea Yanga, ana mabao 14 ya kufunga mpaka sasa, akishika nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora, nyuma ya Aziz Ki, hivyo inaonyesha kuwa ni bao moja tu alilolifunga akiwa nje ya boksi.
Wanaoshika nafasi ya pili kwa kupachika mabao ndani ya boksi ni kiungo mshambuliaji raia wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki wa Yanga na straika wa KMC, Waziri Junior, ambao wote wamefunga mabao 10 wakiwa ndani ya eneo la hatari.
3# Mudathir (mfungaji bao la mapema)
Kiungo mkabaji wa Yanga, Mudathir Yahaya, ndiye mfungaji wa bao la mapema zaidi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara hadi kufikia raundi ya 25.
Bao alilofunga sekunde ya 48 dhidi ya KMC, Februari 17, mwaka huu, katika mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu linaendelea kuwa bao la mapema zaidi katika ligi mpaka sasa.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa CM Kirumba jijini Mwanza, Yanga ilishinda mabao 3-0, mchezaji huyo akifunga mabao mawili, moja likifungwa na Pacome Zouzoua.
Anayeshika nafasi ya pili kwa kupachika bao la mapema ni kiungo mkabaji wa Azam FC, Sospeter Bajana, ambaye alifunga dakika ya 54, katika mechi ambayo timu hiyo ilicheza dhidi ya JKT Tanzania.
4# Djigui Diarra (mbabe wa 'clean sheets')
Kipa wa Yanga, Djigui Diarra, anaongoza kwa kukaa langoni mechi nyingi bila kuruhusu wavu wake kuguswa. Raia huyo wa Mali, amefanya hivyo mara 11, akifuatiwa na kipa wa Coastal Union raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Ley Matampi, aliye na 'clean sheets' 10 mpaka sasa.
Mechi iliyoamua nani awe juu katika makipa hao wawili, ilikuwa ni ya Aprili 27, kati ya Yanga dhidi ya Coastal Union, iliyochezwa, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Kabla ya mechi hiyo, kila mmoja akiwa na 'clean sheets' 10, lakini dakika 90 zilimalizika kwa Yanga kushinda bao 1-0.
5# Kipre Junior (mkali wa 'asisti')
Winga wa Azam FC, Kipre Junior, yuko juu ya watoa pasi za mwisho kwenye Ligi Kuu, akiwa amefanya hivyo mara nane mpaka sasa.
Raia huyo wa Ivory Coast mwenye 'asisti' nane, anafuatiwa na raia mwenzake na huko, Yao Kouassi, anayeichezea Yanga, pamoja na Mburkina Faso wa Yanga, Aziz Ki, ambao wote wana 'asisti' saba kila mmoja, huku Fei Toto akiwa nazo sita.
Wachezaji Awesu Awesu na Rahim Shomari wa KMC, Paschal Msindo na Lusajo Mwaikenda wa Azam FC, Clement Mzize wa Yanga, Clatous Chama wa Simba, na Impiri Mbombo wa Tabora United, wote wakiwa na 'asisti' tano kila mmoja.