Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachezaji wampa tuzo Ibrahim Bacca

Bacca Ibrahim Yanga Wachezaji wampa tuzo Ibrahim Bacca

Wed, 24 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Beki wa Yanga, Ibarahim Abdullah 'Bacca' amepigiwa kura na baadhi ya wachezaji wa Ligi Kuu, kuona anastahili kunyakua tuzo ya beki bora kwa msimu huu wa 2023/24.

Mwanaspoti limezungumza na wachezaji hao kwa nyakati tofauti, mitazamo yao ni endapo zikiwepo tuzo za beki bora kwa msimu huu, wanaona Bacca anastahili kuipata kutokana na kazi aliyoifanya.

Nahodha wa Prisons, Benjamin Asukile amesema angekuwa katika nafasi ya kupiga kura kumchagua nani awe beki bora asingesita kulitaja jina la Bacca.

"Tangu msimu uanze, Bacca ameisaidia timu yake ligi ya ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika pia kwenye kikosi cha Taifa Stars, tumeona jinsi alivyokuwa anaimarisha ulinzi salama kwa timu," amesema.

Beki wa Mashujaa, Said Juma 'Makapu', amesema Bacca ameonyesha kiwango kizuri, hivyo ikiwepo tuzo ya nafasi hiyo, anaona anastahili kuipata. "Wapo mabeki wengi wazuri, naona upepo kwa sasa upo kwa Bacca, huenda mwakani ikawa kwa mwingine akaibuka na akafanya vizuri, ndio soka lilivyo," amesema Makapu ambaye amewahi kuichezea Yanga.

Aliyekuwa beki wa Azam FC, Aggrey Morris ambaye kwa sasa amestaafu, amesema: "Kwa nafasi ya beki wa kati, Bacca ni mzuri chini na juu, kukaba kwa miguu na kuruka mipira ya kichwa, anapanda na kushuka, msimu huu zikiwepo tuzo za mabeki naona anastahili kuipata."

Kipa wa Namungo FC, Deogratius Munishi 'Dida', amesema "Dogo (Bacca) amefanya kazi nzuri na endapo wakitoa tuzo na akapata atakuwa amestahili na anatoa chachu kwa vijana wengine kujituma kwa bidii."

Kipa wa KMC, Wilbol Maseke amesema: "Mabeki wapo wengi wanaofanya vizuri, ila kama ni kinyang'anyiro cha tuzo Bacca anapita, yupo kwenye ubora mkubwa."

Nahodha wa zamani wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' amesema: "Bacca yupo kwenye kiwango kikubwa, anachostahili kukionyesha hadi mwisho wa msimu na ikitokea akapata tuzo sitashangaa, kwani kafanya kazi kubwa."

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: