Wachezaji wawili wa soka wamepoteza maisha yao baada ya kupigwa na radi wakati wa mchuano huko Manyansi eneo bunge la Kitutu Chache, nchini Kenya.
Kwa mujibu wa Citizen Digital, kisa hicho kilitokea Jumamosi mwendo wa 4:30 wakati timu za Manyansi FC na Gianchore FC zilikuwa zikimenyana.
Jambo la kushangaza ni kwamba kila timu ilipoteza mchezaji mmoja kwenye kisa hicho ambacho kimezua huzuni.
Duru zinasema wawili hao walikuwa wakisakata kabumbu wakati radi ilipiga na kuwabeba bila huruma.
Waliripotiwa kufariki dunia papo hapo huku wenzao wawili nao wakifikishwa hospitali kwa matibabu.
Ni kisa kilichovuruga mchuano huo wa kirafiki uliokuwa umewavutia mashabiki wa soka.