Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachezaji wa Kitanzania wanaong'ara Ligi Kuu

Wazawa Pic Data Feisal Salum

Wed, 22 Dec 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Ligi Kuu Bara inazidi kushika kasi huku vita ikiendelea kutawala kwa timu na wachezaji kusaka rekodi na matokeo mazuri ili kujiweka pazuri kwenye msimamo.

Kwa sasa zipo baadhi ya timu zilizocheza michezo minane na nyingine zikisubiri ratiba, lakini kubwa zaidi ni msimu huu wazawa kuonekana kufanya vizuri tofauti na misimu mingine ya hivi karibuni.

Hata katika orodha ya wafungaji wazawa wameonekana kuwa juu ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo mara kadhaa wachezaji wa kigeni walikuwa wanangíara zaidi.

Gazeti hili limefuatulia kwa makini timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo na kukuletea baadhi ya nyota wazawa walioupiga mwingi hadi sasa na kuziweka salama timu zao.

JEREMIAH JUMA - PRISONS

Baada ya kucheza Ligi Kuu miaka 12, hatimaye mshambuliaji wa Prisons, Jeremia Juma amekuwa wa moto msimu huu na kuisaidia kuwa pazuri katika msimamo.

Juma ndiye kinara wa mabao akiwaacha wafungaji bora wa muda wote husasan nyota wa Simba na Yanga ambao mara kadhaa wamekuwa wakibadilishana mabao.

Msimu huu, Prisons haikuwa na mwanzo mzuri, lakini kufuatia kungíara kwa nyota huyo kumeifanya timu kujinasua mkiani na kupanda hadi nafasi ya nane.

Straika huyo amewaficha mastaa wanaocheza soka la kulipwa nchini na kuamsha ari kwa wachezaji wazawa kuwa na matumaini kuweza kuibuka wafungaji bora.

Pia ndiye staa pekee anayeshikilia rekodi ya kufunga mabao matatu ëhat trickí Ligi Kuu msimu huu aliyoitupia dhidi ya Namungo waliposhinda mabao 3-1.

VITALIS MAYANGA - POLISI TZ

Straika wa Polisi Tanzania, Vitalis Mayanga amekuwa na kiwango bora na kuipa heshima timu yake kwa kuwa na matokeo mazuri katika Ligi Kuu.

Vilevile ndiye mchezaji wa kwanza kufunga mabao manne na kuongoza kwa muda kwenye orodha ya wafungaji bora kabla ya kupinduliwa na Juma.

Kama haitoshi, Mayanga ambaye amezichezea timu kadhaa ikiwamo Ndanda na Kagera Sugar msimu huu ameuanza kwa kishindo huku akijihakikishia namba kikosini.

Ubora wake umeifanya Polisi Tanzania kuwa nafasi tano za juu ikiwa na pointi 11, lakini kuwa miongoni mwa timu zenye ushindani mkali.

CHRISPIN NGUSHI - MBEYA KWANZA

Nyota huyu ndio msimu wake wa kwanza kukipiga Ligi Kuu, lakini hakuna ubishi kwamba kiwango chake ni cha hali ya juu na amekuwa msaada mkubwa ndani ya timu.

Ngushi, kijana chipukizi amekuwa na kiwango bora hasa akiwa mchezaji mwenye kuamua matokeo muda wowote pindi timu yake inapokuwa nyuma kwa mabao.

Aliwahi kufanya hivyo wakati akiisaidia kusawazisha mabao mawili dhidi ya Mbeya City, huku bao lake la kideoni likiacha historia hadi sasa katika Ligi Kuu.

Nyota huyo mzaliwa wa Kyela mkoani Mbeya, tayari ametupia mabao matatu na kuiweka timu hiyo katika nafasi ya tisa, lakini pia akiwa miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kufanya makubwa msimu huu.

HANS MASOUD - COASTAL UNION

Ni beki mwenye mafanikio makubwa aliyeupiga mwingi akiisaidia timu yake kuwa sehemu salama katika msimamo wa Ligi Kuu.

Kama haitoshi ubora wake unatokana na uwezo aliouonesha nyota huyo wa zamani wa Alliance kufuatia kufunga bao moja, lakini kutoruhusu mabao mengi langoni mwao.

Coastal Union katika mechi saba imefungwa mabao mawili sawa na waliyofunga na kuifanya kuwa miongoni mwa timu zilizofungwa idadi ndogo ya mabao na kazi kubwa imefanywa na beki huyo.

FEISAL SALUM - YANGA

Ni moja ya nyota wanaoimbwa muda wote bila kujali ni kwa mashabiki wa Simba, Yanga au timu yoyote, kwani Feisal Salum ‘Fei Toto’ amekuwa na kiwango bora msimu huu.

Kiungo huyo mshambuliaji amekuwa na msaada mkubwa anapokuwa uwanjani, kwani mabao yake ya kideo anayofunga kwa mishuti nje ya 18 yamekuwa yakiiokoa Yanga.

Utakubaliana kwamba miongoni mwa mechi ambazo zilikuwa mfupa mgumu ilikuwa dhidi ya Ruvu Shooting ambayo iliwakamata vyema Yanga, lakini nyota huyo alifanya maajabu.

Shuti la umbali alilopokea kwa kifua na kunyoosha mguu hadi wavuni liliirejesha Yanga kwenye ari na morari na kuweza kushinda mabao 3-1 wakitoka nyuma bao moja na kusawazisha kisha kufunga mawili ya ushindi.

Hadi sasa kipenzi huyo wa mashabiki wa Yanga ndiye kinara wa mabao klabuni hapo na asisti akiwa amefunga manne na kutengeneza nne akiifanya timu yake kuwa kileleni kwa pointi 23.

GEORGE WAWA - DODOMA JIJI

Akiitumikia kwa msimu wake wa pili sasa Dodoma Jiji, beki George Wawa ameendeleza makali msimu huu na kuiweka sehemu nzuri timu yake.

Wawa ambaye alishuka na Singida United, kwa sasa ndiye beki wa kutegemewa katika kikosi cha kocha Mbwana Makata tangu alipotua msimu uliopita.

Beki huyo katika msimu uliopita alikuwa miongoni mwa wachezaji waliocheza mechi nyingi, huku akiwa kinara upande wa Dodoma Jiji alipocheza mechi 29 kati ya 36.

Pia, hata msimu huu staa huyo amekuwa kwenye kiwango cha juu akiendelea kuaminiwa na benchi la ufundi kutokana na kucheza mechi zote, ambapo timu yake imefungwa mabao matatu.

DENIS NKANE - BIASHARA UNITED

Licha ya kutajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wa ndani wenye umri mdogo, lakini winga wa Biashara United, Denis Nkane amekuwa na kiwango bora.

Nkane, licha ya kuwa na bao moja na asisti mbili, lakini amekuwa moja ya wachezaji wazawa walioupiga mwingi na kujihakikishia nafasi kikosini.

Winga huyo ambaye ni msimu wake wa tatu Ligi Kuu akiicheza Biashara United, amekuwa na mwenendo mzuri na kuwavutia wadau na mashabiki wengi zikiwamo Simba na Yanga.

Mbio, kasi na udambwi dambwi awapo uwanjani pamoja na chenga za maudhi vimekuwa vikimpa nafasi ya kuonyesha ubora na kuipa mafanikio timu yake.

Mbali na nyota hao, wengine walioonyesha viwango bora hadi sasa ni Shaban Msala (Ruvu Shooting), Mpoki Mwakinyuke (Mbeya City) na George Mpole (Geita Gold).

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz