Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachezaji vijana wapewe nafasi Ligi Kuu

Vijana Pic Wachezaji vijana wapewe nafasi Ligi Kuu

Wed, 23 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mtibwa Sugar haikuanza vizuri Ligi Kuu ya NBC msimu huu baada ya kupoteza mechi yake ya kwanza nyumbani dhidi ya Simba kwa mabao 4-2 katika Uwanja wa Manungu Complex, Alhamisi iliyopita.

Lakini pamoja na kupoteza mchezo huo, Mtibwa Sugar ilionyesha soka la kuvutia ikifanikiwa kutengeneza nafasi nyingi za mabao na kuliweka lango la Simba matatani mara kwa mara na kama safu yake ya ushambuliaji ingekuwa makini, pengine ingeweza kupata ushindi au sare katika mechi hiyo.

Jambo ambalo wengi liliwakosha ni Mtibwa Sugar kutumia wachezaji watano ambao wametokea katika kikosi chao cha vijana wenye umri chini ya miaka 20 ambao wote licha ya umri wao mdogo, hawakuonekana kubabaika mbele ya mastaa wa Simba na umati wa mashabiki waliojitokeza kutazama mchezo huo.

Wachezaji hao watano waliocheza juzi ambao wametokea katika kikosi cha vijana cha Mtibwa Sugar ni Nickson Mushi, Ladack Chasambi, Said Kazi, Omary Buzungu na Nasri Kombo.

Kitendo cha kocha Habibu Kondo kuwapa fursa vijana hao ni muendelezo wa Mtibwa Sugar ambao wamekuwa nao kila msimu wa kuingiza baadhi ya wachezaji wa kikosi chake cha umri chini ya miaka 20 kwenye kile cha wakubwa.

Miongoni mwa nyota wanaotamba katika soka hapa nchini ambao ni matunda ya utamaduni huo wa Mtibwa Sugar ni Dickson Job, Kibwana Shomari, Abuutwalib Msheri, Nickson Kibabage, Ismail Mhesa, Shiza Kichuya na George Chota.

Hii imekuwa ikiwasaidia Mtibwa Sugar kupunguza gharama za fedha ambazo wangezitumia iwapo nafasi zinazochezwa na vijana hao zingekuwa zinachezwa na wachezaji wanaosajiliwa kutoka tiu nyingi ambao huwa wanahitaji kiasi kikubwa cha fedha za usajili na mishahara.

Lakini pia faida nyingine ni klabu kuingiza fedha kupitia mauzo ya wachezaji hao kwenda timu nyingine, fungu ambalo linaisaidia katika shughuli za uendeshaji wa timu na masuala mengineyo.

Na hii ndio lengo halisi linalokusudiwa hadi kupelekea kuwekwa kwa kanuni inayolazimisha timu kuwa na kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 20 ili ipate leseni ya kushiriki katika Ligi Kuu kwamba wachezaji hao waje kuwa na msaada kwa kikosi cha wakubwa au ikishindikana wasaidie timu kupata fedha kupitia wao.

Bila shaka hiki kilichofanywa na Mtibwa Sugar kitakuwa chachu ya ushawishi kwa timu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu kuona umuhimu wa kutoa fursa kwa baadhi ya vijana kutoka katika timu zao za chini ya umri wa miaka 20 au hata chini ya umri wa miaka 17 ya kucheza baadhi ya mechi za vikosi vya wakubwa.

Kuna kundi kubwa la vijana ambao wana vipaji na wanaweza kuwa msaada kwa timu hizo ndani ya uwanja ingawa changamoto ambayo inawakabili ni uzoefu tu ambao ni rahisi kuupata ikiwa watakuwa wakipewa nafasi za kucheza.

Timu hazipaswi kuogopa kuwapa nafasi msimu huu na itakayoendelea ikiwa wanaonekana wana kitu kinachoweza kuwa na msaada kwa sasa au siku za usoni.

Iko mifano mingi ambayo roho ya uthubutu ya kuwapa nafasi wakiwa bado wapo kwenye vikosi vya vijana ilikuja kuzaa matunda hapo baadaye kwa klabu husika na hata timu ya taifa.

Wachezaji kama Said Ndemla, Jonas Mkude, Abdallah Seseme, Hussein Kazi, Ibrahim Ajibu, Manyika Peter, Iddi Kipagwile ni matunda ya uamuzi ambao Simba iliufanya kuwapa nafasi ya kucheza katika kikosi cha wakubwa kwenye kipindi ambacho walikuwa katika timu ya U20.

Azam FC ilifanya uthubutu wa kuwapa nafasi akina Aishi Manula, Sospeter Bajana, Yahya Zayd, Shaban Chilunda, Metacha Mnata na Masoud Abdallah ambao leo wamekuwa nyota wakubwa katika nchi kisoka.

Mfano mwingine ni mshambuliaji tegemeo la Yanga hivi sasa, Clement Mzize ambaye ni zao la kikosi cha vijana cha timu hiyo.

Iko mifano mingi ya nyota ambao walikuwa tegemeo kubwa la timu zao baada ya kupewa nafasi ya kucheza huku wakiwa katika vikosi vya vijana.

Msimu wa 2023/2024 una mechi nyingi za mashindano tofauti hivyo sio vibaya kwa makocha kufikiria kuwapa nafasi makinda wa timu zao za vijana ili waonyeshe kile walichonacho.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: