Wakati Kikosi cha Taifa Stars kikifanya maandalizi ya mwisho huko Misri kwa ajili ya mchezo wa Mzunguuko watatu wa Kundi F, kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ dhidi ya Uganda utakaopigwa kesho Ijumaa (Machi 24), nyota wa kikosi hicho wameapa kufanya kweli kwenye mchezo huo.
Uganda watakuwa nyumbani katika Uwanja wa Suez Canal mjini Ismailia-Misri, kabla ya timu hizo kucheza mchezo wa Mzunguko wa nne Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam Machi 28.
Taifa Stars ipo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi F ikiwa na alama moja nyuma ya Niger yenye alama mbili na Algeria inaoongoza ikiwa na alama sita, Uganda ambao ni wenyeji wa mchezo huu wanaburuza mkia wakiwa alama moja.
Kulingana na hali ya kundi, mshambuliaji wa Stars, Simon Msuva ambaye anacheza soka la kulipwa Saudi Arabia amesema watapambana kuibuka na ushindi k ili kuweka hai matumaini ya kwenda Ivory Coast.
Msuva alisema Stars ina wachezaji wenye uwezo wa kushindana na aina ya wapinzani ambao wapo kundi moja kwenye kinyang’anyiro hicho.
“Morali naona ipo juu.Kila mchezaji anaonekana kuwa tayari kutoa alichonacho kwa ajili ya mchezo. Mwalimu amekuwa akitufanya tujisikie raha kwenye programu zake mbalimbali za mazoezi. Naiona nafasi ya kufanya vizuri dhidi ya Uganda,” amesema Msuva
Naye nahodha wa kikosi hicho, Mbwana Samatta amesema Uganda wamekuwa wapinzani wagumu, lakini watakabiliana nao kwani michezo miwili dhidi yao imebeba hatma ya Tanzania.