Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachezaji Stand United hali tete, uongozi waiangukia Serikali

Stand United Wachezaji Stand United hali tete, uongozi waiangukia Serikali

Tue, 14 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Uongozi wa klabu ya Stand United ya Shinyanga umekiri kukabiliwa na ukata na kujiweka njia panda juu ya mustakabali wake kwenye Ligi ya Championship baada ya mdhamini wao, kampuni ya Jambo kusitisha huduma ghafla hivyo kusababisha wachezaji wa timu hiyo kutolipwa mishahara kwa miezi miwili huku wakitishia kugoma.

Timu hiyo ambayo imepanda daraja msimu uliopita, ikinolewa na Ally Kisaka inakamata nafasi ya 10 kwenye Championship ikivuna pointi 12 katika michezo 10, ikishinda mitatu, sare tatu na kupoteza nne, huku ikifunga mabao sita na kuruhusu nane.

Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Msaidizi wa Stand United, Fredy Masai amesema kutokana na changamoto za kibiashara inazopitia kampuni ya Jambo, mmiliki wake ameamua kusitisha huduma mbalimbali ikiwamo udhamini wa Stand United ikiwa ni jitihada za kutatua changamoto alizonazo, ambapo uamuzi huo wa ghafla umeiathiri kwa kiasi kikubwa timu yao iliyokuwa inajiendesha kwa udhamini huo.

Masai amesema klabu yao inategemea kwa asilimia kubwa kampuni hiyo kujiendesha mpaka sasa kwani ndiyo inalipa mishahara na posho za wachezaji, usafiri na chakula.

Masai amesema katika kukabiliana na hali hiyo ya dharura, uongozi umewasiliana na uongozi wa serikali ya mkoa, wilaya, wabunge na wadau wengine ambao mpaka sasa wametoa ahadi, huku akidai wako njia panda kama changamoto hiyo haitapata ufumbuzi kwani uendeshaji wa timu ni gharama kubwa ambapo mchezo mmoja wa ugenini hugharimu Sh8 milioni ambazo hawawezi kuendesha kwa kutembeza bakuli.

“Mpaka sasa wachezaji wanadai mishahara ya miezi miwili Septemba na Oktoba (tangu kuanza kwa ligi) hii imetokana na mdhamini kusitisha ghafla huduma zote baada ya matatizo ya kiuendeshaji yaliyotokea kwenye kampuni. Uongozi tumechukua hatua kadhaa kukabiliana na changamoto hii tumeongea na Mkuu wa Mkoa, DC (Mkuu wa Wilaya), mbunge na wadau wengine watusaidie,”

“Lakini kwa asilimia kubwa mpaka sasa ni ahadi tunaendelea kupambana tuone, lakini kiukweli hatuwezi kutegemea tu mchango wa serikali ya mkoa kuendesha timu kwa sababu safari moja tu kwenda kucheza nje ya mkoa ni kama Sh8 milioni, sasa serikali itatoa hiyo hela kila mechi?” amesema Masai

Hata hivyo, Ofisa habari wa timu hiyo, Ramadhan Zolo amesema mbali na udhamini wa jambo klabu yao kwa sasa haina chanzo kingine cha mapato zaidi ya kutegemea mapato ya mlangoni na mgao kidogo wa fedha za wadhamini wa Ligi ya Championship (NBC na TV3).

“Ni kweli tatizo lipo sababu kubwa ni mdhamini wetu jambo kusuasua hapo katikati kuna hali tu ya kibiashara kaipitia lakini sasa anashughulikia pamoja na uongozi kulimaliza, kwa upande wetu tunalifanyia kazi kuhakikisha wachezaji wanapata stahiki zao. Sisi kama uongozi tunakaa kutathimini madai ya wachezaji kuhakikisha kwamba madai yote yanashughulikiwa na hakuna anayedai,” amesema Zolo

Chanzo: Mwanaspoti