Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachezaji Simba wapewa ujanja

Ujanja Pic Data Wachezaji wa Simba wakiendelea na mazoezi

Sat, 30 Oct 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Wadau mbalimbali wa soka wamewapa ujanja wachezaji wa Simba kurudi kwenye mstari wa kuwajibika ipasavyo kama kweli wanataka kuitoa Red Arrow ya Zambia na kutinga makundi ya Shirikisho.

Kipa wa zamani wa Simba,Yanga na Taifa Stars, Steven Nemes alisema kichapo walichokipata dhidi ya Jwaneng Galaxy, kiwe somo kwa mastaa wa timu hiyo na akawataka wakaangalie marudio ya mchezo huo, ili kujua walipoangukia.

“Kwanza wachezaji wawe na tabia ya kuambiana ukweli inapotokea mmoja wao anafanya uzembe kwa lugha ya nidhamu, si kila kitu waambiwe na kocha wanapaswa kutumia utashi wao,”alisema Nemes na akaongeza kuwa;

“Simba bado inaiwakilisha Tanzania kupitia Kombe la Shirikisho Afrika, jambo la kwanza watengeneze saikolojia za wachezaji na kuwajengea morali, maana kikosi ni kile kile, viongozi waweke tofauti pembeni, kisha wauonyeshe ulimwengu kama wanaweza,”amesema.

Jambo lingine alishauri kila mechi Simba ichukulie kwa uzito kama wanavyocheza na TP Mazembe, Al Ahly na timu nyingine ngumu, anaamini wakifanya hivyo watawashangaza wengi Shirikisho.

“Timu yoyote inayocheza CAF, inapaswa iheshimiwe kwani inasimama kwa ajili ya kuwakilisha taifa lake, hicho pia kiliiponza Simba kutolewa mapema,”alisema.

Beki wa zamani wa timu hiyo, Godwin Aswile alisema; “Wachezaji wa Simba waondoe matabaka, wote wapo kwa ajili ya faida ya klabu na siyo maslahi binafsi, inasikitisha kuona mchezaji anapewa nafasi anaonyesha kazi dhaifu inayokuwa inamtafsiri hajitambui anachokitaka kwenye soka.”

“Makocha wakati mwingine wanabebeshwa mizigo mizito, ifike hatua mchezaji asiyefiti kwenye nafasi yake anakuwa hawafai kwenye kikosi, atafutwe atakayeitendea haki,Simba inakwenda Shirikisho hicho ni kipimo kingine kwa mastaa hao, maana mechi walioanguliwa ni uzembe wao na siyo kocha,”alisema.

Amesema anashangazwa kuona timu ilikuwa na jumla ya wachezaji 30, kuondolewa Clatous Chama na Luis Miquissone inaonekana kuyumba, wakati asilimia kubwa ya mastaa bado wapo.

“Zamani tulikuwa na wivu wa maendeleo ya kuonyeshana uwanjani, sasa sijajua hawa mastaa wa sasa wana wivu na vitu gani, kama kweli wapo kazini kwa nini wanaruhusu kuonyesha kwamba wao siyo bora, wajitafakari sana,”alisema.

Kauli yake iliungwa mkono na mchezaji mwingine wa zamani wa timu hiyo, Frank Kasanga ‘Bwalya’ aliyesema taswira ilivyo baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa, iwe fundisho kwa wachezaji kujitambua katika utendaji wao.

“Kilichotokea kimewashusha thamani, jambo ambalo si jema kwenye kazi yao, fursa waliyonayo kucheza Shirikisho waitumie kurejesha heshima yao, wajitume na kuwa wazalendo kwa timu,”Amesema.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz