Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachezaji Simba walia na Ratiba

Tshabalala Pic Data Mohammed Hussein ‘Tshabalala’

Sat, 7 May 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Kikosi cha Simba kimeingia kambini juzi mchana na jioni kilitarajiwa kujifua mazoezi ya kwanza ili kujaindaa na mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting, lakini mastaa wake wameilalamikia ratiba wakidai inawabana na kuwapa ugumu kufanya yao.

Nahodha Msaidizi wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ pamoja na Rally Bwalya na Kibu Denis kila mmoja, alichambua ugumu wa ratiba iliyopo mbele yao katika Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Tshabalala alisema mara zote timu inapokuwa inafanya vizuri katika michuano huwa ni lazima itakutana na ugumu kwenye michezo yao mingi iliyokuwa mbele yao.

“Tunafahamu ubora tulionao umekuwa sababu ya kukutana na ushindani wa kutosha msimu huu, ikiwamo ratiba ngumu ila haina jinsi kupambana kwa vile haiwezi kubadilishwa, tutashindana hadi mwisho kuona tulichokipata,” alisema Tshabalala.

Bwalya alisema ligi msimu huu imekuwa na ushindani wa kutosha timu walizokutana nazo zimeimarika ila wao walikuwa na changamoto ya kucheza mechi za mashindano mengine kila baada ya muda mfupi.

“Ugumu wa ratiba kila baada ya siku chache kucheza mechi ndani yake kuna nyakati tulikuwa tunatumia muda mwingi kusafiri, lazima kuna mahala wachezaji watakuwa na fatiki,” alisema Bwalya huku, Kibu Denis akisema; “Ugumu wa matokeo mazuri katika mechi za hivi karibuni naamini ni upepo mbaya tu umetupia ila licha ya ugumu wa ratiba uliyopo naimani tutafanya vizuri kwenye mechi za mbele.”

MSIKIE PABLO

Naye Kocha wa Simba,Pablo Franco alisema ndani ya mwezi huu wanatakiwa kucheza mechi kila baada ya siku tatu hadi nne kwa maana hiyo hawana muda wa kufanya mazoezi ya kutosha kwa ajili ya kile kilichotokea mchezo uliopita.

Pablo alisema kuna baadhi ya wachezaji hawapo fiti, kuna wengine wamechoka kwa kutumika zaidi ikiwemo uchovu wa kusafiri kwa umbali mrefu ila kuna njia atakazozifanya ili kuhakikisha wanafanya vizuri.

Alisema jambo la kwanza kutakuwa na mabadiliko ya mara kwa mara kwenye kikosi kuna baadhi ya wachezaji watakuwa wanaingia na kutoka hakuna wale watacheza mfululizo ili kuwapa muda wa kupumzika.

“Kama kuna mchezaji ilitokea huko nyuma alikuwa hapati nafasi ya kucheza mara kwa mara kulingana na ratiba yetu ilivyo ngumu hakuna ambaye atakaa bila ya kutumika kwa muda mrefu,” alisema Pablo.

Miongoni mwa wachezaji wanaoweza kupewa nafasi ya kucheza zaidi na hapo awali haikuwa hivyo ni, Gadiel Michael, Israel Mwenda, Kennedy Juma, Jimsony Mwanuke, Pater Banda na Yusuph Mhilu.

“Kila mchezaji anatakiwa kuishi kwa kutambua ugumu wa ratiba iliyopo mbele yetu, hatutakuwa na muda wa kufanya mazoezi zaidi ya kuweka miili sawa (recovery) kwa ajili ya mechi moja kwenda nyingine,” alisema Pablo na kuongeza;

“Haina jinsi kutokana ratiba ndio ilivyo tunatakiwa kupambana katika kila mechi iliyokuwa mbele yetu ili kumaliza msimu na kuona mwisho wa msimu tumemaliza na mafanikio gani kwenye mashindano yote.”

Chanzo: www.mwananchi.co.tz