Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachezaji Simba kufanyiwa kufuru, maajabu makubwa yaja Dar

Simba Sc Coach?fit=639%2C426&ssl=1 Wachezaji Simba kufanyiwa kufuru, maajabu makubwa yaja Dar

Thu, 20 May 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ ameweka wazi atawekeza mamilioni ya pesa katika kikosi hicho kinachopigania heshima ya Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mo Dewji kupitia akaunti yake ya Twitter baada ya Simba kupigwa mabao 4-0 na Kaizer Chief ugenini kwenye mechi ya awali ya robo fainali, aliweka wazi; “Nilipanga kujizawadia Ferrari na Rolls Royce, sina budi kuweka mpango huu kapuni kwa sasa na kuelekeza fedha zaidi katika klabu yetu ya Simba. Furaha ya Simba ni muhimu kuliko starehe yangu, Simba kwanza.”

Tathmini iliyofanywa na Mwanaspoti kwenye soko la Magari imebaini thamani ya magari hayo mawili ya kifahari aliyotaka kununua ni Sh1.3 Bilioni.

Ferrari ya kisasa ni Dola za Kimarekani 244, 000 (zaidi ya Sh578 Milioni). Rolls-Royce mpya inauzwa Dola 312,000 (zaidi ya Sh722 milioni) na kwa pamoja ni sawa na Sh1.3 Bilioni ambayo Mo Dewji amesema sasa ataiwekeza Simba ili kufanya vizuri ndani na nje.

BIL 1.3 NI NINI?

Mwanaspoti linakutafsiria maana halisi ya fedha hiyo kama Mwanasimba huyo ataamua kuiwekeza ndani ya klabu hiyo kwa kuanzia na mechi ya Jumamosi hii dhidi ya Kaizer kwenye Uwanja wa Mkapa saa 10 jioni.

MABAO MATANO

Kwa kipigo cha mabao 4-0 ugenini, Simba inahitaji ushindi wa mabao 5-0 kusonga mbele kwenye hatua ya nusu fainali.

Kama Mo ataamua kununua kila bao la ushindi tafsiri yake ni kila moja thamani yake itakuwa Sh 260 milioni.

Thamani ambayo huenda ikawa ni kubwa zaidi tangu aanze kuwekeza ndani ya klabu hiyo na haijawahi kutolewa kwenye soka la Tanzania.

DAKIKA

Kama akisema agawe Bil 1.3 kwa wachezaji wote wa Simba inamaanisha kila dakika wote watagawana Sh14.4 milioni mpaka mechi iishe.

WACHEZAJI WOTE

Simba ina wachezaji 27 wanaocheza Ligi ya Mabingwa Afrika. Maana yake ni kama wakishinda au akiamua kuahidi anaweza kuwaahidi Sh48 milioni kila mchezaji awe amecheza au hajacheza.

MAGARI MAPYA

Kwenye Sh1.3 Bilioni, Mo anaweza kutoa zawadi ya gari kali la kisasa aina ya Toyota Harrier New Model na chenji ikabaki ambayo itatosha kununulia kiwanja nje kidogo ya Jijini Dar es Salaam na maisha yakaendelea.

Harrier hiyo kwenye maduka mengi ya Dar es Salaam huuzwa Sh35 Milioni hivyo kuna uwezekano wa kubakiwa na Sh13 milioni ambazo kwa wazawa zitatosha kununulia kiwanja kidogo cha kuanzia maisha kilomita kadhaa nje ya Jiji.

USAJILI MPYA

Kama Mo akiamua kufanya kiburi hata kama Simba itateleza kwenye mechi ijayo anaweza kumsajili straika ghali wa Kaizer, Mserbia Samir Nurkovic. Thamani ya mchezaji huyo kwa mujibu wa mtandao wa kimataifa wa thamani za wachezaji duniani (transfermarkt) ni Sh.1.5 Bilioni pesa ambayo inazungumzika, hata kama Kaizer wakikomaa Mo atalazimika kuongeza Sh200 milioni.

MSIKIE GOMES

Akizungumza na Mwanaspoti jana, Kocha wa Simba, Didier Gomes alisema katika mechi ya marudiano amewaambia wachezaji wake ili wafuzu wanatakiwa kuwa katika kiwango bora zaidi ya walivyocheza ugenini na wasahau kila kitu.

“Naimani tutabadilika katika aina yetu ya uchezaji katika mechi ya marudiano na tutakuwa katika kiwango bora tofauti na mchezo wa kwanza,” alisema Gomes na kuongezea wataingia na mbinu za kushambulia zaidi kuliko kujilinda.

Kocha huyo alisema amewaambia wachezaji wake wapambane kibabe kwa masilahi ya Simba na taifa kwani walikotoka ni mbali kuliko wanakokwenda na wamefanya mengi makubwa dakika 90 zilizobaki zinahitaji akili na utulivu.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz