Kocha Mkuu wa FC Barcelona, Xavi amewajia juu mastaa wake kufuatia sare ya mabao 2-2 dhidi ya Real Mallorca kwenye mechi ya La Liga iliyochezwa Jumanne (Septemba 26).
Kocha huyo aliwacharukia wachezaji wake kutokana na makosa ya kizembe waliyofanya kwenye mchezo huo na kudondosha pointi mbili muhimu.
“Tulifanya makosa mengi, utoto ulikuwa mwingi sana. Lakini baadae tulirudi mchezoni, na kusawazisha kabla ya kwenda mapumziko, tukapata bao la pili.
Wachezaji walifanya makosa na sitaki kuona yakijitokeza tena. Tulitengeneza nafasi nyingi. Hata kama tulijua kwamba mechi itakua ngumu sana, tuliruhusu mabao kizembe ni makosa.
Tunatakiwa kuwa imara kwenye safu ya ulinzi. Kwa sababu hiyo tumepoteza pointi muhimu.” alisema Xavi
Licha ya sare Barcelona iliendelea kubaki kileleni kwenye msimamo wa La Liga kwa muda, lakini kwa sasa msimamo wa Ligi hiyo unaongozwa na Girona yenye alama 19, ikifuatiwa na Real Madrid yenye alama 18, huku Barca ikiporomoka hadi nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 17.
Hata hivyo kama Real Madrid ingechomoza na ushindi katika mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Atletico Madrid, ingekuwa kileleni kwa sasa, lakini hali imekuwa tofauti.
Kutokana na hilo Mkurugenzi wa zamani wa Real Madrid Pedja Mijatovic amekiri kikosi chao kina mapungufu, hasa baada ya kukubali kumuachia Karim Benzema aliyetimkia Saudi Arabia.
Mijatovic amekiri wazi kwamba watapata tabu bila ya Karim Benzema ambaye alitimkia Saudi Arabia.
“Hakuna mchezaji mwingine anayekaribia uwezo wa Benzema, unaposhindwa kuwa na takwimu kama zake, hapo kutakuwa na tatizo. Mechi muhimu kama Madrid dabi tumeona tulivyopata tabu. Hiki ni kipindi cha mpito.” amesema