KOCHA Antonio Conte amewaudhi mastaa wa Totteham Hotsputs kuafuatia kauli dhidi yao na taarifa zimedai hawamtaki kwenye timu. Kocha huyo amerejea Italia kwa ajili ya mapumziko mafupi kupisha mechi za kimataifa ambazo zitachezwa wiki hii.
Taarifa zinadai kuna uwezekano mkubwa mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy akamfukuza kazi Muitaliano huyo mwenye maneno mengi. Vilevile wapo mastaa ambao wangependa kuona anaondolewa kipindi hiki cha mapumziko ya mechi za kimataifa. Conte aliwaponda wachezaji wake akidai hawajitumi uwanjani.
“Wachezaji hawajitumi kabisa kwasababu hawaoni umuhimu wa mechi wanayocheza. Tottenham imezoea kucheza hivyo. Wachezaji hawapendi kucheza kwa presha. Kila mechi wanayocheza wanachukulia kawaida. Hii ndio historia ya klabu hii. Kila siku nawaambia nataka wachezaji wapambane, sio mazoezini tu hata uwanjani,” alisema Conte.
Wadau wa soka England wanajiuliza maswali kufuatia kauli hiyo wengi wakidai Conte ameikosea heshima klabu na hakupaswa kuzungumza hivyo. Spurs mara ya mwisho kubeba Kombe ilikuwa Carabao 2008.