Kocha Mkuu wa Azam FC, amewaonya mastaa wa timu hiyo huku akiwaambia kwamba ni lazima wajitafakari kutokana na matokeo walioyapata siku za karibuni katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mchezo uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ulishuhudia Azam FC ikipoteza alama tatu mbele ya Ihefu FC iliyochomoza na ushidni wa 1-0 katika Uwanja wa Highland Estate mkoani Mbeya.
Kipigo hicho kimeifanya Azam kutolewa rasmi kwenye mbio za Ubingwa msimu huu 2022/23, kutokana na michezo yake mitano iliyobaki kuwapa alama ambazo hazitawafikia vinara Young Africans wenye alama 65.
Endapo Azam FC yenye alama 47 kwa sasa, itashinda michezo yote iliyosalia itafikisha alama 62.
Kocha Ongala amesema: “Kilichotokea kwenye mchezo wetu uliopita tulikaa na wachezaji na kuzungumza nao na kuwaambia kwamba wanapaswa wajitafakari kutokana na kile ambacho kinatokea.
“Lakini muhimu zaidi ni kuwa na mwendo mzuri na kufanya yote kwa vitendo kwani tunaweza kuzungumza siku nzima na tusimalize,”
Azam FC jana Jumatano (Machi 22) ilicheza mchezo wa Kirafiki dhidi ya JKU ya Zanzibar katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam, na kufanikiwa kupata ushindi wa 2-0.
Timu hiyo pili ilikua na mpango wa kucheza mchezo mwingine wa Kirafiki dhidi ya Gor Mahia ya Kenya mwishoni mwa juma hili, lakini mchezo huo umefutwa kwa kuhofia hali ya usalama ya mjini Nairobi.