Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachezaji 12 tishio Ligi kuu Tanzania Bara

94366 Wachezaji+pic Wachezaji 12 tishio Ligi kuu Tanzania Bara

Wed, 5 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Si jambo rahisi kwa wachezaji wanaocheza timu tofauti na Simba, Yanga ama Azam kuteka hisia za mashabiki, wapenzi na wadau wa soka nchini.

Hali imekuwa tofauti kwa wachezaji 12 wa timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara ambao wamechomoza na kupigana vikumbo na wachezaji wanaocheza klabu hizo tatu kubwa nchini na kufanya majina yao kuwa gumzo katika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo unaoelekea ukingoni.

Kiwango cha kuvutia kilichoonyeshwa na wachezaji hao 12 katika idadi kubwa ya mechi za mzunguko huu, kimewafanya wajiweke katika nafasi nzuri sokoni siku za usoni.

Kasi ya kufunga mabao ya Paul Nonga, Daruwesh Saliboko wa Lipuli na mshambuliaji wa Kagera Sugar, Yusuf Mhilu ambao kila mmoja amefunga mabao manane imewafanya kuwa tishio kwa mabeki wa timu pinzani wakichagizwa pia na uwezo wao wa kufika haraka katika eneo la adui na kutengeneza nafasi timu zao zinaposhambulia.

Pia sifa za Nonga, Saliboko na Mhilu zimemfanya mshambuliaji wa Namungo Reliants Lusajo, kugeuka lulu katika kikosi hicho ambacho hadi sasa amefunga mabao saba katika Ligi Kuu na Waziri Junior wa Mbao FC ambaye amepachika sita.

Kitendo cha Gerrard Mdamu wa Mwadui kuifunga Simba mara mbili tofauti msimu huu, kimemuweka katika mazingira mazuri mchezaji huyo mwenye sifa ya kutokuwa na mzaha kwa nyavu za timu pinzani anapokuwa na mpira katika eneo la hatari.

Pia Soma

Advertisement
Mdamu aliifunga Simba katika mchezo wa kwanza ambao Mwadui ilishinda bao 1-0 mkoani Shinyanga Oktoba 30 kabla ya kupachika jingine katika mchezo wa hatua ya 32 bora ya mashindano ya Azam Sports Federation uliochezwa Januari 25 mwaka huu ambao timu yake ilipoteza kwa mabao 2-1.

Sadallah Lipangile wa KMC ambaye amekuwa moto wa kuotea mbali na kuirudisha timu yake kwenye mstari, amefunga mabao manne katika mechi nne ambazo timu hiyo imecheza mwezi Januari.

Wachezaji ambao wametikisa katika safu ya kiungo ni Lucas Kikoti (Namungo), Novatus Dismas (Biashara United) na Pato Ngonyani (Polisi Tanzania).

Uwezo wa Kikoti kuichezesha timu, kupiga pasi zinazofika kwa walengwa kwa usahihi, kutibua mipango ya viungo wa timu pinzani, kupika mabao na pia kufunga mabao vimemfanya azitoe udenda Simba, Yanga na Azam ambazo zimeanza kutazama uwezekano wa kumnasa wakati wa usajili wa dirisha kubwa.

Kikoti amefunga mabao matano yakiwemo mawili aliyozifunga Simba na Azam na ndiye amekuwa mpishi wa mabao ya Lusajo na Bigirimana Blaise.

Mshambuliaji mwenye umri wa miaka 19 anayecheza Biashara United, Novatus Dismas na Ngonyani wa Polisi Tanzania wameng’ara katika nafasi ya kiungo wa ulinzi.

Wachezaji hao wamekuwa msaada katika kuzipa uimara timu zao kwenye ulinzi kwa kuziba njia za wapinzani kupenyeza mipira kuingia langoni mwao, kupoka mipira na kuchezesha timu kuanzia nyuma, umezifanya Biashara na Polisi Tanzania kuzipa wakati mgumu timu pinzani katika kufumania nyavu zao.

Katika safu ya ulinzi majina yanayotikisa ni beki wa kati Coastal Union, Bakari Mwamnyeto na mlinzi wa kulia wa Mtibwa Sugar, Kibwana Shomari.

Mwamnyeto amekuwa mhimili wa safu ya ulinzi kutokana na uwezo wake wa kudhibiti washambuliaji wa timu pinzani unaochagizwa na utulivu na matumizi mazuri ya akili na nguvu jambo lililomfanya kuwa bidhaa adimu sokoni.

Kwa upande wa Shomari, kasi yake na matumizi mazuri ya akili imekuwa ikizipa taabu timu pinzani kwani amekuwa hapitiki kirahisi.

Mdamu alisema sababu kubwa ambayo imemfanya yeye na wenzake wafanye vizuri katika mzunguko wa kwanza ni kiu ya kupiga hatua zaidi.

“Unajua kwa kiasi kikubwa kila mchezaji ana ndoto na wengi wetu tumekuwa na malengo ya kufika mbali zaidi hasa kucheza soka la kulipwa nje ya nchi hivyo hilo haliwezi kutimia kama tutashindwa kufanya vizuri katika ligi,” alisema Mdamu.

Mawazo ya Mdamu yaliungwa mkono na Waziri ambaye aliongeza pia kwamba ushindani wa ligi umechangia kufanya kundi kubwa la wachezaji kuonyesha kiwango bora. “Ligi ni ngumu na kila mchezaji anataka kuisaidia timu yake ili ifanye vizuri badala ya kugeuka wasindikizaji. Lakini pia unapofanya vizuri unatengeneza mazingira mazuri ya kupata maslahi bora,”alisema Waziri.

Chanzo: mwananchi.co.tz