Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachambuzi hawapumziki jamani

IMG 4330.jpeg Wachambuzi wa masuala ya Soka

Sun, 18 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Msimu wa ligi umekwisha na watu wengi wa soka sasa wanaenda mapumziko kisha baadaye wataanza maandalizi kwa ajili ya msimu mpya.

Ila katika wadau wa soka, kuna kundi sidhani kama linapumzika aiseeh hadi unalionea huruma ambalo ni lile la wachambuzi.

Hawa wamekuwa na hekaheka katika kila siku iendayo kwa Mungu na hawapoi kiukweli wala kuwa na habari ya kuweka chini zana zao na kupumzika kidogo kama wenzao.

Wakati ligi inaendelea walikuwa na kibarua cha kutupa madondoo ya kile kilichokuwa kinatokea katika viwanja tofauti na kutupa uhondo wa mambo ya mbinu na kiufundi pasipo kusahau hesabu za makocha.

Sasa msimu umemalizika shughuli ya wachambuzi inahamia katika masuala ya usajili. Hapa bwana kuna kazi kwelikweli.

Kuna wachambuzi watageuka watoa tetesi za usajili, kuna watakaokuwa wanatoa tathmini ya wachezaji waliosajiliwa au kuachwa na kuna wengine watakuwa wanazisaidia timu kuzijulisha akina nani wa kuachwa na nani wa kusajiliwa.

Baada ya hapo mjiandae kusikia uchambuzi wa maandalizi ya msimu na mechi za kujipima nguvu kabla ya kuanza kwa ligi kuu na mashindano mengine katika msimu unaofuata.

Hapa napo ni pa kuwa makini napo maana kuna watu wanaweza wakamtangaza mchezaji bora katika msimu unaokuja au atakayechemsha kaa kumuona katika mechi za bonanza tu bila hata kujipa muda wa kumtazama zaidi katika mechi za ushindani.

Wakishamaliza na masuala ya maandalizi kwa ajili ya msimu mpya, hawatokuwa na muda tena aa kupumzika na kazi itarudi upya katika kutuchambulia mabao, visigino, kanzu, chenga, matobo, magoli yaliyokataliwa na marefa na vitu vingine kibao.

Kiufupi kwa wachambuzi hakuna kulala ndio maana nawakubali sana ingawa kuna baadhi yao huwa wanazingua.

Chanzo: Mwanaspoti