Uongozi wa Singida Big Stars umesema moja ya changamoto wanayoipata wachezaji wao wa kigeni kutoka Brazil, Bruno Gomes na Rodrigo Fegu, ni kutozoea kusafiri umbali mrefu.
Kocha Msaidizi wa Singida Big Stars, Mathias Lule, aliliambia gazeti hili wachezaji hao wanapata tabu sana wanaposafiri kwa umbali mrefu kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa ajili ya kwenda kucheza mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Lule alisema nyota hao bado hawajazoea hali hiyo na inawapa ugumu huku ikichangia kuathiri viwango vyao kutokana na uchovu wanaopata.
"Sisi Singida Big Stars hatugombanii nafasi yoyote katika Ligi Kuu Tanzania Bara, malengo tuliyojiwekea ni kucheza vizuri kupata matokeo chanya kwenye kila mchezo tunaocheza, lakini klabu haijaweka malengo wala kutuwekea makocha malengo, ila kwa jinsi tunavyokwenda tutafikia pazuri.
Ila tuna changamoto moja kwenye timu yetu, Wabrazil hawajazoea ligi ya Kitanzania, hapa tunasafiri sana tena umbali mrefu, kilomita nyingi kwao hawajazoea, hiyo imekuwa changamoto kubwa inayosababisha hata viwango vyao kupanda na kushuka," Lule alisema.
Kuhusu mechi hiyo, Lule alisema itakuwa ngumu kwa sababu Ihefu kwa sasa imepata ushindi mfululizo, hali ambayo imewajengea uwezo wa kujiamini wachezaji wake.
Singida Big Stars kwa sasa iko jijini Mbeya ikijiandaa na mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ihefu itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Highland Estates, Mbarali.