Wachezaji nane wa Kitanzania, wanatarajiwa kutimkia Ulaya wiki chache zijazo kwenye mataifa ya Moldova na Uturuki kwaajili ya kupigania ndoto zao za kucheza soka la kulipwa.
Wachezaji hao ni Paulo James, Mohamed Othman, Nassor Mbarouk, Salum Rashidi, Joseph Kimwaga, Laurent Haji, Mussa Mpwawa na Haroun ally Balhabou.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya African Youth Empowerment (AYE) , Muyimba Gerald ambayo imefanikisha upatikanaji wa nafasi hizo alisema wachezaji hao wataenda FC Sfintul Gheorghe Suruceni na Antalyaspor.
"Kila siku nimekuwa nikisema kuwa nafasi za wachezaji kucheza Ulaya zipo nyingi, hawa kilichobakia ni kusafiri kwa sababu kila kitu kipo sawa, tunaimani kuwa watakuwa mabalozi wetu wazuri wakiwa huko," alisema.
Hata hivyo, Muyimba alisema bado milango ipo wazi kwa wachezaji wengine kutokana na mpango ambao upo mbele yao wa kusaka vipaji,"Mwezi ujao tutaanza mchakamchaka mwingine wa kusaka vipaji kwa sababu timu zipo nyingi ambazo zinahitaji wachezaji wenye vipaji na Tanzania tumebarikiwa,"
"Tutapita mikoa mbalimbali na zoezi la usahili limeanza, tunatamani kuona wachezaji wengi wa Kitanzania wakipata nafasi ya kucheza Ulaya, tutatumia mtandao ambao tupo nao kuhakikisha wanapata timu."