Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabongo kucheza Ulaya mbona rahisi

Aisha Masaka Aisha Masaka

Tue, 14 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Yapo majina mengi ya wachezaji wa Kitanzania ambao wamecheza na wanaendelea kukipiga Ulaya, lakini sio wote ambao wamekuwa moto wa kuotea mbali kama ilivyokuwa kwa Sunday Manara ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa nyota wa mwanzoni kabisa kuipeperusha bendera ya taifa barani humo.

Mwaka 1976 wakati Yanga inaingia kwenye mgogoro na baadhi ya wachezaji nyota kuondoka kwenye timu hiyo, Manara alitimkia Uholanzi ambako alienda kuichezea timu ya Heracles kama mchezaji wa kulipwa.

Katika moja ya mahojiano yake na gazeti hili, Manara aliwahi kueleza mazingira ya kucheza soka la kulipwa Ulaya kwa kusema;

“Nilipata taabu kidogo na maisha ya Ulaya, kwa mimi mchezaji ambaye nimetoka Dar es Salaam na kwenda Ulaya kwa mara ya kwanza tena kucheza mpira kwa kweli mwanzoni nilisumbuka.

“Haikuwa rahisi kuzoea mazingira ya soka la Ulaya, aina ya ulaji wa wachezaji na hata tabia zao, siyo siri nilipata taabu hadi kuzoea hali hiyo na mimi kuwa kama wao.”

Mbali na Manara ambaye pamoja na changamoto mbalimbali alizokumbana nazo alitoboa na kufanya makubwa nchini Uholanzi hadi 1978 na kuondoka kwenda kuichezea klabu ya New York Eagles ya Marekani ambayo aliichezea mwaka mmoja na kutimkia Australia kwenye klabu ya Australian mwaka 1980, hawa hapa baadhi ya nyota wengine ambao wamechora ramani na wengine wanaendelea kupigania ndoto zao barani humo.

MBWANA SAMATTA

Pamoja na kwamba kwa sasa sio moto wa kuotea mbali lakini amefanya mengi makubwa akiwa Ulaya na kuweka rekodi kibao, ikiwemo kuwa mchezaji wa kwanza wa Kitanzania kufunga bao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na Europa Ligi.

Hakuishia hapo Samatta ambaye alijichotea umaarufu mkubwa barani humo kwenye kipindi chake cha kwanza cha kuichezea KRC Genk ya Ubelgiji, ni mchezaji wa kwanza kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki na kati kufunga kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Ligi kwenye Uwanja wa Wembley akiwa na Aston Villa dhidi ya Man City.

Licha ya kwamba Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu England ilipoteza Machi mosi, 2020 kwenye mchezo huo (2-1), Samatta aliwafanya Watanzania kufurahia bao lake na wala hawakuwa na simanzi ya kupoteza.

Awali aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza Mtanzania kucheza EPL baada ya kujiunga na timu hiyo.

Yapo mengi mazuri ya kuongea kuhusu Samatta ambaye amekuwa chachu ya vijana wengi kuona kumbe inawezekana kucheza ligi kubwa na kufanya vizuri kwa leo itoshe kusema kuwa huyu ni shujaa wa Kitanzania na hakika jina lake litakumbukwa.

KELVIN JOHN

Jarida moja nchini Uingereza lilitoa orodha ya wachezaji wa kutazamwa ambao wanaweza kuwa gumzo kwa miaka michache ijayo, jina la Kelvin lilikuwa moja ya vijana hao, ukubwa wa kipaji chake kiliifanya KRC Genk fasta kufanya maamuzi ya kumsajili kwa mipango yao ya baadae.

Bado hajaanza kukiwasha mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza cha KRC Genk lakini kile alichokifanya akiwa na timu yao ya vijana ni balaa tupu.

Mshambuliaji huyo kinda, mwaka jana, 2022 alicheza Ligi ya Mabingwa Ulaya upande wa vijana chini ya miaka 19 na kufanya vizuri, miongoni mwa michezo aliyong’ara ni dhidi ya Chelsea na alitoa asisti ya bao moja kwenye ushindi wa 5-1.

Kwa sasa Kelvin ambaye yupo kikosi cha kwanza cha KRC Genk amekuwa akipewa shavu la kukipiga na vijana wenzake chini ya miaka 21 ili kuwa na nafasi ya kucheza michezo mbalimbali ya ushindani, kwenye mechi 11 amefunga bao moja na asisti tatu.

NOVATUS DISMAS

Ndiye mchezaji wa Kitanzania ambaye kwa sasa anafanya vizuri kwenye ligi ya Ubelgiji ‘Jupiler Pro’ kuliko yeyote akiwa na Zulte Waregem. Amekuwa akiaminiwa na kupata nafasi ya kucheza wiki baada ya wiki kwenye michezo mbalimbali ya ushindani.

Tumezoea kuona akitumika kama kiungo mkabaji kwenye timu ya taifa na hata pale ambapo alikuwa akicheza Ligi Kuu Bara akiwa na Biashara na hata Azam FC lakini huko Zulte Waregem anacheza kama beki wa kushoto.

Anafanya vizuri kwenye nafasi hiyo na katika michezo 22 aliyocheza kwenye ligi ametoa asisti mbili, ameonyeshwa kadi za njano tano na nyekundu moja.

AISHA MASAKA

Yupo mbioni kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kike wa Kitanzania kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa Wanawake, hilo linawezekana ikiwa itaendelea kupambana na kujihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza cha BK Hacken.

Ugeni na majeraha ni miongoni mwa changamoto ambazo alikumbana nazo kwenye msimu wake wa kwanza lakini sasa anaonekana kuwa fiti kuhakikisha anapeperusha bendera ya Tanzania kwenye soka la Wanawake nchini Sweden.

HARUNA MOSHI ‘BOBAN’

Anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wa Kitanzania waliokuwa na vipaji vya kipekee, hata wakati ambao umri ulimtupa mkono bado Mwinyi Zahera alihitaji huduma yake kwenye kikosi cha Yanga kabla ya kutundika kwake daruga.

Japo alicheza kwa kipindi kifupi na kuamua kurejea zake nyumbani Tanzania lakini aliacha gumzo huko Sweden ambako alikuwa akiichezea Gefle. Changamoto za Ulaya ziliwafanya Wazungu wasikifaidi kipaji chake.

HENRY JOSEPH

Akiwa kwenye ubora wake ilikuwa ngumu kwake kuchukua mpira ukiwa mguuni, alijua kukata umeme na kuchezesha timu.

Henry aliichezea Kongsvinger ya Norway kwa miaka minne na kufunga mabao matatu na kutoa asisti tatu kwenye michezo 95 ya mashindano yote ambayo ni Ligi Kuu ‘Eliteserien’, OBOS-ligaen na NM-Cup.

WENGINE

Wakali wengine wa Kitanzania walioliamsha na wanaoendelea kuliamsha Ulaya ni pamoja na Renatus Njohole, nyota wa zamani wa Milambo na Simba aliyepiga nchini Uswisi akianza kuwika Yverdon Sports kabla ya kupita Fc Valmont, Fc Baulmes, Fc Le Mont na Fc Bavois.

Yupo pia Athuman Machupa, mtoto wa Friends Rangers aliyekipiga Simba na Malindi kabla ya kwenda Sweden na kuzichezea klabu kama Vasalund na Vasby United na kusalia huko huko hadi leo akiungana na Watanzania wenzake, Shekhan Rashid na Joseph Kaniki.

Chanzo: Mwanaspoti