Mgaagaa na upwa hali wali mkavu tuliambiwa hivyo na wahenga na ngoma imekuwa hivyo kwa timu zilizokuwa zikipambania nafasi ya kutinga hatua ya nusu fainali. Hatimaye kila timu imevuna chake huku kazi ikipigwa na wachezaji wa timu zote ndani ya dakika 90 kusaka ushindi.
Hapa tunakuletea namna kazi ilivyokuwa kwa wababe hawa kusaka ushindi na rekodi tofauti ambazo zimeandikwa katika hatua hii. Ikumbukwe kwamba mabingwa watetezi wa taji hili ni Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi:-
SUPER SUB Kuna mastaa ambao walikuwa wanaanzia benchi kisha wanabadili matokeo ndani ya uwanja katika mechi za hatua ya robo fainali.
Pape Sakho wa Simba kwenye mchezo dhidi ya Ihefu alitokea benchi dakika ya 75 akichukua nafasi ya Saidi Ntibanzokiza akapata nafasi ya kufunga bao moja kwenye mchezo huo.
Kwa upande wa Yanga ni Fiston Mayele yeye alitokea benchi mchezo dhidi ya Geita Gold dakika ya 45 akichukua nafasi ya Clement Mzize akapachika bao dakika ya 57.
ATHARI ZA MAPIGO HURU Nyota wa Singida Big Stars, Bruno Gomes kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City alipachika mabao mawili na moja kati ya hayo alipiga kwa pigo huru dakika ya 6 akiwa nje kidogo ya 18 likazama mazima nyavuni ikiwa ni athari ya mapigo huru.
Clatous Chama wa Simba kwenye mchezo dhidi ya Ihefu alitoa pasi mbili za mabao na moja kati ya hiyo ilitokana na pigo la faulo dakika ya 2 ilikutana na mtupiaji Jean Baleke aliyeuzamisha mpira nyavuni.
Never Tigere wa Ihefu, pigo lake la faulo dakika ya 61 lilikutana na mtupiaji Rafael Daud ambaye alimtungua kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula.
KADI NYEKUNDU Nyota wa Azam FC, Daniel Amoah dakika ya 21 alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kuonekana akimchezea faulo Charles Ilanfya, mshambuliaji wa Mtibwa Sugar.
Jeofrey Makasi nyota wa Geita Gold alionyeshwa kadi mbili za njano kwenye mchezo dhidi ya Yanga ile ya dakika ya 47 ilimfungashia virago ndani ya uwanja kwa kuonyeshwa kadi nyekundu.
HAT TRICK Ni nyota wa Simba, Jean Baleke kasepa na mpira kwenye hatua ya robo fainali alipowatungua Ihefu kwenye mchezo wa hatua ya robo fainali Uwanja wa Azam Complex.
Alifanya hivyo dakika ya 2, 15 na 27 akasepa na mpira wake na hakuyeyusha dakika 90 kwenye mchezo huo alimpisha Mohamed Mussa.
MABAO MENGI Mchezo uliokusanya mabao mengi ni Simba 5-1 Ihefu na kufanya jumla mchezo huo kukusanya mabao sita ndani ya dakika 90.
Singida Big Stars 4-1 Mbeya City, huu ulikusanya jumla ya mabao matano kwa mastaa hao waliokuwa wakisaka nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali.
Azam FC 2-0 Mtibwa Sugar ni mabao mawili yalikusanywa huku mchezo wa funga kazi hatua ya robo fainali ubao wa Uwanja wa Azam Complex ulisoma Yanga 1-0 Geita Gold.
KAZI IPO Yanga ambao ni mabingwa watetezi watamenyana na Singida Big Stars na Azam FC itakuwa dhidi ya Simba kwenye mechi za hatua ya nusu fainali.
WABABE WANAKUTANA Yanga iliwanyoosha Sigida Big Stars kwenye mchezo wao wa ligi walipokutana Uwanja wa Mkapa mabao 4-1, Simba mchezo wake wa kwanza kupoteza ndani ya ligi msimu huu imetunguliwa na Azam FC bao 1-0 na mtupiaji akiwa ni Prince Dube.
Ule wa mzunguko wa pili ngoma ilikuwa 1-1 wababe hawa wanakutana kuulizana maswali mengine ndani ya uwanja.