Ligi Kuu England imetimiza umri wa miaka 31. Ndani ya muda huo, Manchester United, Chelsea, Arsenal, Liverpool, Tottenham na Everton pekee ndizo zilizobaki kwenye ligi hiyo hadi sasa.
Kwa ujumla wake, kuna klabu 50 tofauti zimechuana kwenye Ligi Kuu England tangu ilipoanzishwa mwaka 1992 na hakuna jina jingine jipya tangu Brentford ilipopanda mwaka 2021 – licha ya kwamba Luton Town itaongeza jina lake kwenye orodha hiyo kwa kuanzia msimu ujao.
Kwa kuzingatia klabu zote zilizowahi kucheza kwenye Ligi Kuu England, hii hapa orodha ya zile 20 zilizokusanya pointi nyingi, zilizotumikia misimu mingo kwenye ligi hiyo pamoja na wastani wa pointi kwa msimu na hivyo kupata idadi ya timu hizo 20 zilizofanikiwa zaidi kwenye mchakamchaka huo wa Ligi Kuu England.
Pointi zote 1992-2023
Licha ya kwenda misimu saba bila ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England, Manchester United ipo kileleni kwa pointi za jumla, ikiweka pengo la pointi 223 kwenye msimamo wa muda wote, huku Arsenal ikiwa ni timu nyingine pekee iliyovuka pointi 2000. Chelsea na Liverpool wanakamilisha ile Big Four ya awali iliyozoeleka kwenye ligi hiyo kabla ya kuibika kwa Big Six.
Timu nane katika orodha hiyo ya 20 bora ya muda wote kwenye Ligi Kuu England hazitakuwapo kwenye msimu wa 2023-24, huku Bolton Wanderers ikipambana na hali yake huko kwenye League One na timu nyingine tatu zilizoshuka daraja msimu huu, Leeds United, Leicester City na Southampton ambazo zitakuwa kwenye Championship msimu ujao.
Kati ya klabu 50 zilizoshiriki Ligi Kuu England, 43 zilifanikiwa kuvuka pointi 100 kwenye ligi hiyo, huku Brentford ikiwa timu ya mwisho kufikisha idadi hiyo.
Msimamo wenyewe unavyosoma na pointi zao
1. Man United – 2,441 2. Arsenal – 2,225 3. Chelsea – 2,182 4. Liverpool – 2,109 5. Tottenham – 1,847 7. Man City – 1,718 6. Everton – 1,610 8. Newcastle – 1,481 9. Aston Villa – 1,419 10. West Ham – 1,298 11. Southampton – 1,088 12. Blackburn – 970 14. Leicester – 821 13. Leeds United – 820 16. Fulham – 692 15. Middlesbrough – 661 15. Sunderland – 618 19. Crystal Palace – 609 18. Bolton – 575 20. West Brom – 490
Misimu waliyotumikia Ligi Kuu England
Kuna timu sita tu ndizo zilizoshiriki kwenye misimu yote 31 kwenye Ligi Kuu England. Nje ya timu hizo sita, kuna timu mbili Aston Villa na Newcastle United ambazo zilitumikia misimu minne nje ya Ligi Kuu England na hivyo zenyewe kuwa kwenye ligi hiyo kwa misimu 28.
Miamba mingine, timu nane – Southampton, Blackburn, Sunderland, Fulham, Leicester, Bolton, Leeds na West Brom – zilicheza Ligi Kuu England, zikashuka kwenye Championship, zikashuka tena hadi kwenye League One na zaidi ya hapo, lakini zenyewe ni miongoni mwa timu zilizokusanya pointi nyingi kwenye rekodi zao za Ligi Kuu England.
Misimu kwenye Ligi Kuu England
31 – Man United, Chelsea, Arsenal, Liverpool, Tottenham, Everton 28 – Aston Villa, Newcastle United 27 – West Ham 26 – Man City 24 – Southampton 18 – Blackburn 17 – Leicester City 16 – Fulham, Sunderland 15 – Leeds United, Middlesbrough 14 – Crystal Palace 13 – Bolton, West Brom
Pointi nyingi kwa msimu
Top Four kwenye msimamo huu inarudia orodha ileile ya timu zilizokusanya pointi nyingi, lakini Manchester City imeiengua Tottenham kwenye nafasi ya tano. Baada ya Spurs wanafuata Leeds United, ambao walikuwa kwenye kiwango bora sana mwanzoni mwa miaka 2000, huku Blackburn, Newcastle na Brentford zikikamilisha 10 bora.
Wimbledon kiwango chao matata kabisa walichokionyesha kwa misimu minane imewafanya waingia kwenye orodha ya timu zilizokuwa na wastani mzuri wa kuvuna pointi nyingi ndani ya msimu mmoja na kuzipiku timu kama za Southampton na Fulham.
Wastani wa pointi nyingi kwa msimu 1. Man United – 78.74 2. Arsenal – 71.77 3. Chelsea – 70.39 4. Liverpool – 70.19 5. Man City – 66.08 6. Tottenham – 59.58 7. Leeds United – 54.67 8. Blackburn – 53.89 9. Newcastle – 52.89 10. Brentford – 52.50 11. Everton – 51.94 12. Aston Villa – 50.68 13. Sheffield Wednesday – 49.00 14. West Ham – 48.07 15. Wimbledon – 46.75 16. Nottingham Forest – 46.17 17. Stoke City – 45.70 18. Coventry City – 45.44 19. Brighton – 45.17 20. Charlton Athletic – 45.13
Timu zilizobeba ubingwa
Kwa ujumla, kwenye klabu 50 zilizowahi kucheza Ligi Kuu England, saba tu ndizo zilizofanikiwa kubeba ubingwa wa ligi hiyo. Miamba hiyo saba ni Manchester United, Chelsea, Manchester City, Arsenal, Blackburn Rovers, Leicester City na Liverpool.
Kwenye ile Big Six, Tottenham pekee ndiyo haijawahi kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England.
Mabingwa wenyewe
-Man United - 13 -Man City - 6 -Chelsea -5 -Arsenal - 3 -Blackburn Rovers - 1 -Leicester City - 1 -Liverpool - 1