Kocha wa timu ya Kakamega Homeboyz Patrick Odhiambo ametuma salamu kwa Al Hilal ya Libya watakapomenyana kesho katika ugani Nyayo mjini Nairobi.
Mechi hiyo ya Kombe la Mashirikisho Afrika (CAF), itakuwa ya kwanza kwa Homeboyz tangia kujiunga na Ligi Kuu ya Wanaume ya Shirikisho la Soka nchini (FKF-PL).
"Tumefanya maandalizi vizuri na kila mtu amejitayarisha vilivyo. Wachezaji wengi ni wazoefu kwenye mashindano haya, wachache tu ndio wageni na wote kwa pamoja wataelekezana kuandikisha matokeo mazuri," Odhiambo aliambia Mwanaspoti.
"Tutakuwa nyumbani mbele ya mashabiki kwa hivyo lazima tujitume. Hali ya anga tumeizoea na tutaitumia vilivyo. Tumesoma wapinzani wetu tunajua wanavyo cheza ingawaje wamefanya mabadiliko kwenye timu," aliongezea Odhiambo.
Odhiambo ambaye ni kocha wa zamani wa Sony Sugar na Biashara United ya Tanzania aliwahi kucheza dhidi ya Al Hilal alipokuwa akiipigia klabu ya Gor Mahia.
Walipata nafasi yao kwa kuibuka washindi dhidi ya wanamvinyo Tusker FC kwa kushinda 1-0 katika fainali ya kombe la Mozzart Bet Cup nja kujikatia tiketi ya moja kwa moja kushiriki mashindano ya CAF.
"Tulijifunza mengi ambayo tumeyafanyia kazi uwanjani. Uwanja huu tumeuzoea kwa kuwa tumepata alama tatu mara si moja. Vijana najua wataamka vizuri na wako tayari kuwakilisha taifa," alisema nahodha wa Homeboyz Farouk Shikhalo. Baada ya mkondo wa kwanza, wataelekea Libya kucheza mkondo wa pili wa raundi ya kwanza ya Jumapili, Agosti 27, 2023.
Mshindi kwa jumla baada ya mechi zote mbili atafuzu kwa raundi ya pili ya mashindano hayo na kukutana na Rayon Sport (Rwanda).
Hii ni mechi ya kwanza Kenya inakuwa mwenyeji baada ya kuondolewa adhabu ya kufungiwa na Fifa.