Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waamuzi wanalea madhambi Ligi Kuu

Waamuzi Madhambi Waamuzi wanalea madhambi Ligi Kuu

Wed, 27 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mchezo wa Ligi Kuu ya NBC kati ya Simba na Coastal Union, jioni ya Septemba 21, ulishuhudia mchezaji wa zamani wa Simba, Haji Ugando, akimfanyia madhambi makubwa beki wa Simba, Henock Inonga. Ugando alioneshwa kadi nyekundu. Mechi za ligi zimekuwa na ubabe mwingi sana ambao waamuzi wanashindwa kuuchukulia hatua aidha kwa uwezo wao mdogo wa kutafsiri sheria au kwa makusudi.

Utakuta mchezaji anafanya madhambi mara tatu mfululizo, hachukuliwi hatua yeye binafsi kwa aidha kuonjwa kwa kadi ya njano au kutolewa kabisa.

Kwa mfano, kwenye Ngao ya Jamii kule Tanga. Kwenye mchezo wa ufunguzi wa Azam FC na Yanga, Mudathir Yahya wa Yanga alimfanyia madhambi manne Feisal Salum wa Azam ndani ya dakika 20 za kwanza, na mwamuzi hakutoa kadi.

Waamuzi wana miongozo yao inayowasaidia kupima madhambi na kutoa kadi. Siyo kila madhambi yanastahili kadi...mengine huishia kupuliwa filimbi tu na mengine onyo la mdomo.

Lakini mchezaji anapofanya madhambi mfululizo, hata kama ni madogomadogo, anatakiwa kuonywa kwa mdomo na akirudia, aonyeshwe kadi. Takwimu zinazotumika kwenye makala haya ni za Bodi ya Ligi kutokana na ripoti za waamuzi wa michezo husika.

IHEFU 0-1 GEITA GOLD

Jumla ya matukio 33 ya madhambi yalifanyika kwenye mchezo huu, huku Geita Gold ikiongoza kwa kuyafanya mara 19, na Ihefu mara 14. Mwamuzi Ally Mnyupe kutoka Morogoro alitoa kadi tano za njano, moja kwa Ihefu iliyoangukia kwa Geogrey Manyasi ambaye alicheza madhambi mara nne. Mara tatu za kwanza zote mwamuzi alimsamehe, hadi mara ya nne ndiyo akamuonesha kadi ya njano.

Ukishangaa ya Manyasi utayaona ya Elius Maguri wa Geita Gold. Mwamba alifanya madhambi mara sita lakini hakuoneshwa kadi, hadi alipofanyiwa mabadiliko dakika ya 85.

Katika madhambi haya sita, Maguri alistahili njano angalau moja, kama mbili zilishindikana japo kimsingi kuna madhambi matatu ambayo yalistahili za njano, japo timu yake ilipata kadi nne za njano.

NAMUNGO 0-1 JKT TZ - MADHAMBI 17

Uwanja wa Kassim Majaliwa Mjini Ruangwa ulishuhudia madhambi 17 yakifanyika, huku wenyeji Namungo wakiyafanya mara saba na wageni JKT Tanzania mara 10.

Mwamuzi Thabit Maniamba alitoa kadi nne za njano, moja kwa wenyeji Namungo, iliyoangukia kwa mkongwe Jacob Massawe, tatu kwa wageni JKT Tanzania, ikiwemo moja kwa Maka Edward ambaye aliipata baada ya kufanya madhambi matatu, na ndiye aliyekuwa kinara wa madhambi kwenye mchezo. Hapa kwa Maka mwamuzi alifanya kama inavyostahili. Maka alifanya madhambi mara mbili, akaonywa kwa mdomo (tumemalizana), aliporudia akaonywa kwa kadi.

DODOMA JIJI 2-1 COASTAL UNION

Mchezo mwingine uliojaa ubabe katika siku ya ufunguzi wa msimu. Jumla ya madhambi 40 yalirekodiwa kwenye kitabu cha mwamuzi Emmanuel Mwandembwa. Wenyeji Dodoma Jiji walifanya madhambi mara 24 huku wageni Coastal Union wakifanya mara 16. Jumla ya kadi za njano nane zilitoka, sita kwa Dodoma Jiji na mbili kwa Coastal Union. Kinara wa madhambi alikuwa Raizin Hafidh wa Dodoma Jiji na Miraji Hassan wa Coastal Union ambao walifanya madhambi mara tano kila mmoja lakini wote hawakuoneshwa kadi yoyote.

MTIBWA 2-4 SIMBA SC

Jumla ya madhambi 21 yalifanyika katikati ya mashamba ya miwa kule Manungu. Mwamuzi Nassor Mwinchui kutoka Tanga alionesha kadi nne za njano, ikiwemo moja pekee kwa Simba iliyoenda kwa Jean Baleke, lakini kwa kufunga goli la ujanja ujanja.

Kelvin Nashon wa Mtibwa alifanya madhambi mara nne na kuoneshwa kadi moja ya njano!

SINGIDA BIG STARS 0-0 TZ PRISONS

Mchezo mwingine uliojaa ubabe na kushuhudia wanaume 22 wakifanyiana undava mara 23.

Chilo Mkama wa TZ Prisons peke yake alifanya madhambi mara sita na kuambulia kadi moja ya njano katika jumla ya kadi za njano mbili za mchezo huo ambazo zote zilienda kwa Tanzania Prisons.

Kadi nyingine ilienda kwa Edwin Balua dakika 64. Mwamba huyu angeweza kutolewa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja mnamo dakika ya tisa kwa madhambi yake mabaya kwa Gadiel Michael wa Singida Fountain Gate lakini alinusurika. Baada ya njano yake ya dakika ya 64, akafanya tena madhambi dakika ya 77, akanusurika.

YANGA 5-0 KM

Kwenye ushindi wa 5-0 dhidi ya KMC katika mchezo wake wa kwanza msimu huu, jumla ya faulo 28 zilirekodiwa kwenye kitabu cha mwamuzi Omary Mdoe kutoka Tanga.

Mudathir Yahya alifanya madhambi mara tano lakini alitoka salama bila hata kadi moja. Katika faulo hizo, nne zilifuatana; dakika ya 21, 29, 31 na 39. Katika dakika hizo, hakukuwa na mchezaji mwingine aliyefanya madhambi. Yaani ni kama mpira ulisimama kupisha shoo ya Mudathir, akawa anawatimba tu...mara nne mfululizo.

Mudathir alipaswa kuonywa kwa kadi ya njano kwa madhambi yote haya mfululizo...lakini aliachwa. Hii ndiyo faida anayokutana nayo akiwa Yanga. Alipokuwa Azam FC, Mudathir alikuwa akichafua kitabu cha waamuzi kwa jina lake kuandikwa kwenye orodha ya waliooneshwa kadi.

Ilikuwa kawaida kwa Mudathir kukosa mchezo wa ligi kwa kutumikia adhabu iliyotokana na kadi tatu za njano. Lakini sasa hivi anafurahia tu maisha. Anafanya madhambi yale yalealiyokuwa akiyafanya akiwa azam FC, lakini waamuzi hawamuoneshi kadi!

Jumla ya kadi mbili za njano zilitoka kwenye mchezo huu, zote zikienda kwa KMC.

IHEFU 1-0 KAGERA SUGAR

Idadi ya kadi 21 za njano zilizozaliwa kwenye mchezo huu siyo ya kushtua sana ukizingatia kuna mechi nyingi zilizozaa kadi nyingi zaidi ya hizi. Lakini kitu cha tofauti ni kwamba kuna miamba miwili kwenye mchezo huu waling’ara sana kwa madhambi.

Dickson Godian wa Kagera Sugar aliyefanya madhambi mara tano, na Juma Nyosso wa Ihefu aliyefanya madhambi mara sita.

MTIBWA SUGAR 1-1 COASTAL UNION

Madhambi 30. Kelvin Nashon wa Mtibwa Sugar alitoka na madhambi matano peke yake, huku Yassin Salum akifanya madhambi mara tatu mfululizo mnamo dakika za 36, 40 na 41. Khatib Kombo wa Coastal Union naye alifanya madhambi mara tatu...lakini hawa wote hawakutoka na kadi, japo mchezo huu ulizalisha kadi mbili za njano!

SIMBA 2-0 DODOMA JIJI

Jumla ya madhambi 23 yalizalishwa kwenye mchezo wa Simba na Dodoma Jiji. Japo hiyo idadi ni kubwa lakini hakukuwa na wachezaji wakorofi waliorudia rudia mara nyingi madhambi. Ni Mwana David pekee wa Dodoma Jiji ndiye aliyefanya madhambi matatu katika mchezo huu uliozalisha kadi mbili za njano zilizoenda kwa Dodoma Jiji, lakini siyo kwa Mwana David.

YANGA 5-0 JKT TANZANIA

Jumla ya madhambi 26 yalifanyika katika mchezo huu ulioshuhudia timu zikigawana sawa madhambi hayo.

Yanga ilifanya madhambi 13 kama ilivyokuwa kwa JKT Tanzania. Khalid Aucho wa Yanga na Hassan Dilunga wa JKT ndiyo walikuwa vinara wa madhambi, kila mmoja akifanya mara tatu.

Mwamuzi Ahmed Arajiga wa Manyara alitoa kadi nne za njano, moja ikienda kwa kinara wa madhambi upande wa JKT, Hassan Dilunga, huku kinara wa yanga, Khalid Aucho akitoka salama.

KMC JKT TANZANIA

Licha ya kushuhudia madhambi 35, mchezo huu pia ulishuhudia kadi nyekundu ya kwanza ya msimu iliyoenda kwa Masoud Abdallah ‘Cabaye’ wa KMC. Cabaye alikula umeme dakika ya 90+4 baada ya kuoneshwa njano ya pili, njano ya kwanza aliipata dakika ya 54. Zao hilo la akademi ya Azam FC, halikutishwa na kadi kwani alicheza kibabe na kuhatarisha uwepo wake mchezoni, katika dakika za 67, 74 na 83. Mwamuzi Abdul Wajihi kutoka Tanga alimvumilia sana hadi dakika ya mwisho ndipo uvumilivu ukamshinda na kumtoa.

DODOMA JIJI 1-1 MTIBWA SUGAR

Kelvin Nashon wa Mtibwa akiwa katika siku yake nzuri kwa madhambi, aliyafanya mara sita kwenye mchezo huu ulioshuhudia madhambi 41, lakini hakupata hata kadi moja.

Katika dakika za 4, 9, 12, 20 Kelvin Nashon alitamba yeye tu kwa madhambi.

Kituko alikuwa Meshack Abraham ambaye alifanya madhambi matatu bila kadi, lakini akaja kupata kadi kwa kubishana na mwamuzi baada ya kuushika mpira.Mtenje Albano wa Dodoma Jiji naye alifanya madhambi mara nne na akatoka salama.

KAGERA SUGAR 1-0 GEITA GOLD

Huu ni ule mchezo uliovunjika siku ya kwanza kutokana na umeme kukatika. Jumla ya madhambi 33 yalirekodiwa na Mwamuzi Shomari Lawi kutoka Kigoma, na kadi tatu za njano ambazo zote zilienda Geita Gold. Godian Dickson wa Kagera Sugar alifanya madhambi matano, yakiwemo matatu mfululizo.

Ally Ramdhan agawa wa Kagera Sugar anaye alifanya madhambi mara tatu mfululizo, dakika ya 54, 57 na 67 lakini hakuonywa.

HITIMISHO

Unapoona Ugando anampanda Inonga namna ile, usidhani kijana yule ana roho mbaya ya kutaka kumuumiza wenzake, hapana.

Ni matokeo ya udhaifu wa waamuzi wetu ambao wamekuwa wakikwepa kutoa adhabu kwa wachezaji wanaofanya madhambi.

Hizi kadi huwakumbusha wachezaji kuwa makini uwanjani, zisipokuwa zinatoka huwafanya wacheze bila hofu. Ni sawa na dereva anayezidisha mwendo bila kuhofia tochi. Waamuzi wausaidie mpira wetu.

Chanzo: Mwanaspoti