Katika kuhakikisha kila siku wanatatua changamoto katika nyanja ya Mpira wa miguu nchini, Mamlaka zinakuja na mafunzo kwa wote wanaohusika na soka kwa namna moja ama nyingine.
Kila wakati katika baadhi ya michezo ya Ligi kuu ama madaraja mengine kumekuwa na malalamiko dhidi ya waamuzi, na hivyo ili kutatua kama si kumaliza tatzo hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya waamuzi Tanzania (FRAT) Sudi Abdi, amewataka waamuzi kuzingatia sheria 17 za soka msimu mpya utakapoanza.
Chama hicho kinaendesha semina katika Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), lengo likiwa ni kutoa elimu na kuwajengea uwezo mkubwa waamuzi nchini.
“Msimu uliopita hapakuwa na malalamiko sana kwa waamuzi wetu, jambo ambalo tunazidi kulifanyia kazi ili kuhakikisha kama sio kumaliza basi tunapunguza,” alisema.
Aliendelea kuwa kwa sasa wanachokifanya ni kuwafundisha waamuzi kufahamu mabadiliko ya sheria ya kuotea, kitu ambacho bado kimekuwa ni tatizo kubwa.
“Matatizo yaliyopo ni ya kibinadamu ambayo hayazuiliki ila kumekuwa na maendeleo mazuri jambo ambalo linaonyesha mwanga huko mbeleni,” alisema.
Abdi alisisitiza kuwa hadi kufikia tarehe rasmi ya Ligi kuanza kila kitu kitakuwa sawa huku akiwataka kuzingatia umuhimu wa semina hiyo kwa kujifunza na kuzingatia sheria kwa manufaa ya Ligi yetu.
Ligi Kuu Tanzania Bara itazinduliwa Septemba 25, kwa mechi ya Ngao ya Jamii ambayo itawakutanisha wapinzani wa jadi, Simba dhidi ya Yanga.