Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waamuzi waaanza kuelezea uamuzi wa VAR kwa mashabiki

Mexico V Russia Group A FIFA Confederations Cup Russia 2017 Waamuzi waaanza kuelezea uamuzi wa VAR kwa mashabiki

Tue, 7 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Teknlojia ya mwamuzi msaidizi wa video maarufu kwa jina la VAR ilianza kutumiwa na Ligi Kuu ya England katika msimu wa 2019/2020.

Hata hivyo, nchi ya kwanza kuanza kutumia teknolojia ya VAR in Ureno katika mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake kati ya Sporting CP na SC Braga. Baada ya kutumika katika ligi hiyo, Australia katika Ligi Kuu ya nchi hiyo ilianza mwaka 2017.

Nchi hiyo ilianza kutumia VAR kuanzia Aprili 7, 2017 katika mchezo wa Ligi Kuu uliozikutanisha timu za Melbourne City na Adelaide United. Machi 2018, baada ya majaribio kadhaa ya matumizi ya VAR, Bodi ya Kimataifa ya Soka (IFAB) iliingiza teknolojia hiyo kwenye sheria 17 za soka na miezi mitatu baadaye ilianza kutumika kwenye mashindano ya Kombe la Dunia yaliyofanyika Russia.

Kwa upande wa Afrika, nchi ya Morocco iliweka historia kwa kuanza kutumia teknolojia hiyo 2019 katika ligi ya ndani baada ya kupitishwa na IFAB.

Morocco ambao kwa sasa ni kama washindi wa nne wa Kombe la Dunia, pia wameweka historia kwa kuandaa michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia ambayo kwa sasa inashika kasi katika miji ya Rabat kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah na Batouta uliopo mji wa Tangier.

Nimeanza kuzungumzia historia fupi ya VAR ili kuwapa picha halisi wasomaji wa safu hii hasa baada ya hatua ya Fifa na IFAB kuongeza kipengele cha waamuzi kufafanua uamuzi wa VAR mara baada ya kufanya uamuzi katika mchezo husika.

Kipengele au kazi hiyo ilizinduliwa katika michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia inayoendelea nchini Morocco na tayari mashabiki wa soka wameanza kupata uelewa wa uamuzi kadhaa mpaka sasa.

Historia iliandikwa katika mchezo kati ya Al-Alhy dhidi ya Auckand City ambapo Al Ahly ilishinda kwa mabao 3-0.

Katika mchezo huo, beki wa Auckland City FC, Adam Mitchell alimfanyia faulo winga wa Al Ahly, Taher Mohamed nje kidogo ya eneo la penalti.

Katika uamuzi wake, mwamuzi Ma Ning wa China awali aliamua iwe ni penalti dhidi ya Auckland City. Hata hivyo baada ya kufanya marejeo kupitia televisheni ya pembeni ya uwanja (pitch side monitor) alibadili uamuzi huo na kuwa ‘free kick’ huku Mitchell akitolewa nje ya uwanja kwa kadi nyekundu.

Baada ya uamuzi huo, mwamuzi alielezea uamuzi huo kupitia kipaza sauti (PA system) kuwa, “uamuzi utakuwa free kick, mchezaji aliyevaa namba tatu wa Auckland alifanya faulo ya kumzuia mchezaji wa Al Ahly nafasi kufunga.”

Hata hivyo, ufafanuzi huo wa mwamuzi ulikuwa kwa ufupi sana tofauti na matarajio na alifanya hivyo kwa sababu mbalimbali za kiufundi.

Mojawapo wa sababu hiyo ni kuepuka ucheleweshwaji wa mchezo husika ambao ungesababisha kuongeza muda mwingi wa mchezo baada ya dakika za kawaida, yaani dakika 90.

Mapokeo

Mashabiki wa soka waliohudhuria mechi hiyo walipata uelewa wa uamuzi huo na sababu ya kadi nyekundu kwani Mitchel alikuwa beki wa mwisho na hivyo alistahili kadi nyekundu kwa mujibu wa sheria 17 za soka.

Hakukuwa na mapokeo hasi kwa hatua hiyo ya mwamuzi kwani hilo bado lipo katika majaribio na litafanyiwa maboresho zaidi kadri siku zinavyokwenda.

“Hatudhani kuwa mashabiki wa soka wanapata ufafanuzi wa kutosha kutoka kwa mwamuzi. Bado tunafanyia majaribio japo yanawaweka waamuzi katika mazingira magumu,” alisema ofisa mtendaji wa FA ya England.

Kwa upande wake, mwamuzi wa zamani wa EPL, Peter Walton alisema mashabiki wanatakiwa kuelewa zaidi utendaji kazi wa VAR. Walton anasema mashabiki wanatakiwa kuelewa uamuzi wa VAR kwani wanaotoa uamuzi wa mwisho wapo kwenye chumba maalumu kwa kushirikiana na mwamuzi wa kati.

“Mashabiki wanatakiwa kupata maelezo ya kina na kujua uelewa wa sheria mbalimbali zitokanazo na matukio ya faulo uwanjani. Maboresho zaidi yanatakiwa ili kuondoa utata au tatizo hili,” anasema.

Chukua hii

Ili uwanja wa soka uwe na haki ya kuchezewa mechi ya mashindano inayotambuliwa na Fifa, shirikisho la bara na nchi husika ni lazima uwe na urefu wa kati ya mita 90 hadi 120 na upana kati ya mita 45 hadi 90.

Ndio maana baadhi ya viwanja kama cha Mkapa kinaonekana ni kikubwa, lakini kile cha Azam Complex ni saizi ya kati.

Chanzo: Mwanaspoti