Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waamuzi wa ligi yetu watabadilika lini?

Tatu Malogo Refa Mwamuzi Tatu Malogo

Sun, 4 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kumekuwa na mijadala mingi kuhusu waamuzi wanaochezesha ligi zetu. Mijadala ilikolezwa na kitendo cha kukosa hata mwamuzi mmoja katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zinazoendelea nchini Ivory Coast.

Lilikuwa ni jambo la kushtua kukosa waamuzi kwenye Afcon? Hapana! Ni jambo ambalo wengi walitarajia. Ndio sababu kubwa kumekuwa na mjadala.

Waamuzi wetu wamekuwa kwenye ubora mdogo sana kwa siku za karibuni. Wenye nafuu wanahesabika. Wengi wanafanya baadhi ya uamuzi wa ovyo kwenye mechi za Ligi Kuu Bara na ligi za madaraja ya chini.

Bahati mbaya ni kwamba wanaboronga katika nyakati hizi ambazo mechi zote za ligi ziko mbashara. Kila kitu kipo hadharani.

Yawezekana madudu haya yalikuwepo kwa kiwango kikubwa tangu zamani, lakini mambo yalikuwa gizani.

Walifanya madudu na yakafunikwa tu huko huko gizani.

Leo ni tofauti. Kosa analofanya mwamuzi linaonekana wazi kwenye luninga. Wachambuzi wako macho kweli kweli. Dakika chache tu utaliona jambo hilo kwenye mitandao ya kijamii.

Zamani hakukuwa na Instagram, Twitter wala Tiktok. Kwa sasa ni tofauti. Zamani watu wangeweza kuona tukio na wakose sehemu ya kusemea, ila leo dunia iko huru.

Dakika chache tu mbele kina Jemedari Said, Wilson Oruma na wengineo watakuwa wamechapisha madudu hayo mitandaoni. Hakuna siri tena.

Kinachoshangaza ni kwamba pamoja na utandawazi wa sasa, kwanini waamuzi bado wanafanya makosa mengi? Inafikirisha sana. Ni kama huyu aliyekataa bao halali la Kagera Sugar dhidi ya Yanga juzi.

Aliwaza nini kusema mchezaji wa Kagera Sugar aliotea? Picha za marudio zinaonyesha hakuwa ameotea. Na sheria iko wazi. Kama huna uhakika muache aliyenufaika anufaike. Ukikataa na ikawa bao halali kama vile inaumiza sana.

Hebu fikiria namna Kagera Sugar inajikongoja katika uwekezaji wake. Inaishi katikati ya mashamba ya miwa. Inasajili kwa shida. Inasafiri kwa shida. Lakini wamenyimwa bao halali kabisa. Inaumiza sana.

Kwanini waamuzi wetu wanafanya makosa yaleyale kila siku? Yawezekana hawana uwezo wa kumudu mechi.

Hawafahamu vizuri sheria ama wanafanya makusudi? Kila moja inaweza kuwa ni sababu.

Mfano Khalid Aucho alimpiga kiwiko Ibrahim Ajibu pale Tanga. Mwamuzi Emanuel Mwandembwa akaona. Akatoa kadi ya njano badala ya nyekundu. Kwanini alifanya hivyo wakati sheria iko wazi kama ni faulo ya namna ile nje ya eneo la hatari ni kadi nyekundu ya moja kwa moja? Hakuna anayejua.

Huyu ni Mwandembwa. Mwamuzi mwenye uzoefu mkubwa. Amechezesha ligi kwa miaka mingi. Anafahamu kitu sahihi na ambacho si sahihi. Kwanini alifanya vile?

Unapotoa kadi ya njano sehemu ilipostahili nyekundu maana yale ni kwamba uliyaona madhambi ila umeshindwa kutafsiri sheria ya adhabu. Ndio sababu Mwandembwa alifungiwa.

Ni kama yule mwamuzi msaidizi aliyekataa bao halali la Azam FC dhidi ya Yanga pale Tanga. Haukuwa mpira wa kuotea. Mchezaji wa Azam wala hakuwa karibu na eneo la kuotea. Kwanini alifanya vile? Pia mwamuzi mwingine aliinyima Azam bao dhidi ya Dodoma Jiji. Kisa nini? Anajua mwenyewe.

Mwamuzi mwingine alikataa bao halali la Simba dhidi ya Kagera Sugar. Kuna mwingine alifanya kituko mechi

ya Namungo na KMC mwanzoni kabisa mwa msimu huu. Ni kichefu chefu.

Kwanini waamuzi wanafanya hivi? Wanajua wenyewe.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi wanajaribu karibu kila kitu kupambana na tatizo la waamuzi lakini ni kama limekuwa sugu.

Kama ni mafunzo wanatoa ya kutosha. Kama ni mitihani wanatoa ya kutosha. Kama ni adhabu wanaotoa za kutosha. Hata hivyo, wakirudi uwanjani wanafanya madudu yaleyale. Mfano kuna mwamuzi anaitwa Amina Kyando. Alifungiwa muda mwingi msimu uliopita. Akakaa nje ya uwanja kwa muda mrefu. Aliporejea msimu huu akaanza kuboronga tena vilevile. Tena mapema tu kwenye Ngao ya Jamii pale Tanga. Kisha baadaye akavurunda zaidi.

Mwamuzi kama huyu unajiuliza kwanini anafanya makosa ya mara kwa mara? Inaumiza sana.

Kwa namna waamuzi wetu wanachezesha ligi, bado kuna safari ndefu sana ya kufikia kiwango cha kuchezesha Afcon ama mashindano mengine makubwa.

Katika ubora wake Jonesia Rukya alijitahidi sana. Akateuliwa kuchezesha mechi za fainali ya Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (Wafcon) tena mara mbili. Akateuliwa kwenye fainali za Mataifa ya Afrika chini ya umri wa miaka 17 zilizofanyika nchini 2019. Akawa mwamuzi wa kwanza mwanamke kuchezesha mechi za wanaume kwenye mashindano rasmi ya CAF. Ni historia.

Kabla ya hapo aliteuliwa kwenye orodha ya waamuzi wa awali kuchezesha Kombe la Dunia kwa Wanawake. Alikuwa vizuri sana.

Bahati mbaya akapata changamoto za kiafya na kukaa nje kwa muda mrefu. Aliporejea bado anajitafuta hadi sasa.

Yule Frank Komba aliteuliwa kwenye Afcon U-17 ya mwaka 2017 na 2019. Akateuliwa tena kwenye mashindano mengine ya CAF. Hii ni kwa sababu ya umakini wake kazini. Wengine vipi? Ni Mungu anajua.

Ila ukweli lazima usemwe. Waamuzi wengi wako kwenye kiwango cha chini sana. Wanatakiwa kupunguza makosa yao uwanjani. Wanatakiwa kupandisha ubora wao. Vinginevyo mashindano haya makubwa wataishia kuyatazama kwenge televisheni tu, wakati enzi hizo kina Leslei Liunda, Nassor Hamduni na Omary Abdulkadir walikuwa wakituibeba kimataifa.

Chanzo: Mwanaspoti